![]() |
| Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita (Acting RAS Geita) Herman Materu akiongea wakati akifunga mkutano wa MDH uliokutana kwa siku mbili mjini Geita August 03, 2022. |
Na Urban Epimark, GEITA.
Serikali katika mkoa wa Geita imelipongeza shirika linalotoa huduma za afya hapa nchini MDH kwa kazi kubwa na nzuri inalofanya na kuisaidia sekta ya afya kutoa huduma bora kwenye eneo la walio ambukizwa VVU na utoaji chanjo ya UVIKO-19.
MDH katika mkoa wa Geita imesaidia kwa kiwango kikubwa katika ukusanyaji wa takwimu za walengwa kwa wakati, kujenga miundombinu bora ya utoaji huduma za afya na pia kusaidia upatikanaji wa rasilimali watu na fedha za kutoa huduma hizo.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agust 03 mjini Geita na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa (Acting RAS-Geita) Bw Herman Materu wakati wa kufunga mkutano wa siku mbili wa wadau na wataalam wa Afya wa timu ya MDH mkoa wa Geita uliojadili utendaji wake kwa kioindi cha robo ya tatu ya mwaka (mwezi April hadi Juni 2022) uliokutana kwa siku mbili August 02 na 03 katika ukumbi wa EPZ.
"Kwa niaba ya serikali ya mkoa wa Geita, nalipongeza shirika la MDH kwa mchango mkubwa inalotoa kwa serikali kupitia sekta ya afya kwenye eneo la upimaji maambukizi ya VVU kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto na pia uchanjaji wa UVIKO-19, hongereni sana" alisema Kaimu RAS GEITA.
Kaimu RAS aliendelea kueleza maeneo MDH imekuwa ikitoa mchango mkubwa ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa takwimu za walengwa kwa wakati, ujenzi wa miundombinu bora na ya uhakika ya utoaji huduma za afya kwa waliogundulika na pia ajira kwa rasilimali watu wenye utaalum pamoja na fedha za kuwezesha mambo yote hayo, alisema.
"Nimeelezwa na Mganga Mkuu wa mkoa (RMO-GEITA) Dr Japhet Simeo kwamba katika eneo la kuibua na kukusanya takwimu za wenye VVU na kuwaanzishia huduma za matibabu pamoja na kuhakikisha maabukizi yanafifishwa au kuzibitiwa, mmekuwa imara sana na hivyo sisi serikali tunawapongeza. Tunatoa ahadi kwenu kwamba serikali ya mkoa wa Geita itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa MDH ili malengo na maazimio yote mliyo jiwekea katika mkutano huu yaweze kufikiwa" aliongeza Bw Materu.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa MDH hapa nchini (CEO) Dr David Sando ametoa shukrani nyingi kwa serikali kwa ushirikiano mkubwa inayo toa kwa MDH na kuahidi kuwa tayari kupokea ushauri na miongozo ya jinsi ya kuendelea kuimarisha huduma zao hapa nchini na pia mkoani Geita.
"Uongozi wa MDH unatoa shukrani nyingi kwa ushirikiano mkubwa tunaoupata kutoka kwenye serikali ya mkoa wa Geita, ikiwemo ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa (RMO Geita), ofisi za waganga wakuu wa Halmashauri zote za mkoa wa Geita (DMO) na wataalum wote wa utoaji huduma za afya katika kuhakikisha utekekezaji na ufanisi wa afua ya Ukimwi na Uchanjaji wa UVIKO-19 unafikiwa vyema" amesema CEO wa MDH.
CEO Dr Sando aliendelea kueleza kwamba huduma kwa wanaoishi na virusi vya ukimwi kwenye hospitali zetu pamoja na vituo vya afya zitaendelea kutolewa na MDH hapa nchini kulingana na miongozo ya wizara ya afya.
Halikadhalika Dr Sando ameongeza kwamba, kuanzia mwaka jana 2021 MDH imekuwa ikifanya kazi kwa pamoja na wizara ya afya katika utoaji chanjo ya UVIKO-19 na pia kuhakikisha vikwazo vyote vinavyojitokeza katika uchanjaji vinafanyiwa kazi na kuondolewa na kumwakikishia Kaimu RAS kwamba mkoa wa Geita utabakia kuwa kinara wa uchanjaji kati ya mikoa mingine kama ilivyo sasa, alisema CEO Dr Sindo.
Awali akitoa marejeo kuhusu yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe Dr Deograsia Mkapa alimweleza Mgeni Rasmi Kaimu RAS wa mkoa wa Geita kwamba,
"Mkutano huu wa siku mbili tumeweza kupitia takwimu za utekekezaji mpango wa wa upimaji VVU kwa wenye maambukizi na kuhakikisha walengwa wanajifahamu hali zao na pia kuwaingiza katika mpango wa huduma zinazotolewa kwa wanaoishi na VVU kulingana na utaratibu wa wizara ya afya na kuwahudumia hadi kuhakikisha maambukizi yanazibitiwa kwa waliougundulika na kurejea kwenye shughuli zao za kiuchumi" alisema DMO wa Bukombe.
Pia katika eneo la uchanjaji UVIKO-19 Dr Mkapa alimweleza Kaimu RAS kwamba yamepatikana mafanikio makubwa kwani idadi ya watu waliokusudiwa kupatiwa chanjo hiyo ya UVIKO-19 katika mkoa wa Geita ilifikiwa na kuvuka kupitia zote maalum la uchanjaji ambalo lilifanyika mwezi Juni mwaka huu hapa mkoani.
Mkutano huo uliwashirikisha pia Wakurugenzi na Mameneja wa shirika la MDH kutoka Makao makuu jijini Dar es Salaam, wataalam wa Idara ya Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri zote za mkoa wa Geita.
Halikadhalika pamoja na timu ya utekelezaji mpango wa Mradi wa Afya wa shirika hilo la MDH kwa mkoa wa Geita, mkutano huo ulitoa pia pongezi nyingi kwa mpangilio mzuri wa uwasilishwaji wa mada za kujadili ambapo CEO wa MDH Dr David Sando alimpongeza Meneja wa Mradi wa MDH katika mkoa wa Geita (RPM-Geita) Dr Nicholaus Tarimo kwa maandalizi na uongozi mzuri uliowezesha yote hayo kwa ubora, hivyo kuonesha ukomavu katika utendaji.
Mwisho.










0 Comments