![]() |
| Muhudumu wa Afya akijiandaa kutoa huduma za utabibu na afya kwa mzee. Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe Martin Shigela ameagiza uzingatiaji sheria kuhudumia wazee mkoani Geita. |
Na Urban Epimark, GEITA
Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe Martin Shigela amemtaka Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita Dr Japhet Simeo kuwaandikia barua watumishi wote wa Idara ya Afya mkoani Geita kuwakumbusha kuzingatia sheria na kutoa huduma za afya kwa usahihi kwa wazee kwani serikali haijatoa vitambulisho vya matibabu kwa wazee kujifurahisha bali imevitoa ili vitumike kuwahudumia.
Mhe Shigela ametoa maagizo hayo wakati wa mkutano wake na wazee wa mji wa Geita na viongozi wa dini uliowashirikisha pia wataalam mbalimbali wa Idara za serikali uliofanyika mwanzoni mwa juma hili mjini Geira ili kujitambulisha na pia kupokea maoni yao na michango yao ya mawazo.
"Ni vyema Mganga Mkuu ukawakumbusha tena watumishi wote wa Idara ya Afya kwa kuwaandikia barua kuzingatia sheria lakini pia ni vyema wakatambua kuwa serikali haijatoa vitambulisho vya matibabu kwa kujifurahisha, inatoa kwa kumaanisha ili wazee wapewe huduma za afya bila malipo hivyo wasipuuzwe" aliagiza Mkuu wa mkoa.
Ilimbidi Mkuu wa mkoa kutoa maagizo hayo kufuatia hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Halmashauri ya Mji wa Geita katika mkutano huo Bw Manoni Wiliam Mgema kwamba pamoja na wazee kupatiwa vitambulisho au hata barua za kupatiwa huduma za matibabu bila malipo, wanapoenda kupata huduma hizo watumishi wa Afya wanawapuuza.
Akitoa ufafanuzi na baadhi ya majibu ya hoja za wazee kuhusu huduma za afya, Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita (RMO-GEITA) Dr Japhet Simeo aliueleza mkutano huo kwamba anakiri zipo changamoto kama hizo kwa baadhi ya watumishi, na hivyo kuahidi kwa Mkuu wa mkoa kutekeleza maagizo yake.
"Mhe Mkuu wa mkoa ni kweli zipo changamoto hizo kwa baadhi ya watumishi katika Idara ya Afya wasio zingatia miongozo na sheria, na hata leo asubuhi nimechelewa kuingia katika mkutano huu sababu palitokea mzee mmoja alifika ofisini kwangu kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa hapa Geita na kuleta hoja yake inayofanana na hiyo, hivyo mimi na Mganga Mfawidhi ikabidi kulishughulikia na kumsaidia ili apate huduma" alifafanua hivyo Dr Simeo.
Dr Simeo aliendelea kueleza zaidi pia kwamba, Idara yake inatambua na kuthamini utoaji huduma za matibabu kwa wazee bila malipo na akatoa takwimu za jinsi serikali katika mkoa wa Geita imekuwa ukitoa huduma hizo kwa kugharamia matibabu ya wazee tangu miaka mitano iliyopita.
![]() |
| Mganga Mkuu wa mkoa wa Geita (RMO-GEITA) Dr Japhet Simeo (pichani) akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zinazohusu Idara ya Afya katika moja ya mikutano ya kiutendaji katika mkoa wa Geita. |
RMO alitaja idadi ya wazee waliopo katika mkoa huu wa Geita kulingana na taarifa ya sensa ya mwaka 2012 kuwa wapo jumla ya elfu 59, lakini akaongeza kwa kusema kwamba, idadi hiyo huenda ikaongezeka baada ya matokeo ya sensa ya mwaka huu 2022.
"Miaka mitano iliyopita kuanzia 2015 hadi 2020, mkoa wa Geita imetoa huduma za matibabu ya kujirudia bila malipo kwa wazee elfu 60 kwa gharama ya shilingi bilioni 1,320,000,000 na kuanzia mwaka 2021 hadi sasa mwaka 2022, serikali umetoa huduma kama hizo kwa wazee 18,072 kwa gharama za shilingi milioni 397,584,000" ameeleza Dr Simeo.
Mkutano huo baina ya Mkuu wa mkoa na wazee pamoja na viongozi wa dini ililenga RC na RAS mpya kujitambulisha na pia kuomba baraka na hekima zao kabla hawajaanza majukumu yao rasmi ili wajue pa kuanzia.
Mkutano huo ulikuwa wa ufanisi mkubwa kwani mwitikio wake ulikuwa mzuri na Mkuu wa mkoa Mhe Martin Shigela aliwashukuru wazee hao kwa kumkaribisha yeye na RAS mpya vizuri na kuwaahidi kuwapa ushirikiano mkubwa wakati wote wa kutekeleza majikumu yake.
Mwisho.




0 Comments