![]() |
| Waziri wa Madini Mhe Dkt Doto Biteko akiongea na uongozi na watumishi wa mgodi wa BUCKREEF mkoani Geita. |
Na Urban Epimark, Geita.
Serikali imelimwagia sifa shirika tanzu la madini nchini (STAMICO) pamoja na mwekezaji mpya katika sekta ya madini BUCKREEF kwa mafanikio makubwa yaliyo fikiwa kwa kufufua shughuli za uchimbaji madini na kuiingizia serikali pato kubwa na kutoa ajira kwa wazawa kwa kipindi cha muda mfupi.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Madini Mhe Dkt Doto Biteko mkoani Geita mwishoni mwa juma wakati alipofanya ziara ya kutembelea mgodi wa BUCKREEF uliopo mkoani humo.
"Nalipongeza sana shirika letu la madini nchini STAMICO kwa ushirikiano mkubwa mnao uonesha kwa mwekezaji mpya wa mgodi huu wa BUCKREEF kwani mafanikio yameanza kuonekana kwa muda mfupi sana, hongereni sana STAMICO na BUCKREEF" alisema Waziri.
Waziri Dkt Biteko alitaja maeneo matatu makubwa ambayo serikali inajivunia kupitia uwekezaji wa kampuni hii ya BUCKREEF ikiwemo kuzalisha pato la shilingi bilioni 30 kwa muda mfupi na kutoa mrahaba serikalini wenye thamani ya shilingi bilioni 2.5.
Mafanikio mengine aliyoeleza Waziri ni kampuni hiyo ya BUCKREEF kutoa ajira nyingi kwa wazawa ambapo hadi sasa BUCKREEF imetoa ajira za moja kwa moja kwa watanzania 354.
"Haya ni mafanikio makubwa sana kwani mgodi huu ulikuwa ukimilikiwa na serikali kwa asilimia 100, lakini ulisimama kwa muda mrefu bila mafanikio lakini sasa matunda yanaonekana" aliongeza Waziri Dkt Biteko.
Fanikio la tatu ambalo serikali imetoa pongezi kwa BUCKREEF ni kukubalika kwa uongozi na shughuli za mgodi huu mpya kwa jamii inayoizunguka na hivyo kuungwa mkono na watu wa mkoa wa Geita.
Mhe Biteko alifafanua kwamba, kukubalika kwa mwekezaji BUCKREEF kwa jamii kwa muda mfupi bila kipingamizi kitaalum kunaitwa "Social License Operation kwa kifupi SLO" hivyo amewataka BUCKREEF kwa kushirikiana na STAMICO waendelee kusonga mbele bila kuchoka.
Alimalizia Waziri Dkt Doto Biteko kwa kueleza kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amedhamiria kufufua miradi yote kwenye sekta ya madini ile iliyosimama ili iweze kuchangia pato kwa uchumi wa Taifa na kutoa ajira nyingi kwa wazawa, hivyo endeleeni na jitihada hizi, aliongeza hivyo.

Waziri wa Madini Mhe Dkt Doto Biteko akipatiwa maelezo ya jinsi kazi zinavyo endeshwa katika mgodi wa BUCKREEF na moja ya wasimamizi wa mgodi huo wakati wa ziara yake mgodini hapo July 16, 2022
Nae Mbunge wa Jimbo la Busanda (CCM) katika mkoa wa Geita Mhe Tumaini Magesa ambapo mgodi huo wa BUCKREEF ulipo ameishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa inao uonesha kwa wawekezaji wanaokuja nchini ikiwemo BUCKREEF.
Mhe Magesa alibainisha mbele ya Waziri wa madini jinsi serikali ilivyosaidia upatikanaji wa fedha za kuwalipa wananchi fidia ili kupisha mwekezaji huyu ambapo hadi sasa asilimia 98% ya fidia zote imeshalipwa.
![]() |
Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhe Tumaini Magesa akiishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa kwani walio takiwa kulipwa fidia kupisha shughuli za mradi ni asilimia 98% tayari wameshalipwa. |
Pia Mhe Magesa ameipongeza BUCKREEF kwa kujali sheria ya Local Content kwani asilimia kubwa ya watumishi wa BUCKREEF wengi ni watanzania na wengi wao ni wenyeji wa kutoka mkoani wa Geita.
BUCKREEF ni mwekezaji mpya aliyeingia nchini miaka ya hivi karibuni baada ya kuvutiwa na sera nzuri za uwekezaji katika sekta ya madini ambapo waliingia mkataba na shirika la madini STAMICO kwa kugawana hisa za shirika hilo ambapo asilimia 55 za STAMICO zinamilikiwa na BUCKREEF na STAMICO kubakiwa na asilimia 45.
Mwisho.






0 Comments