Na Urban Epimark, Geita.
Serikali imesema TANESCO imeandaa mradi mahususi wa kuondoa tatizo la upatikanaji huduma za umeme kwenye maeneo ya migodini kote nchini uitwao "Grid Mapato" ambao utaongeza ufanisi na mapato kwa shirika hilo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati Mhe January Makamba katika ziara yake mkoani Geita aliyoianza tangu July 14, na July 15 kutembelea mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) ambao kwa muda mrefu umekuwa ukitumia jenerata kubwa ya kuzalisha umeme kwa matumizi ya mgodini GGML.
"Mgodi huu wa GGML unahitaji takribani jumla ya megawati 40 ili ujiendeshe na muda wote tangu kuanzishwa kwake umekuwa ukitumia jenereta za dizeli kuendesha mitambo hiyo, hivyo TANESCO italeta umeme wa gridi kutokea kituo cha kupoozea umeme cha mjini Geita na cha Mpomvu" alisema Mhe Waziri.
Sambamba na hilo serikali imepanga kupeleka umeme katika migodi 336 iliyopo nchini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa gharama ya shilingi bilioni 6 ili kazi za uchimbaji wa madini nchini zifanyike kwa tija zaidi.

Kituo cha kupoozea umeme wa msongo mkubwa wa Grid ya Taifa kilichopo mkoani Geita kitakachotumika kusambaza umeme kwenye maeneo ya mgodi wa Dhahabu wa Geita unaomilikiwa na mwekezaji GGML.
"Pamoja na migodi hiyo kusambaziwa umeme na REA, TANESCO pia ina mkakati wa kufikia migodi mingi zaidi kupitia mradi wa Gridi Mapato ambao tayari una mtaji wa shilingi bilioni 300 ambazo zitapeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi na viwanda vya uchenjuaji" alifafanua Waziri wa Nishati.
Halikadhalika Mhe Makamba alikagua shughuli za usambazaji umeme katika Jimbo la Busanda lililopo Halmashauri ya wilaya ya Geita na kujionea utekelezaji wake.
Katika Halmashauri hiyo ya Geita, jumla ya vijiji 26 tuu ndivyo vilivyounganishwa na huduma ya umeme kati ya vijijini 84 na hivyo kuahidi kuwa vijiji vilivyosalia vitasambaziwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya 3, mzunguko wa pili pamoja na mradi wa umeme wa Geita hadi Nyakanazi kwa vijiji vyote vinavyopitiwa na mradi huo.
Wakati huo huo Waziri wa Nishati Mhe January Makamba akiwa mjini Geita alikutana na wanawake wajasiriamali wanaojishughulisha na biashara ya kupika chakula na kuongea nao na kisha kuwaeleza mpango wa serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan wa kuwaondolea adha ya matumizi ya nishati ya kuni na mkaa na badala yake watumie nishati salama ya gesi ya kupikia.
"Mbali na matumizi ya kuni na mkaa kuchangia ukataji miti na kuharibu mazingira yetu, bado ule moshi wa kuni na mkaa unasababisha madhara makubwa kiafya ikiwemo ugonjwa wa mapafu, macho kuwa mekundu na kuwasha lakini pia sura za akina mama zinaharibika" alisema Waziri Makamba.
Huku akishangiliwa kwa vifijo na vigelele na wajasiriamali hao waliokusanyika eneo la kituo cha mabasi madogo cha Geita Mjini, Mhe Makamba aliendelea kusema kwanba,

Kazi za ujenzi zinaendelea katika moja ya maeneo ya mgodini GGML ambapo kasi ya maendeleo itaongezeka wakati umeme wa Grid ya Taifa utakapokuwa ukisambaa mgodini na kupunguza gharama za uendeshaji.
"Mimi nimetumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kama Waziri wake wa Nishati kuwaeleza kwamba, ameamua kuingilia kati adha zenu za kupika jikoni na hivyo serikali yake imebuni mkakati mpya wa majaribio ya matumizi ya gesi majumbani kwa miezi 6 kuanzia sasa hadi December ili kuja na mpango mahususi wa matumizi bora ya nishati salama ya gesi ya kupikia" aliwaeleza Mhe Makamba.
Nao wanawake wajasiriamali hao wa mjini Geita walimshukuru Rais Samia kwa hatua hiyo na kumkata Waziri Makamba afikishe shukrani zao kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan na kuahidi kutekeleza maagizo yake yote anayoyatoa kwao na kumtakia uongozi ulio mzuri kwa Taifa la Tanzania.
Katika ziara hiyo, Waziri January Makamba aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Rosemary Senyamule na Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe Wilson Shimo pamoja na Mbunge wa Geita Mjini Mhe Costantine Kanyasu.
Mwisho.





0 Comments