Na Urban Epimark, DAR ES SALAAM
“AWATAKA MADIWANI NCHINI WAACHIWE KUJADILI PESA ZA MAENDELEO ZITAKAPOPELEKWA; MA-DC & MA-DED ACHENI KUVUTANA KUHUSU PESA ZA MIRADI”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa viongozi wenye mamlaka katika wizara ya TAMISEMI wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya kote nchini kuacha kuvutana kuhusu pesa za serikali zinapoletwa kwenye mikoa yao na kuagiza mabaraza ya madiwani kote nchini waachiwe kujadili pesa zitakapo elekezwa kwenye miradi ya maendeleo na wao kutekeleza.
Pia ameonya mapato ya serikali kwenye maeneo yenye madini kuto kukusanywa vizuri na akatoa mfano wa wilaya ya Malinyi katika mkoa wa Morogoro kuwa ilikuwa haifanyi vizuri katika kukusanya mapato lakini baada ya kumpeleka Mkuu wa mkoa mwingine na Mkuu wa wilaya, Halmashauri ya wilaya ya Malinyi sasa inafanya vizuri ajabu kwa ukusanyaji mapato.
Rais Samia ameeleza hayo kwa viongozi wapya wa mikoa alio wateua na leo kuwaapisha wakiwemo Wakuu wa Mikoa 9 na Makatibu Tawala pamoja na wakuu wa taasisi za umma Ikulu jijini Dar es Salaam.
"Nimewateua ninyi Ma-RC na Ma-RAS wapya na pia wale nilio wahamisha ili muende mkaongeze nguvu kwenye maeneo mengine katika kutekeleza azma ya serikali kuwaletea wananchi maendeleo. Nimewateua kulingana na sifa, uwezo na uaminifu wa mtu kwa taifa lake na serikali yake na si vinginevyo. Sijaangalia sura ya mtu, kabila, rangi au imani yake ya dini" amesema Rais Samia.
Rais Samia aliendelea kueleza kwamba anawataka wakatekeleze majukumu makubwa mawili yaani kukusanya mapato ya serikali na kusimamia vizuri utoaji huduma kwa wananchi na kuongeza kwamba mapato mengi ya serikali kwenye eneo la TAMISEMI hayakusanywi wala kusimamiwa vizuri.
"Serikali inapeleka pesa nyingi huko chini ngazi ya mikoa na wilaya, zaidi ya asilimia 70% ya pesa za serikali zinaelekezwa TAMISEMI lakini usimamizi sio mzuri na pia mapato yanayokusanywa ni madogo mno" amesa Mhe Rais.
Ametoa mfano wa ukusanyaji mapato dhaifu kwenye Halmashauri ya wilaya ya Malinyi katika mkoa wa Morogoro kwamba, ilikuwa haikusanyi vizuri mapato hadi kushindwa kumudu kutoa huduma muhimu kwa wananchi lakini serikali ilipoamua kumpeleka Mkuu wa mkoa mwingine kuwa RC wa Morogoro na pia kumteua DC mwingine wilaya ya Malinyi, makusanyo yalifanyika vizuri na sasa Halmashauri ya wilaya ya Malinyi inafanya vizuri mno kimapato.
Ametoa mfano wa maeneo yenye migodi na uchimbaji madini kwamba, mapato hayakusanywi vizuri na akawataka ma-RC na ma-RAS waliopelekwa kwenye maeneo hayo wakahakikishe mapato ya serikali kwenye maeneo ya madini yanakusanywa vizuri.
Wakati huo huo Mheshimiwa Rais Samia amemuonya Mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe Albert Chalamila aache utoto na mizaha anapokuwa kazini na akafanye kazi yake ipasavyo na yeye Mheshimiwa Rais ataendelea kumfuatilia kwa karibu.
"Mhe Chalamila nimekuteua tena uende kunisaidia kuusimamia mkoa wa Kagera. Nakutaka uache utoto. Naamini umekuwa sasa, na usiende kubweteka tena nitaendelea kukufuatilia" alimuusia Rais Samia.
Halikadhalika amewataka wakuu wa mikoa walioteuliwa kutoka maeneo ya jeshini wasitumie kombati zao wanapoenda kuwatumikia wananchi uraiani bali waziache jeshini hadi watakaporejea tena huko wakitoka uraiani.
![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akimwapisha Albert John Chalamila kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo August 01, 2022 |
Nae waziri wa TAMISEMI Mhe Innocent Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini na kumkabidhi kuiongoza wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na wenzake na hivyo kuahidi kumsaidia kusimamia vizuri maendeleo ya wananchi kwa niaba yake.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Tulia Ackson nae ameshukuru Mheshimiwa Samia kwa kuwateua viongozi hao kwa imani kwamba wataenda kusimamia vyema zoezi la sensa ya watu na makazi ili bunge liweze kupanga vyema malengo ya maendeleo na pia kuisimamia vyema serikali kwa kufuata takwimu zitakazopatikana wakati wa sensa ya watu na makazi.
Katika mabadiliko na uteuzi wa wakuu wapya wa mikoa pamoja na makatibu tawala, Mkoa wa Geita umepata RC na RAS mpya ambao tayari wameshaapishwa rasmi leo.
![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akimwapisha Fatma Abubakar Mwasa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo August 01, 2022 |
Kesho Agosti 02, 2022 na kuendelea wakuu wote wa mikoa na makatibu tawala kote nchini wataanza semina maalum ya kupatiwa elimu na malengo ya kuyatekeleza ambapo Mheshimiwa Rais Samia mwenyewe atahudhuria kwenye semina hiyo.
Mwisho.





0 Comments