 |
| Jiandae kuhesabiwa |
Na Renatus Masuguliko; Mwandishi wa Habari na Mjumbe wa Kamati ya Sensa ya Mkoa wa Geita
Sensa ya Watu na Makazi ni nini?
Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchakata, kuchambua na kusambaza taarifa za kidemografia, kiuchumi, Mazingira na kijamii za watu wote na Makazi yao katika nchi kwa kipindi Maalum.
Kwa maana nyingine,Sensa ni zoezi lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi kwa umri na jinsi, mahali wanapoishi, viwango vyao vya Elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo, hali ya makazi na taarifa nyingine nyingi.
Nini Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi?
Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu sana kwani inasaidia kupata takwimu za msingi za watu na hali ya makazi ambazo zitasaidia kutunga sera, kupanga na kufuatilia mipango ya Maendeleo ya kimkakati inayolenga kukuza ustawi wa nchi na watu wake.
Aidha, matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 yatasaidia Serikali na wadau wengine kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika kutekeleza mipango ya Maendeleo iliyokusudiwa kwa lengo la kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Umuhimu wa sensa ni kuwezesha kupatikana kwa takwimu sahihi zitakazo iwezesha Serikali na wadau wengine kupanga mipango ya Maendeleo ya watu wake katika sekta mbali mbali za Afya, Elimu, hali ya ajira, miundo mbinu kama bara bara, nishati na maji safi.
Kwa msingi huo,Sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa nafasi yake analazimika kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha inakuwa ya mafanikio makubwa.
Je, ninani anapaswa kuhesabiwa?
Wanaopaswa kuhesabiwa ni watu wote watakao lala ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania usiku wa kuamkia siku ya Sensa 23 Agosti, 2022 pamoja na watu wote watakao kuwa katika kaya za jumuiya kama vile hotelini, nyumba za kulala wageni, hospitalini, magereza, mabweni ya Wanafunzi, kambi za Jeshi, vituo vya kulelea watu wenye mahitaji Maalum kama yatima na wazee, kambi za wavuvi, watu wasio na Makazi Maalum na vituo vya usafiri wa umma ( kama vituo vya mabasi, garimoshi, viwanja vya ndege, na bandari) watahesabiwa kwa kutumia utaratibu Maalum utakaoandaliwa na Kamati za Sensa katika ngazi ya mtaa, kitongoji na shehia.
Je, upi ni wajibu wa viongozi katika kufanikisha zoezi la Sensa?
Viongozi wote kuanzia Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji au Shehia jukumu lao kubwa ni kuhakikisha Sensa inafanyika kwa mafanikio makubwa.Hili litafanikiwa endapo viongozi katika ngazi zote watakuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha, kuelimisha wananchi wajibu wao na nini cha kufanya wakati wa Sensa.
Viongozi wanapaswa kuuandaa umma kwa kuuelimisha, kuuhamasisha umuhimu wa Sensa ili waweze kushiriki pamoja na kutoa ushirikiano na msaada unapohitajika wakati wote wa Sensa.
 |
| Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Mhe Alhaj Said Kalidushi |
Pamoja na kuwatumia viongozi hao, uhamasishaji utafanyika kwa kuwashirikisha Wanafunzi mashuleni, vyuoni, vikundi vya Sanaa na burudani ili viweze kutumia fani za sanaa kama nyimbo, maigizo , ngonjera na ngoma za utamaduni katika kutoa Elimu ya Sensa.
Je, Mwananchi unatakiwa kufanya nini wakati wa Sensa 2022?
Mwananchi ndiye mlengwa mkuu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 hivyo wajibu mkubwa wa mwananchi ni kuhakikisha kuwa anajiandaa kuhesabiwa kwa kuelewa siku ya Sensa yenyewe na kujibu kwa usahihi maswali utakayo ulizwa na karani wa Sensa.
Mwananchi unatakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Karani wa Sensa atakapo kutembelea katika kaya kwa kujibu maswali yote utakayoulizwa kwa usahihi.
Nimuhimu kwa Mkuu wa kaya kuhakikisha anachukua taarifa zote muhimu kama umri, Elimu, jinsi, hali ya ndoa, umiliki wa vitambulisho vya Taifa na shughuli za kiuchumi za watu wote waliolala katika kaya yake usiku wa kuamkia siku ya Sensa ili aweze kukumbuka wakati Karani atakapo kutembelea katika kaya.
 |
| Mch. Leonard Thomas ( Askofu Mkuu wa Makanisa ya Emmanuel of Africa) Tanzania. |
Wakizungumzia wajibu wa kuhesabiwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini wanasema inatajwa hata katika maandiko matakatifu katika Biblia na Kuruani tukufu kuwa na manufaa.
Je, ni maeneo gani Maalum ya kuhesabia Watu?
