![]() |
| Afisa Usalama wa Chakula wa TBS Kanda ya Ziwa Bi Nuru Mwasulama. |
Na Urban Epimark, Geita.
Shirika la Viwango hapa nchini (TBS) katika kanda ya Ziwa limepanga kutoa mafunzo ya siku mbili kwa wajasiriamali wanao sindika mazao ya mpunga na mafuta ya alizeti katika mkoa wa Geita.
Hayo yameelezwa na Afisa usalama wa chakula wa TBS kanda ya Ziwa Bi Nuru Mwasulama leo kwa njia ya simu akiwa jijini Mwanza.
"TBS kanda ya Ziwa inakusudia kutoa mafunzo ya kuongeza mnyororo wa thamani kwa wazalishaji na wauzaji wa mazao ya mpunga na mafuta ya alizeti ili kutoa uelewa wa jinsi ya kuzalisha kwa ubora na pia kutumia vifungashio bora ili kutunza thamani ya bidhaa isiharibike na hivyo ziweze kushindana vyema sokoni" alisema.
Mtaalam huyo wa kudhibiti ubora wa chakula aliendelea kusema lengo haswa la mafunzo hayo kwa wasindikaji wa mpunga na mafuta ya alizeti ni kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya maboresho katika mnyororo wa ubora.
"TBS hua inafanya kaguzi wezeshi na kaguzi tambuzi ili kuwezesha mazao makuu ya kimkakati katika kanda ya ziwa yakiwemo mpunga na mafuta ya alizeti ambayo yote ni mazao ya kibiashara pia katika mkoa wa Geita" alifafanua zaidi.
Halikadhalika akaendelea kueleza kwamba, TBS inaweka msisitizo kwa wazalishaji wa mpunga na mafuta ya kupikia ya alizeti ili wajasiriamali waweze kuzalisha kwa viwango vinavyokubalika na kuweza kushindana katika soko la ndani na pia soko la nje la Afrika Mashariki kwani viwango vinavyotumika ni vya aina moja.
Nae Afisa Maendeleo ya Biashara wa SIDO mkoa wa Geita Bw Bakari Kitoboli amesema tayari walengwa wamesha andaliwa na taasisi yake tayari kwa kushiriki mafunzo hayo.
![]() |
Afisa Maendeleo ya Biashara wa SIDO mkoa wa Geita Bw Bakari Kitoboli (katikati) akiwa katika picha na watumishi wengine wa SIDO mkoa wa Geita kwenye maonesho Fahari ya Geita. |
Bw Kitoboli aliendelea kusema kwamba, mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi cha NVTC cha mjini Geita kilichopo jirani na mzunguko wa barabara (keep left) iendayo eneo la mgodi wa GGML, mafunzo yanatarajiwa kufanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa yaani Juni 2 na 3 mwaka huu 2022.
Ametoa rai kwa wajasiriamali wote walioandaliwa wafike eneo la mafunzo mapema na kushiriki vyema mafunzo hayo kwani wanao hitaji mafunzo hayo ni wengi lakini kwa safari hii fursa ilizotolewa na TBS ni washiriki 40, alisema.
![]() |
| Aina ya mchele uliosindikwa na kuwekwa kwenye kifungashio bora. |
Mwisho.




0 Comments