Na mwandishi wetu;
Picha: Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita (Geita Press Club - GPC) Renatus Masuguliko akitoa msisitizo kuhusu mwongozo kwa waandishi wa habari katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuzingatia sheria za nchi, weledi na maadili.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa
Habari Mkoa wa Geita (Geita Press Club - GPC), ametoa wito kwa waandishi wa
habari kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia maadili ya taaluma yao
pamoja na sheria za nchi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na mwandishi wetu mjini Geita, Mwenyekiti huyo amesema kuwa hadi sasa waandishi wa habari katika mkoa huo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa, kwa kufuata maadili ya taaluma bila malalamiko yoyote rasmi kupokelewa na ofisi ya GPC kutoka kwa wadau au waandishi wenyewe.
“Ndugu waandishi wa habari wenzangu, sisi ni kati ya wadau muhimu katika uchaguzi mkuu kupitia dhamana zetu. Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha kuendelea kufanya kazi zenu kwa weledi, kwa kuzingatia sheria za nchi na maadili ya taaluma yetu, hasa tunapokaribia siku ya kupiga kura,” amesema Renatus Masuguliko (Mwenyekit wa GPC).
Katika kuhakikisha wanahabari wanakuwa na miongozo sahihi ya kazi katika kipindi cha uchaguzi, ofisi ya GPC imepokea vitabu 18 kutoka Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ambavyo vinaelekeza namna ya kuripoti uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa mwaka 2025.
Aidha, amehitimisha kwa kuwakumbusha waandishi wa habari kuwa katika siku ya upigaji kura, ni muhimu kujiepusha na kuripoti matokeo kutoka vyanzo visivyo rasmi au visivyo na mamlaka kisheria.
“Matokeo halali ya uchaguzi yatatolewa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC). Tutimize wajibu wetu kwa umakini, na kwa maslahi ya Taifa letu,” amesisitiza Renatus.

0 Comments