TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WANANCHI GEITA WATOA MAONI KUHUSU UMUHIMU WA KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA MPIGA KURA.

 

Samwel Masunzu , Geita

Wananchi mkoani Geita wamesema kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura kutawasaidia kuepuka changamoto mbalimbali za kukosa huduma ambazo wamekuwa wakizikosa kutokana na kukosa kitambulisho cha mpiga kura

Maoni hayo yametolewa na baadhi ya wananchi ambao ni Michael Fitina ,Elizabeth Emmanuel na Shija Kija wakiwa katika kituo cha kuandikisha wapigakura cha ofisi ya mtaa wa Mwembeni kata ya Nyankumbu halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita

Wamesema licha ya vitambulisho hivyo kuwasaidia katika zoezi la kupiga kura, lakini pia vitawasaidia katika changamoto mbalimbali ikiwemo kutafuta kazi na kutambulika wanapokwa safarini hasa maneo ya mikoa ya mipakani

Mmoja wa wananchi katika mtaa huo Sara Joseph amesema kukosa kitambulisho kulipelekea kutokuingizwa katika mfuko wa TASAF,hivyo mbali na  kwamba atapata huduma ya kupiga kura pamoja na huduma nyingine,  kwake kitambulisho hicho ni cha muhimu

“Kuna wakati lilikuja zoezi la kutafuta watu wa TASAF,na mimi nilishindwa kuingizwa kwenye TASAF licha ya kuwa nina watoto wanne na nilitekelezwa lakini ilishindikana kutokana na kukosa kitambulisho” amesema Sara.

Wawakilishi wa vyama vya siasa, Winifrida Ephraim ambaye ni katibu wa chama cha mapinduzi tawi la Mwembeni pamoja na Lusana Charles ambaye ni mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo tawi la Mwembeni wamesema hadi sasa wanaendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili wapate haki ya kushiriki zoezi la kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025

Hata hivyo mbunge wa jimbo la Geita mjini  Costantine Kanyasu amewasistiza wananchi kuendelea kuona umuhimu wa kupata vitambulisho hivyo vitakavyowasaidia kushiriki katika uchaguzi mkuu

“Viongozi bora watapatikana kupitia uchaguzi, na hakuna mtu anayeweza kupiga kura kuchagua kiongozi kama hana kitambulisho cha mpiga kura, kwahiyo niwasisitize nyote mshiriki zoezi hili la kuboresha daftari la kudumu la mpiga kura” amesema Kanyasu

Zoezi la kuandikisha na kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura kwa awamu ya pili linaendelea katika mikoa ya Geita na Kagera ambapo limeanza August 5 na linatarajia kukamilika August 11 mwaka huu 2024 na mkoa wa Geita ukitarajia kuandikisha wapigakura wapya 299,672.




 

Post a Comment

0 Comments