Na
Victor Bariety, Geita
Katika risala ya mradi huo, iliyosomwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Injinia Bahati Subeya, ilielezwa kuwa barabara hiyo imetekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilianza tarehe 24 Julai 2023 na kukamilika tarehe 15 Oktoba 2024 kwa gharama ya shilingi 499,995,000/=. Awamu ya pili ilianza tarehe 22 Machi 2024 na kukamilika tarehe 15 Oktoba 2024 kwa gharama ya shilingi 237,499,984/=. Hivyo kufanya jumla ya mradi kufikia thamani ya shilingi 737,494,984/=.
Picha: Barabara iliyozinduliwa
Aidha, hadi sasa mkandarasi amelipwa kiasi cha shilingi 714,270,224/=, ikiwa ni malipo ya kazi zote zilizokamilika. Mradi huu umesimamiwa na TARURA Wilaya ya Geita na umefikia asilimia 100 ya utekelezaji. Faida zake zimeanza kuonekana wazi kwa wananchi, ikiwemo kurahisisha usafiri na usambazaji wa huduma za kijamii, kuchochea maendeleo ya kiuchumi, na kuboresha mandhari ya eneo husika.
Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndg. Ismail Ali Ussi, alitoa pongezi za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo. Alisema hakuamini kuona mradi wa kiwango cha juu namna hiyo ukiwa na thamani ndogo ukilinganisha na matokeo yaliyopatikana.
Aidha, kiongozi huyo wa Mwenge alisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kwa amani na utulivu katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, akieleza kuwa miradi kama hii ni matunda ya Serikali inayojali wananchi wake bila kujali itikadi za vyama. Alisisitiza kuwa barabara hii ni ya kudumu na itaendelea kuhudumia wananchi kwa miaka mingi ijayo, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuitunza.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi kwa niaba ya wananchi wake, Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini anayemaliza muda wake na ambaye amefanikiwa kutetea kiti hicho, Mhe. Joseph Kasheku Musukuma, alisema kazi zinazotekelezwa na Serikali ya CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kubwa na zimekuwa chachu ya wananchi kuendelea kuiamini serikali yao.
Wananchi wa Nzera waliokuwa wamejitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo walipokea pongezi hizo kwa makofi na vigelegele, wakionyesha furaha yao kwa namna mradi huo umebadili sura ya kata yao na kuwa chachu ya maendeleo endelevu.
PICHA ZAIDI
0 Comments