Na Victor Bariety;
Kuna simulizi maarufu duniani simulizi ya meli ya Titanic, iliyopewa sifa ya kuwa meli kubwa, salama na isiyoweza kuzama. Lakini ndani ya usiku mmoja wa Aprili 1912, matumaini makubwa yakageuka kilio cha kihistoria. Titanic ikazama katika bahari ya Atlantiki, ikibeba zaidi ya watu 1,500 na ndoto zao.
Safari ya Titanic ni hadithi ya kibinadamu, ya kuamini mno nguvu zako bila kujipima na hatari, ya kupuuza dalili ndogo ndogo za hatari zinazoashiria maanguko makubwa.
Na katika ulinganifu wa kisiasa, historia ya vyama vya upinzani nchini Tanzania inaweza kulinganishwa na meli hii vilianza kwa shangwe, matumaini, na nguvu kubwa, lakini viliporomoka taratibu kutokana na migogoro, tamaa, na ubinafsi wa ndani.
SEHEMU YA KWANZA: TITANIC MELI
ILIYOANZA KWA SHANGWE, IKAZAMA KWA KIBURI
Meli ya RMS Titanic ilijengwa na kampuni ya White Star Line mjini Belfast, Ireland Kaskazini, kuanzia mwaka 1909 hadi 1912.
Ilikuwa ni miongoni mwa meli kubwa zaidi duniani kwa wakati huo, ikitambulishwa kama “isiyoweza kuzama.”
Titanic ilianza safari yake ya kwanza
tarehe 10 Aprili 1912 kutoka Southampton, Uingereza, kuelekea New York,
Marekani, ikipitia Cherbourg (Ufaransa) na Queenstown (Ireland).
Ndani yake walikuwamo matajiri, viongozi, wafanyabiashara na watu wa kawaida waliokuwa na ndoto mpya za maisha.
Lakini usiku wa 14 Aprili 1912, saa 5
usiku, Titanic ikagonga barafu kubwa (iceberg) upande wa kulia.
Maji yakaanza kuingia ndani ya sehemu
tano kati ya kumi na sita zilizotengenezwa kuzuia kuzama.
Kwahiyo, meli ambayo ilihesabiwa salama zaidi ulimwenguni, ilianza kuzama taratibu.
Saa 8:20 usiku wa Aprili 15, Titanic ikazama rasmi. Watu zaidi ya 1,500 walipoteza maisha, huku wachache tu wakinusurika kwa msaada wa meli ya Carpathia iliyowasili baada ya saa kadhaa.
Baada ya maafa haya, dunia ilijifunza
umuhimu wa kujitathmini, kuchukua tahadhari, na kuepuka kiburi cha mafanikio.
SEHEMU YA PILI: VYAMA VYA UPINZANI
TANZANIA KUANZA KWA NGUVU, KUPOROMOKA KWA MIGOGORO
Tanzania iliruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya marekebisho ya Katiba. Vyama vingi vikazaliwa, na matumaini ya mageuzi ya kisiasa yakawa makubwa.
NCCR–MAGEUZI: NGUVU YA KWANZA YA MABADILIKO
Chama cha NCCR–Mageuzi kilianzishwa rasmi mwaka 1993 kikiongozwa na Augustino Mrema, aliyekuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani.
Katika uchaguzi mkuu wa 1995, Mrema
alishika nafasi ya pili kwa kupata zaidi ya 27% ya kura za urais, huku chama
chake kikijipatia viti 19 bungeni.
Huo ulikuwa wakati ambapo upepo wa upinzani ulionekana kuwa na nguvu ya kweli. Wananchi wengi waliamini mageuzi yalikuwa karibu.
Lakini muda mfupi baadaye, chama
hicho kilianza kuyumba kwa migogoro ya ndani, makundi ya uongozi, na kukosekana
kwa umoja.
Viongozi wakaanza kugombea madaraka
badala ya kushindana kwa hoja.
NCCR–Mageuzi ikazidi kupoteza mvuto
taratibu, ikibaki kivuli cha jina lake kubwa la awali.
TANZANIA LABOUR PARTY (TLP): SAUTI YA
WAFANYAKAZI ILIYOKWAMA NJIANI
TLP ilizaliwa mwaka huo huo wa 1992, ikijitangaza kama chama cha kuwatetea wafanyakazi na wanyonge.
