Na Victor Bariety, Geita
Septemba 2, 2025
Picha: Mkimbiza Mwenge Kitaifa 2025 akimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Geita, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa barabara ya Kasco.
Kilio cha wananchi wa Geita kuhusu
changamoto za miundombinu kinaendelea kupata majibu ya vitendo. Leo, katika
eneo la Kasco hadi Shule ya Sekondari Nyanza, Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025
umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nyepesi yenye
urefu wa kilomita 1.32, hatua inayoongeza chachu ya maendeleo kwa wakazi wa
Manispaa ya Geita.
Picha: Mkimbiza Mwenge Kitaifa 2025 akisoma maandishi kwenye jiwe la msingi mradi wa barabara ya Kasco
Mradi huo unaotekelezwa na
Halmashauri ya Manispaa ya Geita kupitia fedha za mapato ya ndani, unasimamiwa
na TARURA Geita huku mkandarasi akiwa ni kampuni ya Evax Construction Ltd ya
Mureba. Kwa mujibu wa mkataba namba 63CC1/2924/2025/W/03, gharama ya ujenzi ni
shilingi 999,950,000.00 bila VAT.
Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Injinia Bahati Subeya, mradi huo ulianza Machi 7, 2025 na unatarajiwa kukamilika Septemba 8, 2025. Hadi sasa umefikia asilimia 95 ya utekelezaji, ambapo zaidi ya shilingi milioni 754 zimeshalipwa.
Baada ya kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndg. Ismail Ali Ussi, alisifu ubora wa utekelezaji akisema hakuna chembe ya ubabaishaji.
“Nimetembea mikoa 24, huu ni
mkoa wa 25. Sikuwahi kuona miradi ya kiwango cha juu kama hii inayotekelezwa na
TARURA. Jana nilizindua barabara ya Nzera, leo Kasco, yote kwa ubora wa hali ya
juu. Hakuna harufu ya ufisadi, hakuna ubabaishaji – kazi hii inastahili
saluti,” amesema Ussi huku akishangiliwa na wananchi.
Aliongeza kuwa miradi inayotekelezwa
chini ya usimamizi wa TARURA ni ushahidi kuwa kodi zinazotozwa kwa wananchi
zinatendewa haki. Pia aliipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya
Geita kwa kuendelea kulinda amani, jambo lililompa faraja kubwa katika ziara
hiyo ya kitaifa.
Kabla ya kuweka jiwe la msingi, Ndg. Ussi alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa miradi mikubwa inayotekelezwa kote nchini ni matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kura zetu ndizo zinazoamua
hatima ya maisha yetu. Uchaguzi ni msingi wa amani na maendeleo tunayoyaona.
Rais wetu Samia amethibitisha kwa vitendo – miradi hii ni uthibitisho. Oktoba
tumpe kura nyingi ili aendelee kutupigania,” amesisitiza kiongozi huyo wa mbio
za Mwenge.
Barabara ya Kasco ni ya pili
kutembelewa na Mwenge wa Uhuru ndani ya Manispaa ya Geita baada ya jana
kuzinduliwa barabara ya Nzera Center yenye urefu wa kilomita 1.1, ambayo pia
ilipewa sifa kwa kiwango cha juu cha ubora.
Kwa hatua hizi, Geita inaendelea
kuandika historia ya mafanikio makubwa ya miradi ya TARURA, miradi
inayobadilisha uso wa miji na vijiji, huku wananchi wakiona matunda ya kodi zao
kwa macho.
Imeandaliwa na Victor Bariety – 0757
856 284
PICHA ZAIDI



















0 Comments