![]() |
UGONJWA wa ukimwi bado ni tishio kubwa kwa jamii na kwamba jitihada mbalimbali zinahitajika ili kuepukana na maambukizi mapya ya virus vya ugonjwa huo.
Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya dawa ya PrEP (pre-exposure prophylaxis) ambayo inatajwa kuwa bora zaidi katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU.
Licha ya dawa hiyo kuruhusiwa kutumika hapa nchini, jamii bado haijatambua uwepo wake kutokana na baadhi ya watoa huduma kutoa kwa usiri mkubwa, uchunguzi wetu umebaini.
Mwandishi wetu amefanikiwa kuzungumza na baadhi watumiaji wa dawa hiyo(majina tunayahifadhi) ambao wamedai kuwa waliitambua PrEP baada ya kupewa na mtoa huduma za afya wakiwa kwenye kilabu ya kuuza pombe nyakati za usiku.
Ni baada ya kunywa pombe na kutamani kujamiana na mhudumu wa kilabu hiyo(Barmed) pasipo kuwa na tahadhali ya kufanya ngono kwa kutumia njia za kujikinga na maambukizi ya mapya ya VVU ikiwemo magonjwa ya zinaa.
Hata hivyo uchunguzi huo umebaini kuwa baadhi ya vijana hutamani kutumia njia za kujikinga na maambuki mapya ya VVU lakini wanapotumia mipira ya kiume(Condoms) huwapungizia radha ya tendo la ndoa, kuwachelewesha kumaliza tendo na wengine kukerwa na harufu itakanayo na mafuta ya mipira hiyo.
MRATIBU WA UKIMWI
Kwa mujibu wa mratibu wa Ukimwi wilaya ya Chato mkoani Geita, Dk. Lilian Kagaruki, dawa ya PrEP, ni kinga tiba muhimu sana kutumiwa na watu walio katika hatari ya kuambukizwa, wanandoa ambao mwenzi mmoja ana VVU na mwingine hana.
Wengine ni wale wasichana wanaouza miili yao (madada poa), wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na wale waraibu wa madawa ya kulevya.
"PrEP inaswa kuanza kutumiwa na mtu kabla ya kuambukizwa VVU na kwamba iwapo atathibitika kuwa na maambukizi mapya ya Ukimwi tunamshauri kuanza kutumia ARV"amesema.
Dk. Kagaruki anasema wilaya ya Chato ni miongoni mwa wilaya ambazo bado jitihada kubwa za mapambano dhidi ya ukimwi zinapaswa kupewa kipaumbele kutokana eneo kubwa kuzungukwa na shughuli za uvuvi wa samaki na uchimbaji madini.
![]() |
Hata hivyo amesema PrEP inapaswa kutolewa kwa mtu ambaye amepatiwa elimu sahihi ya matumizi na kwamba haitolewi kama njugu kwa kuwa inaweza kusababisha madhara mengine kiafya iwapo mtumiaji hatozingatia masharti anayopewa.
Sambamba na hilo, Dk. Kagaruki anakiri kuwa dawa hiyo imeonyesha matokeo makubwa kwa aslimia 99 ya watu wanaoitumia huku akiitaka jamii kutoona aibu kujitokeza kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kuanza matumizi yake.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la afya duniani (WHO)iliyotolewa Septemba 2015, ilipendekeza watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU, wanaojulikana kama watu walio katika hatari, wapewe PrEP kama chaguo la ziada la kuzuia, kama sehemu ya kuzuia kwa ujumla.
Mwisho.
Picha zote kwa hisani ya mtandao.



0 Comments