TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WAKURUGENZI WAMETAKIWA KUTENGA BAJETI KWA AJILI YA MADAMPO YA KISASA.

Kaimu katibu tawala mkoa wa Geita Bw Herman Matemu akipanda mti  wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yaliyofanyika  kimkoa katika viunga vya shule ya sekondari ya Waschana Nyankumbu leo Juni 5, 2022

Na Gharos Riwa, Geita

Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Geita wameagizwa kuanza michakato ya upatikanaji wa madampo ya kisasa ili usafi unapofanyika taka ziweze kuhifadhiwa na kuchakatwa bila kuchafua mazingira.

Agizo hilo limetolewa na Kaimu katibu tawala mkoa Herman Matemu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa  Geita  Bi Rosemary Senyamule kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani yaliyofanyika  kimkoa katika viunga vya shule ya sekondari ya Waschana Nyankumbu leo juni 5, 2022

Mipango kama hiyo amesema inabidi tangu Halmashauri zinapoandaa bajeti zao wahakikishe kwamba zinakuwepo ili hayo madampo ya kisasa yaweze kujengwa katika kila Halmashauri. Pia amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuanzia ngazi ya familia kujitafakari ni kwa kiasi  gani maamuzi anayoyafanya yanaweza kutunza mazingira na kwa ngazi ya taasisi ni kwa kiasi gani waajiri na wenye mamlaka wanatambua umuhimu wa mazingira na kuhamasisha upandaji miti.

Katika taarifa ya utekelezaji wa uhifadhi wa mazingira iliyoseomwa na kaimu katibu tawala mkoa Geita Charles Chacha,  imebainika kwamba hali ya mazingira katika machimbo hutofautiana ambapo wachimbaji wakubwa na wakati ni salama kwa shughuli za hifadhi za mazingira huku  wachimbaji wadogo ndiyo wenye changamoto katika uhifadhi wa mazingira.

Taarifa hiyo imebainisha kwamba mkoa wa Geita ina misitu hekta laki mbili mia tano hamsini na nane nukta tatu (200,558.3) kati ya maeneo hayo sita yanamilikiwa na wakala wa misitu Tanzania- TFS, maeneo mengine sita yanamilikiwa na mamlaka za Serikali za mitaa.

“Pamoja na kuwa na misitu ya asili mkoa wa Geita umepanda miti milioni tatu, mia nane ishirini na tano ,mia tatu kumi na tatu kwa mwaka wa  2021/2022” alisoma Charles chacha.

Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kwamba Malengo ya upandaji miti ilikuwa ni kufikia milioni tisa lakini, miti iliyopandwa ni milioni tatu, mia nane ishirini na tano ,mia tatu kumi na tatu na miti iliyopona ni milioni tatu themanini elfu  mia saba hamsini na tatu huku miti hiyo iliyopandwa ni  sawa na asilimia 42.5% .

Charles Chacha amesema changamoto kubwa iliyokwamisha kufikia malengo ni upungufu wa miche ya miti, hivyo serikali imeweka mikakati ya kuyafikia malengo hayo kwa kutumia taasisi zake 66 za elimu na mpaka sasa miche  milioni mbili imeshapatikana.

Wanafunzi na wananchi walioshiriki kwenye maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani Mkoani Geita Juni 6,2022

 Vile vile amesema  Pamoja na faida kubwa inayopatikana kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini katika mkoa wa Geita zipo changamoto za kimazingira zinazo sababishwa na wachimbaji wadogo kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za misiti akitolea mfano katika maeneo ya  Mgusu mjini Geita, Nyarugusu na Rwamgasa katika Halmashauri ya wilaya ya Geita.

Hata hivyo amesema mkoa umeshatoa maelekezo kwa wachimbaji wadogo wote wanaofanya shughuli za madini kuwa na mpango wa matumizi bora ya mazingira pamoja na mpango wa hifadhi za mazingira katika sehemu zao za kazi ili kuhifadhi mazingira na kutofanya shughuli za uchimbaji maeneo ya vyanzo vya maji kwa umbali wa mita 60.

Moja ya chanzo cha maji  kilichoathiriwa na shughuli za uchimbaji wa madini ni pamoja na mabubi liliko Mgusu na machinjioni Wilaya ya Geita.

Katika kuzuia madhara yasiendelee kutokea mkoa kwa kushirikiana na ofisi ya mazingira pamoja na wakala wa misitu kanda, wanafanya juhudi katika kutoa elimu,ushauri na kusimamia sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004, na ile namba 14 ya misitu ya mwaka 2002 pamoja na sheria ndogo zote za Halmashauri.

Maadhimisho hayo yamefanyika kitaifa mkoani Dodoma na Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Kasim Majaliwa na yameongozwa na kaulimbiu “Tanzania ni moja tu, Tunza Mazingira” .

mwisho.

Post a Comment

0 Comments