TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WANANCHI WAASWA KUWATHAMINI WENYE ULEMAVU KAKONKO

Pichani katikati ni Mhe Aloyce Kamamba Mbunge wa Jimbo la Buyungu,ambapo katika ziara yake amegawa baiskeli saba kwa walemavu wa viungo wilayani Kakonko.

Na Daniel Limbe,Kakonko.

SERIKALI wilayani Kakonko Mkoani Kigoma imewataka wananchi kutowanyanyapaa watu wenye ulemavu badala yake kuwajali,kuwahudumia na kuwapa mahitaji yote ya kibinadamu.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa Wilaya hiyo,Kanali Evance Mallasa,Wakati akishuhudia makabidhiano ya baiskeli saba za walemavu zilizokabidhiwa na Mbunge wa jimbo la Buyungu,Aloyce Kamamba,kwa walengwa kata mbalimbali.

Mallasa amesisitiza jamii kuendeleza kuwathamini walemavu hao kwa madai kuwa ulemavu siyo ugonjwa na kwamba hayo ni maumbile ambayo Mwenyezi Mungu ilimpendeza kufanya hivyo.

Akikabidhi msaada huo,Mbunge Kamamba,amedai analazimika kuzitumia fursa zote za maendeleo ambazo zinamanufaa kwa wananchi wa jimbo lake kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na fursa hizo.

Mbunge wa Jimbo la Buyungu Mhe Aloyce Kamamba akiwakabidhi baiskeli wenyeulemavu  katika jimbo lake, aliyesimama mbele ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Siasa walioambatana nae kwenye ziara ya kuhamasisha shughuli za Maendeleo Kakonko.

Aidha amewasisitiza kuzitunza baiskeli hizo Ili ziweze kuwasaidia kurahisisha shughuli zao Kwa kujitafutia kipato na kuinua uchumi wao.

Kwa upande wake kaimu Ofisa ustawi wa jamii Wilaya ya Kakonko, Hellen Hurdson,mbali na kumpongeza Mbunge huyo ameomba msaada kama huo uendelee kutolewa kutokana na Wilaya hiyo kuwa na walemavu zaidi ya 1790.

Akiongea kwa niaba ya wenzake,Neema Bakari,ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Kasungwa ameshukuru Kwa msaada huo na kwamba baiskeli hiyo itamsaidia kufika shuleni Kwa wakati.

Mbunge wa Jimbo la Buyungu Mhe Aloyce Kamamba akiwasabahi wenye ulemavu mara baada ya kuwapatia baiskeli zitakazo wasaidia kutembea ambapo amewasisitiza kuzitunza baiskeli hizo.

Msaada wa baiskeli hizo unatarajiwa kuwa endelevu baada ya wahisani shirika lisilo la kiserikali la "Peace for Conservation" la jijini mwanza kuahidi kumfadhili Mbunge huyo baiskeli zingine 13 ambazo kila moja itagharimu kiasi cha shilingi 500,000 Ili kuunga mkono juhudi zake za maendeleo kwa jamii.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments