![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Rosemary Senyamule (Aliye keti) akimpatia chanjo ya matone ya Polio mmoja wa watoto mjini Geita. |
Na.Salum Maige,Geita.
Mkoa wa Geita umevuka lengo katika kampeni ya utoaji wa chanjo ya Matone ya Polio kwa kufanikiwa kuwafikia watoto 707,733.
Awali mkoa huo ulilenga kuwafikia watoto 553,228 wenye umri chini ya miaka mitano kuwapatia chanjo hiyo ili kuwakinga na ugonjwa hatari wa polio ambao husababisha ulemavu wa kudumu.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Mratibu wa Huduma ya Chanjo mkoa wa Geita, Bi Wille Luhangija amesema watoto hao wamepatiwa chanjo hiyo kwenye kampeni iliyofanyika kuanzia Mei 18 hadi 21 mwaka huu 2022.
Bi.Luhangija amesema awali mkoa ulipanga kuwafikia watoto 553,228 lakini umevuka lengo hilo na kuwafikia watoto 707,733 sawa na asilimia 128.8.
Luhangija amesema,Halmashauri ya Geita imechanja watoto 243,201 sawa na asilimia 124.3,Bukombe watoto 89,164 (125.1%),Chato 161,193 (138.2%), Geita Mjini 77,426 (139.1%),Mbogwe 72,872 (118.4%) na Nyang'hwale 63,139 (131.1%).
Mbele ya Mwandishi wa Habari hizi,Luhangija amefafanua kuwa,Kila Halmashauri imevuka lengo ililojiwekea katika Kampeni hiyo ya Kitaifa ya Kuzuia maambukizi ya Virusi vya Polio kwa watoto kutokana na uhamasishaji wa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari.
Amesema Hatua hiyo ya serikali kuendesha zoezi la chanjo nchi nzima inatokana na kutokeo kwa mlipuko wa Ugonjwa huo katika nchi jirani ya Malawi na shirika la Afya duniani kwa kushirikiana na Shirika la Watoto Duniani UNICEF kutangaza kampeni Maalum ya kukabiliana na Ugonjwa huo.
![]() |
| Mhe Rosemary Senyamule (Mkuu wa Mkoa wa Geita) akiteta na Dkt Simeo Japheth (Mganga Mkuu Mkoa wa Geitab) wa kwanza Kushoto baada ya kumpatia mtoto chanjo ya matone ya Polio |
Hata hivyo,amesema mkoa wa Geita tangu uanzishwe mwaka 2012 haujawahi kupata mgonjwa wa polio,lakini hatua hiyo haizuii kufanya kampeni hiyo ili kuwakinga watoto na kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo.
“Kampeni hii ilifanyika kwa kupita nyumba kwa nyumba kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa,vitongoji kwa kushirikiana pia watoa huduma, tulipita pia kwenye hospitali,kwenye Vituo vya kulelea watoto,hii ni kuhakikisha tunamfikia kila mtoto kumpatia chanjo ya Polio”
“Lengo la Serikali kupitia wizara ya Afya ni kuhakikisha inajilinda na mlipuko wa ugonjwa huo ambao umeathiri watoto kwenye nchi jirani ya Malawi Kwani sisi kama jirani kumbuka watu wengi wanasafiri kutoka huko na kuja nchini kwetu ,hivyo ili kujihami na ugonjwa huo ni lazima kuchukua tahathari ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo kwa watoto wetu”alisema Luhangija.
Amesema ugonjwa huo huenea kwa mtu kula chakula na maji machafu na kwamba dalili zake ni pamoja na misuri ya mtoto kushindwa kutembea,miguu na mikono kuwa na ulemavu tepetepe na ugonjwa huo unaweza kusababisha ulemavu na kwamba ulemavu huo hauna tiba.
“Kila mzazi na mlezi anatakiwa kufuatilia makuzi na maendeleo ya Afya ya mtoto, inapotokea mtoto anaonekana na dalili nilizozitaja anatakiwa kuwahi hospitali ili kufanyiwa uchunguzi. Na kwamba katika utoaji wa huduma hii ya chanjo ya matone ya polio wananchi wajitokeze kwani chanjo hiyo ni salama na haina madhara kwa Afya ya mtoto.”alisema Luhangija.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Geita wamesema kampeni hiyo imefanikiwa kutokana na wao kutambua umhimu wake, kwani ugonjwa huo ni hatari kwa makuzi na maendeleo ya Afya ya mtoto.
Juma Athumani mkazi wa mji wa Katoro Halmashauri ya wilaya ya Geita amesema huduma hiyo ya chanjo ya matone ya Polio itasaidia sana katika kukabiliana na ugonjwa huo kwani ikitokea mlipuko wa polio unaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii na Taifa kwa Ujumla.
“Kwa sababu ni kampeni na tunaona watoto wa nchi jirani wanavyoathirika na ugonjwa huo ndio maana tulijitokeza’’anasema Sofia Juma.
Kwa Upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dk Japheth Simeo amewataka wanachi kuhakikisha wanakuwa walinzi wa Afya za watoto wao mara baada ya kuzaliwa ili kuwakinga na maradhi mbalimbali kwa kuhakikisha wanahudhuria kliniki na kuwapatia chanjo zote.
Aidha,amewashukuru wananchi kwa kujitokeza na kutoa ushirikiano kwenye zoezi hilo la kitaifa ambalo linalenga kudhibiti maambukizi ya Ugongwa wa Polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
![]() |
| Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu akitoa chanjo ya polio. |
Kwa Mujibu wa Utekelezaji wa Program Jumuishi ya Taifa ya Mendeleo na Makuzi ya Awali ya Mtoto(PJT –MMMAM) ni kwamba kundi la watoto wadogo linahitaji kuangaliwa kwa karibu na kufanyiwa uwekezaji mkubwa ili waweze kuwa rasilimali bora yenye tija kwa familia na Taifa kwa ujumla.
Uwekezaji huo ni pamoja na kuwakinga na magonjwa kama vile kuwazuia na maambukizi ya Ugonjwa wa Polio unaoenda kutekelezwa na serikali kupitia wizara ya Afya.
| picha ni Wazazi wakiwa katika Kituo cha Afya. |
MWISHO.



0 Comments