TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MBUNGE BUSANDA AOMBA ZAHANATI KWA MHE RAIS SAMIA KUPITIA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE.

Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Busanda (CCM) Mhe Tumaini Magesa akiongea katika moja ya vituo vya mbio za mwenge ulio kimbizwa katika Halmashauri ya wilaya ya Geita July 21, 2022 

Na Urban Epimark,  Geita.


Mbunge wa Jimbo la uchaguzi la Busanda katika Halmashauri ya wilaya ya Geita Mhe Tumaini Magesa amemwomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan msaada wa kujengewa Zahanati kwa wananchi wa kata ya Lyamgasa kupitia kiongozi wa mbio za mwenge kwa vile idadi ya wananchi ni kubwa na hawana huduma hiyo kwa sasa.


Mbunge huyo alitoa ombi hilo kata ya Lyamgasa leo July 21, 2022 kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Bw Sahili Gerarume mbele ya umati mkubwa wa wananchi wa kata ya Lyamgasa, wilaya ya Geita wakati wa kuhitimisha mbio hizo katika Halmashauri ya wilaya ya Geita.


"Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la uchaguzi la Busanda, nakuomba wewe kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa utufikishie ombi letu kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutusaidia kupata Zahanati kwa wananchi wangu wa Kata ya Lyamgasa kwani idadi ya watu imeongezeka na kuwa wengi na huduma hiyo hapo Lyamgasa haipo" alieleza Mbunge huyo.


Mbunge huyo aliendelea kuongea na kutaja takwinu ya idadi ya watu katika Kata hiyo ya Lyamgasa kuwa ni watu elfu 49 kulingana na sensa ya watu ya mwaka 2012 lakini akasema kwa sasa wameongeza mno na huenda wakafikia watu elfu 70.

 


Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Bw John Waja (kulia) akiongozana na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Bw Sahili Gerarume (katikati) pamoja na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhe Jamhuri Wiliam (kushoto) katika kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Geita wakati wa mbio za mwenge July 21, 2022


"Tuliahidiwa mwanzoni kupatiwa msaada huo wa zahanati muda mrefu wakati watu wakiwa bado sio wengi, lakini sasa nakuomba  kiongozi wa mwenge uangalie idadi ya watu walivyo wengi lakini hawana zahanati, tuliahidiwa lakini hadi sasa inachelewa kuja na huduma hiyo  inahitajika" aliongeza Mhe Magesa.


Pia alielezea changamoto nyingine katika eneo hilo kuwa ni upungufu wa huduma ya umeme kwani eneo limepanuka lakini akasema, tayari serikali ya Rais Sania Suluhu Hassan imeidhinisha katika bajeti mkoa wa Geita kupatiwa kiasi cha pesa bilioni 2.5 zitazo tumika kuunganisha umeme katika vijiji vyote vya mkoa wa Geita, hivyo hata kata ya Lyamgasa itapatiwa huduma hiyo.


Mbunge Magesa amewapongeza madiwani wenzake wa Jimbo la Busanda kwa ushirikiano mkubwa wanao toa kwa wananchi wakati yeye yupo bungeni na pia katika kusimamia maendeleo na miradi inayoletwa jimboni humo na kutoa wito kwao kuendelea kuhimiza wananchi kujiandaa kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi August 23, ili serikali ipate kujua idadi halisi ya watu na kuwa hudumia vizuri.

 


Kiongozi wa mbio za mwenge Bw Sahili Gerarume akisaini vyeti vya pongezi vya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyalwanzaja ambao wapo katika klabu la kupinga rushwa baada ya kuizindua wakati wa mbio za mwenge katika Jimbo la Busana, Halmashauri ya wilaya ya Geita July 21, 2022. Anae mwongoza mwenye nguo nyekundu na Afisa wa PCCB mkoa wa Geita Heriet Nkya. 


Kiongozi wa mbio hizo za mwenge kitaifa Bw Sahili Gerarume katika salamu zake za ujumbe wa mwenge kwa wananchi wa Lyamgasa aliwakumbusha umuhimu wa wananchi kushiriki katika sensa ya watu na makazi  mnamo August 23 ili serikali iweze kupanga Maendeleo na kuwa na majibu ya maombi yao.


Pia alielezea madhara ya wananchi kujihusisha katika matumizi ya madawa ya kulevya kwani yanauwa nguvu kazi ya Taifa na akataadharisha jamii kuachana na mila potofu kwamba, madawa ya kulevya mfano bangi na mirungi yanaongeza nguvu ya kufanya kazi.


"Ndugu zangu wananchi wa kata hii ya Lyamgasa ninyi ni jamii ya wachimbaji wa madini, lakini wapo baadhi yenu wanazo imani potofu za matumizi ya madawa ya kulevya yakiwemo bangi, mirungi na mengineyo eti kwa imani kwamba yanaongeza nguvu mwili, hapana" alisema kiongozi huyo wa mwenge.



Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita (DMO GEITA) Dkt Modest Buchard (kulia) akijadili jambo na mmoja wa wakimbiza mwenge kitaifa Bw Emmanuel Chacha anae tokea mkoani Kagera (kushoto) wakati wa mbio za mwenge katika Jimbo la Busanda katika Halmashauri ya wilaya ya Geita July 21, 2022


Amewataka wananchi kutumia lishe bora ya vyakula mbalimbali ili kupata afya nzuri na nguvu za kufanya kazi.

Halikadhalika alikemea rushwa ya aina yeyote katika utoaji huduma za maendeleo ya jamii hususani kwa viongozi katika kutekeleza miradi ya wanachi na kupongeza klabu zote za wanafunzi alizo zindua katika mbio hizo za kupinga tabia na vitendo vya rushwa kwa jamii na pia kupinga matumizi ya madawa ya kulevya.


Mbio hizo za mwenge zilikimbizwa siku nzima eneo la Halmashauri ya wilaya ya Geita hususani Jimbo la Busanda na kuzindua miradi ya shule kwa maana ya madarasa yaliyo jengwa kwa pesa za UVIKO-19, klabu za wanafunzi za kupinga rushwa, bustani ya miti, zahanati, barabara, mradi wa kisima cha maji na ugawaji wa vyandarua kwa akina mama walio jifungua ili kuzuia ugonjwa wa maleria.

 


Wanafunzi na watu mbalimbali wakishiriki uzinduzi wa mradi wa madarasa ya shule yaliyojengwa kwa fedha za UVIKO-19 katika shule ya sekondari Nyalwanzaja katika Jimbo la Busanda, Halmashauri ya wilaya ya Geita July 21, 2022.


Mwenge huo utalala na kukesha na wananchi katika kata hiyo ya Lyamgasa na kesho July 22 utakabidhiwa wilayani Chato kuendelea na mbio zake.

 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments