TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

TANZANIA INA CHAKULA CHA KUTOSHA: RAIS SAMIA.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye sherehe ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) iliyofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa leo Sept 11, 2022

Na Urban Epimark, DAR ES SALAAM 

Ingali mataifa mengi yanayoizunguka Tanzania wakipata hofu ya upungufu wa chakula kutokana na kupungua kwa mvua za msimu na nchi nyingine kukabiliwa na ukame, lakini Tanzania inayo akiba ya kutosha ya chakula cha kuweza kukidhi mahitaji miaka 3 ijayo.

Tanzania kwenye ghala zake za chakula ina tani takribani Laki moja unusu baada ya serikali hivi karibuni kuongeza fedha za ununuzi wa nafaka kwa ajili ya akiba kutoka tani elfu 50 miaka tatu iliyopita hadi kufikia tani laki moja na nusu hivi sasa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo leo alipokuwa akiwahutubia Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa WAWATA na kisha yeye kushiriki kama Mgeni Rasmi.

"Nimepokea risala yenu ninyi Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) mkionesha hofu yenu kuhusu uhakika wa chakula cha kutosha kwa mahitaji ya nchi yetu yaani Food Security, lakini nawahakikishia nchi yetu inajitosheleza kwa akiba ya chakula. Tunazo jumla ya tani Laki moja na nusu kwenye ghala zetu" ameeleza Rais Samia.


Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kutoka majimbo yote nchini yanayosimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania-TEC wakimsikiliza Mgeni Rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) alipowahutubia katika sherehe ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, iliyofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa leo Sept 11, 2022

Aliendelea kufafanua zaidi  kwamba pamoja na upungu wa mvua za msimu katika nchi yetu na hata nchi nyingine za jirani zinazo izunguka Tanzania kukumbwa na ukame wa mvua na kusababisha tishio la njaa, lakini sisi Tanzania akiba tuliyonayo ya chakula inatutosha kwa kukidhi uhitaji kwa wananchi wetu kwa takribani miaka 3 ijayo, aliongeza kwa kusema hivyo.

Rais Samia aliwapongeza WAWATA pamoja na Baraza la Maaskofu hapa nchini kwa kusaidia mpango wa malezi kwa watoto na vijana wanao chipua na kusifia program ya WAWATA chipuzi ambapo ni njia nzuri ya kueneza malezi na utamaduni mzuri wa kimalezi kutoka kwa wanawake wakatoliki kuja kwa wasichana wanaochipukia katika makuzi na kusema kwamba kunasaidia kudumisha maadili mema kwa kizazi kijacho.

"Nawapongeza sana WAWATA na nimetiwa moyo sana na program ya WAWATA Chipukizi, kwani program hii itasaidia sana  kuandaa vyema vijana kuwa viongozi wa kesho", alisema Rais Samia.


Baadhi ya Mawaziri pamoja na viongozi mbalimbali walihudhuria na kushiriki kwenye sherehe ya Jubilee ya miaka 50 ya WAWATA iliyofanyika leo uwanja wa Benjamin Mkapa leo Sept 11, 2022 Mgeni Rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan. Katika picha ni Waziri katika Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe Jenista Mhagama akifuatiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe Angelina Mabula pamoja na viongozi wengine.

Halikadhalika amewapongeza WAWATA kwa jitihada zao za kujenga na kukuza ujasiriamali hapa nchini na pia kupongeza jinsi WAWATA walivyojipambanua kupeana mikopo ya kifedha katika harakati za kukuza uchumi katika ngazi ya familia na pia Rais Samia  alipokea changamoto au dhamira yao ya kutaka kuanzisha "WAWATA MICROFINANCE"

"Katika hatua hii mmepanga kuanzisha MICROFINANCE yenu, ambayo itawahakikishia fursa nzuri zaidi ya kupeana mikopo nawaahidi kwamba, Serikali itahakikisha inawasaidia jambo hili ili WAWATA muweze kupata MICROFINANCE yenu na nitawaagiza wasaidizi wangu Serikalini walifanyie kazi jambo hilo lifanikiwe kwa haraka" aliongeza Rais Samia. 

