| Mbunge wa jimbo la Buyungu Mhe Aloyce Kamamba akitoa pongezi kwa Serikali kuboresha huduma za Afya katika Jimbo la Buyungu Kakonko mkoani Kigoma. |
Na Daniel Limbe,Kakonko
MBUNGE wa jimbo la Buyungu mkoani Kigoma,Aloyce Kamamba,ameipongeza serikali kwa uamuzi wake kuigeuza kituo cha afya iliyokuwa hospitali ya kuhudumia wakimbizi kutoka nchini Burundi baada ya kambi yao kufungwa rasmi mwaka huu.
Ni kutokana na wakimbizi hao kurejea nchini mwao kwa hiari, baada ya serikali ya rais Evariste Ndayishimiye,kuwahakikishia usalama wa maisha yao wananchi wote wa Burundi waliokimbilia nje ya nchi kutokana na machafuko ya kivita.
Akiwa katika eneo hilo,Mbunge Kamamba, amepokea taarifa ya maendeleo ya kituo hicho cha afya Mtendeli,kutoka kwa mganga mfawidhi Dk.Saimon Mafuru ambaye pamoja na mambo mengine amedai kuna uhaba mkubwa wa vifaa tiba,wataalamu wa afya,uchakavu wa majengo pamoja na kutokuwepo gari la wagonjwa.
“ Licha ya kwamba tunaendelea kutoa huduma za afya kwa wananchi bado kituo chetu cha afya Mtendeli kina kabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa vifaa tiba, uchakavu wa majengo,uchache wa watoa huduma, pamoja na ukosefu wa maji na umeme wa uhakika”amesema Dk. Mafuru
Hata hivyo amedai kwa sasa kuna watumishi saba pekee akiwemo Daktari mmoja,wauguzi pamoja na mfamasia huku akiiomba serikali kuboresha miundo mbinu ya kutolea huduma za afya kwa jamii hatua itakayosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Mbali na kuipongeza serikali kwa uamuzi huo mzuri kwa wananchi wa kata ya Kasanda,Kamamba ameiomba serikali kutenga fedha za kutosha ili kukifanyia ukarabati mkubwa kituo hicho cha afya baada ya kuchakaa na baadhi ya majengo kuwa nyufa zinazohatarisha usalama wa wagonjwa na watoa huduma.
Aidha amesisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kituo hicho kupewa gari la wagonjwa kwa lengo la kuwafikisha kwenye huduma kubwa za afya baadhi ya wagonjwa wenye uhitaji huo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mtendeli, Thomas Gwamikiko, amesema awali wananchi wake walikuwa wakipata huduma bora na zenye uhakika kabla ya wakimbizi wa Burundi kurejea kwao ukilinganisha na sasa ambapo huduma nyingi zimepungua.
Kwa upande wake,Tabu Kazilamihunde, anasema iwapo serikali itaamua kukiboresha upya kituo hicho kilichokuwa kikihudumiwa na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) hakika wananchi wa kata hiyo itawapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Mwisho.
0 Comments