TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

RPC GEITA:WANANCHI WASIMAMIE ULINZI KWA WATOTO WAO KUZUIA UKATILI

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Geita ACP Henry Mwaibambe akitoa salaam za Jeshi la Polisi kwenye maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani, kimkoa kwa Geita maadhimisho hayo yamefanyika 16Mei,2022

Salum Maige,Geita.

Serikali ikiwa kwenye utekelezaji wa program jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya Awali yamtoto(PJT – MMMAM) kuanzia mtoto wa miaka 0 – 8 katika masuala ya Afya, Lishe, Malezi, Makuzi na Ulinzi kwa mtoto ,Jeshi la polisi mkoani Geita limewataka wananchi kuwa walezi bora wa watoto katika misingi ya maadili ambayo haitaleta migogoro na utumiaji wa madawa ya kulevya.


Wito huo umetolewa na kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita,Bw.Henry Mwaibambe kwenye maadhimisho ya kimkoa ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyo fanyika Mei 16,2022 kwenye ukumbi wa bwalo la polisi mjini Geita yakiwa yameratibiwa na Klabu ya waandishi wa habari Mkoani humo GPC.

Mwaibambe alisema,ulinzi wa mtoto ni mnyororo kuanzia mimba hadi kujifungua na kuendelea hadi kusoma lakini mtoto anapolelewa na wazazi na walezi bila kuzingatia misingi mizuri husababisha kundi la watu wenye tabia mbaya ukiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya na uhalifu.

Alisema,kwa mwaka huu anakesi nne za watoto chini ya miaka 18 wakituhumiwa kuwa na tabia mbaya za utumiaji wa madawa ya kulevya na miongoni mwao wapo wanatumia hadi sindano huku wazazi wao wakidai watoto wao wanasoma na wanatabia nzuri.

Aidha,katika suala la ulinzi na usalama kwa watoto aliwataka wananchi kuwalinda watoto dhidi ya watu waharifu kutokana na sababu zisinzo na msingi wa jambo linalohatarisha usalama na maisha ya watoto.

Kauli hiyo ya Kamanda wa Polisi inakuja kufuatia matukio ya watoto sita ya kulawitiwa,kubakwa,kuibiwa,kushambuliwa na fisi hadi kufariki dunia na mwingine kufariki kwa kutupwa ndani kisimani chenye kina kirefu muda mfupi baada ya kuzaliwa yaliyotokea Januari hadi Aprili mwaka huu.

Matukio hayo ni pamoja Mariam Samweli(21)mkazi wa Katoro aliyekamatwa jeshi hilo akituhumiwa kuiba mtoto aliyefahamika kwa jina la Pendo Adrian aliyekuwa na umri wa miezi mitatu.

Mwanamke huyo alikamatwa Februari 16,mwaka huu katika kijiji cha Bwanga wilayani Chato siku chache baada ya mtoto huyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha Januari 29,mwaka huu muda mfupi baada ya mama yake mzazi Vaileth Masumbuko kumuacha mwanae na watoto wenzake na kwenda kuchota maji.

Pichani ni Bw David Azaria (Kushoto) mwanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Waandishi wa Habari kwa Mgeni rasmi na kwa wadau wote waliohudhuria sherehe ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani kimkoa katika Mkoa wa Geita


Tukio la kuibiwa kwa mtoto huyo lilifuatiwa na tukio la Februari 17 ,mwaka huu la mtoto ambaye hakufahamika jina lake aliyekadiliwa kuwa wa siku moja kukutwa ametupwa ndani ya kisima cha maji akiwa amefariki Dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa huko katika kijiji cha mkolani Wilaya ya Geita.

Alifafanua kuwa februari 16,mwaka huu huko katika kijiji cha Izunya wilaya ya Nyang’hwale mtoto Mariam Mateso(5)alifariki kwa kuliwa na fisi aliyemnyakua nyumbani akiwa anaota joto la moto na watoto wenzake.

Katika tukio la kusikitisha ni watoto watatu wa familia moja ambao walibakwa na kulawitiwa na ndugu yao wa ndani ya familia na kuwasababishia maumivu makali sehemu za siri.