Ilikuja kuwa maarufu zaidi baada ya
Mrema kuhamia humo mwaka 1999.
Katika uchaguzi wa 2000, TLP ilipata
viti vitatu bungeni, na mgombea wake wa urais akapata karibu asilimia 7.8 ya
kura zote.
Lakini kama ilivyokuwa kwa Titanic, matumaini hayo yalidumu kwa muda mfupi.
Migawanyiko ya ndani, kukosekana kwa
umoja, na kutojenga misingi imara ya chama kitaifa kulisababisha TLP ipoteze
umaarufu wake haraka.
Mwaka 2005, chama kilipata kiti
kimoja tu bungeni, na baada ya hapo kikawa hakisikiki tena kisiasa.
CHADEMA: MABADILIKO YENYE MVUTANO
CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) kilianzishwa mwaka 1992, lakini kilianza kung’ara zaidi miaka ya 2005 hadi 2015.
Kiliwavutia vijana, wasomi na wapenda
mabadiliko, kikijijengea sura ya chama chenye mpangilio na dira.
Katika uchaguzi wa 2010, CHADEMA kilipata viti 48 bungeni, na mwaka 2015, kiliunda muungano wa UKAWA ulioipa nguvu zaidi kisiasa.
Kwa muda, kilionekana kuwa chama
kinacholeta changamoto kwa chama tawala.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa Titanic, migogoro ya ndani, makundi, na tofauti za kiuongozi zilianza kuibuka.
Baadhi ya viongozi walihama, wengine
wakasimamishwa, na chama kikaanza kupoteza mvuto wake taratibu.
Badala ya kuunganisha nguvu za
upinzani, migogoro ilizidisha mpasuko na kuacha pengo kubwa la uaminifu kwa
wananchi.
CCM: KAMA NAHODHA ALIYEBEBA TAIFA
KWENYE MELI SALAMA
Wakati vyama vingine vikipoteza mwelekeo kutokana na migongano ya ndani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kusimama imara kwa misingi ya utekelezaji wa sera na miradi mikubwa ya maendeleo.
Kupitia serikali zake, CCM imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kama:
Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP)
Reli ya Kisasa ya SGR
Mradi wa Maji na Miundombinu Vijijini
Barabara za juu (flyovers) na miji ya kisasa, pamoja na kuboresha huduma za afya na elimu
CCM imeendelea kuthibitisha msemo wake wa “Chama kinachosema na kutenda,” jambo lililozidi kuongeza imani kwa wananchi wengi.
Kwa kila awamu ya uongozi,
kimeendeleza sera zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja, huku kikijenga
nidhamu na uthabiti wa kisiasa.
UCHAMBUZI: TITANIC NA UPINZANI SOMO KWA WATANZANIA
Titanic ilizama kwa sababu ilipuuzia tahadhari na kuamini haiwezi kuanguka.
Vyama vya upinzani Tanzania vimeporomoka
kwa sababu hiyo hiyo — si kwa sababu ya nguvu ya nje, bali kwa sababu ya
kutothamini umoja wa ndani, kutojipanga, na kushindwa kujisahihisha mapema.
Kama Titanic, vilianza kwa shangwe, lakini makosa madogo yakawa sumu ya mfumo.
Na kama CCM ilivyokuwa “meli imara”
yenye nahodha makini, imeweza kusafiri kwenye bahari ya siasa kwa utulivu,
ikitekeleza miradi, na kudumisha matumaini ya Watanzania.
HITIMISHO
Historia ya Titanic inatufundisha kwamba ukubwa haujalishi kama ndani kuna ufa.
Na historia ya vyama vya upinzani
Tanzania inatufundisha kwamba umaarufu hauwezi kudumu kama ndani hakuna umoja
na dira moja.
Leo, Watanzania wanaendelea kuwekeza imani zao kwa CCM — chama kilichoonyesha uthabiti wa kweli kupitia utendaji, uwajibikaji, na miradi mikubwa inayobadili maisha ya wananchi.
Kwa vyama vya upinzani, somo ni moja tu:
Kabla hujapambana na mawimbi ya nje,
hakikisha meli yako ya ndani haina ufa.
MWISHO
Imeandikwa na Victor Bariety
0757 856 284



0 Comments