
Mkuu wa wilaya ya Sengerema Senyi Ngaga akizungumza katika uzinduzi wa miongozo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya elimu Msingi na Sekondari
Na Anna Ruhasha, Sengerema.
Walimu wa shule za Msingi na Sekondari Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza wameonywa kutotumia viboko kupita kiasi kama njia ya ufundishaji kwa wanafunzi jambo ambalo linapelekea wanafunzi kuchukia masomo pamoja na kuacha shule.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Sengerema Mhe Senyi Ngaga wakati akizindua miongozo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya Elimu Msingi na Sekondari kwa lengo la kuboresha Elimu katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Sengerema.
Amesema kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya walimu kuwachapa viboko wanafunzi kila siku hali ambayo inasababisha wanafunzi kuwa watoro na kuichukia shule.
Afisa elimu shule za msingi katika halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mwl. Donalti Bunonos amesema kuwa miongozo hiyo itakuwa chachu ya kuboresha ufundishaji kwa wanafunzi na kuahidi kwenda kuitekeleza ipasavyo.
Nao baadhi ya wakuu wa shule wameahidi kwenda kuisoma na kuielewa miongozo hiyo ili iweze kuwasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika shule zao.
Mwisho
0 Comments