Maeneo Maalum ya kuhesabia Watu ni pamoja na hospitali, vyuo, Shule, kambi za Jeshi, kambi za wakimbizi, nyumba za kulala wageni, magereza na mengine kama hayo.
Wote watakao kuwa katika maeneo hayo katika usiku wa kuamkia siku ya Sensa watapitiwa na Karani wa Sensa na kuhesabiwa.
 |
| Tuwa Mohamed Tuwa ( Mjumbe wa Baraza la Masheikhe Mkoa wa Geita) akitoa wito kwa wananchi kushiriki zoezi la Sensa Agosti 23, 2022. |
Aidha viongozi wa dini wanataja athari zinazoweza kupatikana kutokana na kutohesabiwa kwa Sensa kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.
Naobaadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa bila kujali tofauti zao za itikadi wamejitokeza na kusisitiza kuwa wananchi hawana budi kujitokeza kuhesabiwa bila hofu.
 |
| Rasta Ikolongo Emmanuel Otto (Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Geita) akihamasisha zoezi la Kitaifa la Sensa Agosti 23, 2022 |
"Watu washiriki Sensa ni kuisaidia Serikali kujua idadi ya wananchi wake ili itakapokuwa inakwenda kugawa bajeti ikiwa inajua inawatu wangapi, kila mwananchi aone jambo la kuhesabiwa ni jambo la msingi na linamhusu yeye moja kwa moja" alisema Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Geita Rasta Ikolongo Emmanuel Otto.
Je,Wawindaji, Wavuvi, Warina Asali, Wapasua Mbao, Wachungaji au Wafugaji watahesabiwa?
Katika jitihada za kuhakikisha kila mtu anahesabiwa na anahesabiwa mara moja tu, kuna Makundi mbali mbali ya watu ambayo yatatakiwa kuhamasishwa ili yatoe ushirikiano mzuri katika kufanikisha kazi ya kuhesabu Makundi hayo.
Makundi hayo ni yale ya Wawindaji, Wavuvi, Wachungaji wanao hama hama, watafutaji madini, Warina asali, wavuna karafuu, na baadhi ya wakulima ambao wana mashamba yaliyo mbali na Makazi yao ya kawaida.
Utakuwa sio rahisi kwa Karani wa Sensa kuelewa ni wapi walipo ili kuweza kufuatwa huko na kuhesabiwa.
Kwa msingi huo, viongozi wa maeneo husika wanapaswa kuyatambua hayo maeneo mapema kabla ya zoezi la kuhesabu Watu kwani Karani wa Sensa atatakiwa kuongozana na viongozi hao kwenda kuwahesabu watu hao huko huko waliko.
 |
| Tryphone Robert Kambona (Mjumbe wa Kamati Kuu ya Siasa kata ya Buhalahala Geita) akihamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa kwenye zoezi la Sensa Agosti 23. |
Bw Kambona amewaomba wananchi mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla kuheshimu siku ya kuhesabiwa, asipuuze. " Jitahidi kama Mtanzania kuhesabiwa kwenye Sensa ili upate haki zako za msingi " alisema Bw Kambona.
Je, wasafiri na Watu wasiokuwa na Makazi Maalum watahesabiwa?
Watu watakao kuwa safarini usiku wa kuamkia siku ya Sensa, yaani watakaokuwa katika Vyombo vya usafiri kama gari moshi, mabasi, ndege, meli na Vyombo vingine vya usafiri.
Watu hawa watahesabiwa pale watakapoanza safari au watakapomalizia safari zao baada ya kufika saa 6 na dakika 1 usiku na nikabla ya asubuhi.
Kwamsingi huo, watu hawa (Wasafiri) watahojiwa usiku wa manane kwa utaratibu utakao pangwa na viongozi.
Kwaupande wa Watu wasiokuwa na Makazi Maalum ambao ni Watu hulala sehemu mbali mbali kamavile maeneo ya wazi, sokoni, chini ya madaraja,barazani, kwenye vituo vya garimoshi na vya mabasi, bandarini na sehemu nyingine.
Watu hawa wanapaswa kuhesabiwa, hivyo utaratibu Maalum umewekwa kuhakikisha kuwa watu hao wanahesabiwa na Karani wa Sensa atakapo wakuta wamelala usiku wa kuamkia siku ya Sensa Agosti 23,2022.
 |
| Justine Simbila (Mwandishi nguli wa Habari za Uchunguzi na Mwanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita) |
" Faida ya Sensa ni kujua idadi ya watu kusaidia kupanga Bajeti kwamba kuna watoto wangapi, watu wazima wangapi, walemavu wangapi, hivyo hakuna sababu ya kujificha halafu unarudi kutumia bajeti ya wengine" alieleza Bw Justine Simbila, Mwandishi nguli wa Habari za Uchunguzi.
Mwisho.
0 Comments