![]() |
| Mkuu wa Wilaya ya Chaton Mhe Martha Mkupasi akikabidhi nyumba mpya za watumishi wa hospita ya rufaa ya kanda ya Chato leo Juni 30,2022. |
Na Daniel Limbe, Chato.
SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imewaonya wananchi wanaojihusisha na vitendo vya kishirikina kwa watumishi wa Umma, na kwamba hatua hiyo inaweza kudhorotesha upatikanaji huduma kwa jamii.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Chato, Martha Mkupasi, amemuagiza Mwenyekiti wa kijiji cha Kitela kata ya Chato, Makoye Majani, kuitisha mikutano ya hadhara kwa lengo la kuzungumza na wananchi wanaozunguka makazi ya nyumba mpya za watumishi wa hospita ya rufaa ya kanda ya Chato.
![]() |
| Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe Martha Mkupasi akiwa ameambatana na Maofisa wengine katika Wilaya yake, wakati wa kukabidhi Makazi mapya ya Watumishi wa Hospitali ya Kanda Chato. |
Mkupasi ametoa maagizo hayo leo wakati akikabidhi nyumba 20 zilizojengwa na serikali kupitia shirika la nyumba nchini (NHC) Kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1
"Mwenyekiti wa kijiji hiki umefanikiwa kuongeza wananzengo (wakazi) wapya kwenye eneo lako...sasa nakuagiza uitishe mikutano ya hadhara uzungumze na wananchi ili wawape ushirikiano mzuri watumishi hawa...sitaki kusikia wanalalamika kuwa nililala jana nikasikia nimekabwa shingoni, mara nilizima laptop(kompyuta mpakato) asubuhi nikakuta imewaka, mara frashi yangu niliweka hapa nimeikuta kule"amesema Mkupasi.
![]() |
| Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe Martha Mkupasi akikagua nyumba mpya za watumishi wa Hospitali ya Kanda ya Chato wakati wa kukabidhi nyumba 20 kwa watumishi wa kada ya Afya. |
Awali akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa nyumba hizo, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk.Brayan Mawala, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha makazi ya watumishi hao pamoja na kuendeleza miundo mbinu mingine ya hospitali hiyo kwa kuipatia fedha mara kwa mara.
Sambamba na hilo, amedai kiasi cha zaidi ya 1.7 bilioni kinahitajika ili kuboresha madirisha ya nyumba hizo, kusawazisha uwanja, kuweka uzio pamoja na matenki ya maji safi ili kuwapunguzia adha watumishi hao.
Pamoja na mambo mengine amedai mgao wa nyumba hizo kwa watumishi 27 kati ya wafanyakazi 114 umezingatia mahitaji muhimu kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa pindi panapojitokeza huduma za dharula.
Akizungumza na mwandishi wetu Dk. Matoke Muyenjwa(mnufaika wa nyumba hizo) mbali na kuishukuru serikali amedai motisha ya nyumba hizo itasaidia kuinua ari ya utendaji kazi kwa watumishi hao ambao sasa wataishi jirani kabisa na hospitali hiyo ya rufaa ya kanda ya Chato.
![]() |
| Mwonekano wa nyumba mpya 20 zilizo kabidhiwa kwa watumishi wa Hospitali ya Kanda ya Chato leo Juni 30,2022. |
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kuendelea kuboresha miundo mbinu ya makazi kwa watumishi wengine ili kuwapunguzia umbali wa kufika kazini.
Kwa upande wake, Rose Masatu (mfamasia) anasema uwepo wa makazi hayo umewasaidia kupunguza gharama za maisha ukilinganisha na awali ambapo walikuwa wakilazimika kulipa kodi za nyumba huko mitaani.

Mwonekano wa mandhari ya nyumba mpya 20 zilizo kabidhiwa kwa watumishi wa Hospitali ya Kanda ya Chato leo Juni 30,2022.
Mwisho.




0 Comments