Hivi karibuni alinukuliwa kamanda Mwaibambe kwamba kuhusiana na mkasa huo alisema,ukatili waliofanyiwa watoto hao ni ndani ya familia na jamii ambao ulibainika baada ya watoto kushindwa kujisaidia haja zote kutokana na maumivu.

“Kuna watoto watatu anawafanyia ukatili wa kingono, siku ya kugundulika kwa tukio hilo mwanafunzi mmoja aliingia chooni kujisaidia katika Shule ya Msingi Bukolii akashindwa kutokana na sehemu ya haja kubwa ilikuwa imeharibika na wanafunzi wenzake walikuwa wakipiga kelele mbona hautoki chooni ili waingie, hadi mwalimu alipofika akaingia akakuta mwanafunzi huyo akiwa kwenye maumivu makali.”

Alisema jeshi la polisi halitakubali kuona ukatili huu unaendelea katika jamii,hivyo aliwataka waandishi wa habari kuwa msitari wa mbele kufichua ukatili huo na kwamba jeshi la polisi litaendelea kutoa ushikiano kwao ili kuwa na jamii yenye maadili na kuzuia matukio kama hayo.


“Wazazi na walezi jitahidini kuwakagua watoto wenu wa kike na wa kiume ili kugungua kama wamefanyiwa ukatili wa kingono, mnahangaikia na biashara zenu tu pamoja na VIKOBA hamwangalii maendeleo ya watoto wenu.”

"Polisi tunategemea sana waandishi wa habari katika shughuli zetu ifahamike  polisi haiwezi kuficha taarifa nawaomba wandishi wawe sehemu ya usalama wa nchi kwa kulipoti matukio sahihi kwa kushirikiana na jeshi la polisi mfano mjamzito abakwa au ajinyonga kwa kukosa nguvu za kiume nimambo ambayo hayana umuhimu sana", alisema Mwaibambe.

Aliongeza kuwa,waandishi wakifanya na wakitimiza majukumu yao ipasavyo ukatili huo unaweza kupungua au kuumaliza kabisa.

Kwa Upande wake Mgeni Rasmi wa Maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule aliyewakalishwa na mkuu wa wilaya ya Bukombe Bw.Said Nkumba alisema serikali inatumiza wajibu wake kwa kuwepo kwa vyombo vya habari kwani serikali haiwezi kuwafikia wananchi wote kwa wakati mmoja.

“Nitumie nafasi hii kuwataka waandishi wa habari tufanye kazi zetu kwa kufuata maadili yetu,na nipende kuwafahamisha kwamba sisi serikali tuko pamoja nanyi katika majuku yenu,hata hili lililozungumza na viongozi wenzangu akiwemo kamnada wa polisi tuone namna ya kukomesha unyama huu wa kikatli”alisema Nkumba.

Mkuu wa wilaya ya Bukombe Mhe.Said Nkumba akitoa hotuba kwenye sherehe ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani kimkoa katika Mkoa wa Geita 16Mei,2022

Kwa upande wake Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita(Geita Press Club – GPC) Bw.Renatus Masuguliko aliahidi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kutoa taarifa za kufichua matukio mbalimbali ya uharifu yakiwemo ya ukatili dhidi ya watoto pamoja shughuli za maendeleo zinazofanywa na serikali kwa wananchi.

Aliyesimama ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita Be Renatus B.D. Masuguliko akitoa salaam kwa wadau wa habari waliohudhuria kwenye sherehe ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani kimkoa katika Mkoa wa Geita leo 16Mei,2022

Aidha,kwa mujibu wa taarifa ya ukatili wa Kijinsia ya jeshi la polisi nchini inonyesha kuwa kwa mwaka mmoja matukio ya ukatili yaliongezeka kutoka matukio 15,680 kwa mwaka 2019 hadi matukio 15,870 kwa mwaka 2020,na katika kipindi cha miezi 9 kuanzia januari hadi septemba ,2021 jumla ya matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa 6,168.

MWISHO.


Post a Comment

0 Comments