![]() |
Viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita kwenye picha ya pamoja na Maofisa kutoka Ubalozi wa Sweden |
Na. Theresia C. Method - Geita
Machi 12, 2025 – Maofisa kutoka Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania wametembelea Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita (GPC) leo kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012.
Meneja wa Miradi ya Haki za Binadamu, Utawala Bora, na Asasi za Kiraia, Stephen Chimalo, amepongeza maendeleo makubwa yaliyofikiwa na GPC tangu ziara yake ya mwisho mwaka 2018.
"Nawapongeza sana. Mara ya mwisho nilikuja hapa 2018, na sasa naona mabadiliko makubwa na yenye kuleta ushawishi mkubwa. Kazi mnazofanya ni nzuri, na ni muhimu kuendelea kufuata miongozo kama hii mliyonionyesha," amesema Chimalo.
Aidha, Afisa Fedha wa Ubalozi wa Sweden, Juliana Monyo, amepongeza GPC kwa kuzingatia uwazi na uadilifu katika usimamizi wa fedha zake.
"Nimefurahi kuona GPC inafuata mfumo wa matumizi ya fedha kwa uwazi na utaratibu wa kiuhasibu. Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya kwa kufuata kanuni za fedha," amesema Monyo.
![]() |
Viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita kwenye picha ya pamoja na Maofisa kutoka Ubalozi wa Sweden |
Afisa Mahusiano wa Ubalozi wa Sweden, Belinda Japhet, amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa na maeneo maalum ya kitaaluma katika uandishi wao ili kuongeza weledi na kuimarisha ubora wa habari wanazoandika.
"Ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa na maeneo maalum wanayobobea. Hii itawasaidia kuandika kwa kina, kwa weledi, na kuleta mabadiliko chanya katika jamii kupitia kazi zao," amesema Belinda.
Katika ziara hiyo, GPC iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli zake kuanzia mwaka 2012 hadi 2024, ikionyesha maendeleo, mafanikio, na changamoto zilizopo.
Afisa Ubalozi kutoka Sweden, Stephen Chimalo, pia amesisitiza umuhimu wa GPC kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha juhudi zake katika kuendeleza tasnia ya habari na utawala bora katika mkoa wa Geita.
Ziara hiyo imeacha alama chanya kwa GPC, huku maofisa wa ubalozi wakiahidi kuendelea kushirikiana na klabu hiyo katika juhudi zake za kiutendaji.
Mwisho
0 Comments