Kuhusu suala la kuhifadhi mazingira ambalo WAWATA walilizungumzia katika risala yao, Rais Samia amesema hata serikalini suala la kutunza na kuhifadhi mazingira ni jambo mtambuka na hivyo akawapongeza WAWATA kuisaidia serikali yao kutoa hamasa kwa jamii kutunza mazingira.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akitembelea maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wakati wa sherehe ya Jubilee ya miaka 50 iliyofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa leo Sept 11, 2022

Kisha Rais Samia aliwataka WAWATA kuweka msisitizo zaidi katika mambo matano ambayo ni kusaidia malezi ya watoto na vijana ili wakue katika maadili mema huku akinukuu maandiko matakatifu kutoka kitabu cha 1Yohane 4:4 

"..... Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye  ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu" mwisho wa kunukuu.

Hivyo akaongeza kusema kwamba, wanawake ni jeshi lenye nguvu, wazitumie kuwalinda vijana wetu wasipotoke kimaadili.


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa'ichi (mwanzo kulia) akiwa na maaskofu wengine wakati wa sherehe ya Jubilee ya miaka 50 ya WAWATA iliyofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa leo Sept 11, 2022

Jambo la pili alilowataka WAWATA walifanye ni kutoa elimu ya uongozi  kwa wanawake ili kuwa tayari kuandaa viongozi mbalimbali walio bora, huku akichota hekima kutoka kwenye kitabu cha Joshua 1: 9 kinachosema, "wanawake muwe shujaa na jasiri kwani Mungu yu pamoja nanyi...."

Amewataka WAWATA kusimama kwa ujasiri kutunza heshima ya jamii kwa kusaidia kupata viongozi jasiri na wenye kutunza heshima kwa Taifa letu.

Mambo mengine aliyowataka WAWATA wasaidie kufanya ni kushiriki vyema katika kukuza tija na uchumi wa Taifa, kuelimisha jamii kuhusu dhana ya kweli katika kushiriki mambo ya siasa na kutunga sera mbalimbali za kunufaisha jamii.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akiwasalimu Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) pamoja na wageni na washiriki wengine wakati alipoingia uwanja wa Benjamin Mkapa kuhudhuria sherehe ya Jubilee ya miaka 50 ya WAWATA leo Sept 11, 2022

Pia Rais Samia amewataka WAWATA kutoa elimu kwa vijana kuhusu matumizi mazuri na sahihi ya teknolojia ya mawasiliano na kuwauliza wazazi wote nchini kwamba, je? wao katika jambo hili wamesimama upande upi na kusema kwamba, "Natoa rai kwa WAWATA na wanawake wote nchini  tushikamane ili tujenge nchi yenye maadili.  Serikali itaendelea kushirikiana na WAWATA  na wanawake wote na kamwe serikali haitakubali kuona wanawake mnarudi nyuma" alisisitiza Rais Samia.

Pia akaongeza kwamba, serikali ingependa kuona WAWATA inasaidia malezi kwa jamii, kuondoa unyanyasaji kwa wanawake na kwa wanaume, na kuwataka WAWATA wayafanyie kazi manyanyaso yaondoke kwenye jamii.


Washiriki katika sherehe ya Jubilee ya miaka 50 ya chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wakishuhudia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika uwanja wa Benjamin Mkapa leo Sept 11, 2022

Nae Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania-TEC Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mhashamu Gervas Nyaisonga amemshukuru Rais Samia kwa kuliheshimisha kanisa kwa kukubali kushiriki nao kama Mgeni Rasmi katika Jubilee hiyo ya miaka 50 ya WAWATA na kusema kwamba kumewatia moyo na khari ya kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii zaidi. 

Halikadhalika Askofu Nyaisonga ameongeza kwamba, kanisa litaendelea kushirikiana na serikali kutekeleza yale yote Rais Samia aliyoshauri na kuongeza kwamba  yatasaidia kuleta ustawi bora wa jamii nzima.

Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania yaani WAWATA kilianzishwa rasmi hapa nchini mwaka 1972, na kwa muda wote huo kimekuwa kikitoa malezi ya jamii kiroho na kimwili kikisaidiana na jamii nzima ikiwemo serikali na kusaidia pia kulea na kukuza viongozi mbalimbali wa kanisa na wengine wengi kwa upande wa serikali pia.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments