TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

VITA YA VIPAUMBELE GEITA MJINI: NANI ANA MCHORO WA KWELI WA MAENDELEO?

Na Victor Bariety – Geita


Picha: Baadhi ya wagombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Geita Mjini kupitia CCM

Wakati dirisha la kuchukua na kurejesha fomu ndani ya CCM kwa ajili ya kuwania Ubunge wa Geita Mjini likiwa limefunguliwa rasmi, hali ya kisiasa imeingia kwenye hatua ya pili—vita ya vipaumbele. Sio tena nani ana mashabiki wengi au konvoy kubwa, bali nani anajua anachotaka kufanya kwa wananchi wa Geita.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Geita, Bw. Michael Msuya, jumla ya watia nia 18 wamejitokeza. Lakini kwa jicho la wachambuzi wa siasa na mitazamo ya wananchi mitandaoni, mapambano ya kweli yako kati ya waliowahi kushika nyadhifa, walioleta mabadiliko, na wenye ndoto kubwa zinazoweza kupimika. 

 1. KANYASU: VIPAUMBELE VYA MADINI NA MAZINGIRA 

Mbunge anayemaliza muda wake, Mh. Constantine Kanyasu, amejijengea jina kupitia vipaumbele vyake vilivyolenga wachimbaji, sekta ya madini, mazingira na sera za kitaifa.

Vipaumbele vyake vilivyowahi kutekelezwa:

Kuanzisha maabara ya mionzi kwa ajili ya kupima madini Geita.

Kutetea fidia ya wananchi waliopata madhara ya mitetemo kutoka migodini.

Kuunga mkono kiwanda cha kusafisha dhahabu (GGR) – kilichozalisha ajira zaidi ya 100.

Kupigia debe upandaji wa miti baada ya uchimbaji – sera ya madini endelevu.

Kama ataendelea, Kanyasu anasema kipaumbele chake ni:

“Kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo, kuunganisha sekta ya madini na vijana wanaomaliza vyuo kwa mafunzo ya kiufundi.”

 

2. MANJALE MAGAMBO: VIPAUMBELE VYA VIJANA NA MAWASILIANO MAPYA

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita, Manjale Magambo, anaungwa mkono na vijana wengi kwa sababu ya historia ya kuwatetea na kuwawezesha.

 Vipaumbele vyake vinavyozungumzwa:

 Kukuza ajira za vijana kupitia miradi bunifu na ya kimkakati.

 Kuanzisha programu za mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wa mtaa hadi mtaa.

 Kufungua milango ya ushirikiano kati ya Geita na wadau wa kimataifa.

 Wafuasi wake wana mnukuu:

 “Geita mpya inahitaji sauti mpya, kasi mpya na maono mapya ya kimaendeleo.”

3. CHACHA WAMBURA: VIPAUMBELE VYA ELIMU NA UWEKEZAJI

Mmiliki wa shule za Waja na msomi mwenye mtazamo wa kitaasisi, Chacha Wambura, anaamini elimu ndio msingi wa maendeleo ya mji.

 Vipaumbele vyake vinavyopigiwa debe na wafuasi:

 Kuweka msukumo mkubwa kwenye elimu bora ya msingi hadi chuo.

 Kuanzisha mfuko wa mikopo kwa wanafunzi wanaotoka familia duni.

 Kujenga vituo vya ubunifu (innovation hubs) kwa vijana wa Geita.

 Ananukuliwa akisema: 

“Tusipojenga watu, hatuwezi kujenga mji—elimu ni dhamira yangu ya msingi.”

4. INJINIA ROBERT GABRIEL: VIPAUMBELE VYA MIUNDOMBINU NA UTENDAJI

 Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mara na Mwanza – Injinia Gabriel, anatoka kwenye rekodi ya utendaji badala ya maneno. Anaungwa mkono na wanaotaka Geita iendelee kuongozwa kwa mtindo wa ‘results-based leadership’.

 Vipaumbele vyake:

 Kuendeleza barabara, stendi na masoko ya kisasa.

 Kuimarisha huduma za afya kupitia usimamizi bora wa rasilimali.

 Kuunganisha Geita kwenye gridi kubwa ya uchumi wa kanda.

  “Wale wanaopiga kelele hawajawahi kusimamia bajeti hata ya shule ya msingi. Mimi nilisimamia bajeti ya mikoa mitatu—na nilifaulu.”

 

TATHMINI YA KITAALUMA: VITA YA VIPAUMBELE SI YA KUSUKUMWA NA HISIA

Katika uchaguzi huu, Geita inakabiliwa na uchaguzi mgumu lakini muhimu sana. Si uchaguzi wa nani ana kipaza sauti kizuri au bango la kisasa, bali nani ana dira, na nani anaweza kuitafsiri dira ya taifa kwa muktadha wa Geita.

 Maswali ya msingi kwa mpiga kura:

 Je, mgombea ana rekodi ya kufanya kazi au ni ahadi tupu?

 Je, kipaumbele chake kinagusa maisha ya wananchi wa kawaida?

 Ana uelewa gani wa Ajenda za Serikali ya Awamu ya Sita?

 HITIMISHO: SIASA NI VITA YA MAWAZO – SI KELELE ZA MITANDAONI

 Kama kweli wananchi wa Geita Mjini wanataka mabadiliko chanya, basi uchaguzi huu usiwe wa ushabiki wa WhatsApp wala kelele za wapambe. Badala yake, uwe uchaguzi wa hoja, mikakati na maono yatakayomkomboa kijana wa Geita, mama wa soko, mzee wa kijiji na mfanyabiashara wa kati.

Katika vita ya vipaumbele—tusichague jina, tushikilie dira.

Victor Bariety

Mwandishi wa Habari, Mchambuzi wa Siasa – Geita

MWISHO

 

Post a Comment

0 Comments