TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA MKOA WA GEITA.


Mkuu wa Mkoa Geita Mhe Martine Shigela akiongea na wanahabari ofisini kwake mtaa wa Magogo mjini Geita leo Oktoba 13,2022

Na Urban Epimark, GEITA.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi mkoani Geita kwa siku mbili October 15 & 16, 2022.

Akitoa taarifa hiyo ofisini kwake mtaa wa Magogo  mapema leo October 13, 2022 Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela amesema Mhe Rais Samia atapokelewa wilayani Chato akitokea mkoani Kagera na kutoa wito kwa wananchi wa wilaya ya Chato na viongozi mbalimbali wa mkoa kujitokeza kuanzia 12:00 asubuhi kumpokea.

"Naomba kutoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Geita pamoja na viongozi mbalimbali ngazi ya mkoa, viongozi wa dini, wazee na wale wa Chama cha Mapinduzi tujiandae kumpokea Mgeni wetu, ambapo ni mara ya kwanza kufanya ziara ya kikazi mkoani Geita tangu alipo apishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" alifafanua Mhe Shigela. 

Mkuu wa mkoa aliendelea kueleza kwamba, baada ya Mhe Rais Samia kupokelewa ataenda moja kwa moja hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Chato na kupokea taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo na kuitembelea ili kujionea hatua iliyofikiwa.

Wanahabari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela ofisini kwake mjini Geita leo Oktoba 13,2022.

Kisha Mhe Rais atasafiri kwa gari kuelekea moja kwa moja Kata ya Buseresere na Katoro mpakani mwa wilaya za Chato na Geita ambapo ataongea na wananchi kabla ya kuelekea kituo cha kupoozea umeme cha Mpomvu ambapo  atapokea pia taarifa ya ujenzi wa kituo hicho cha umeme na kukikagua.

Mchana saa 7:00 ataelekea eneo la kiwanda kipya cha kusafishia madini ya Dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) atapokea taarifa ya kiwanda hicho na kukuzindua rasmi.

Baada ya kufungua kiwabda hicho, Mhe Rais Samia atafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa CCM Kalangalala na kuhutubia umma mzima wa Geita na hapo, wananchi, viongozi wa dini na wa Chama cha Mapinduzi watapata fursa ya kumweleza changamoto zilizopo katika mkoa wa Geita. 

Wanahabari wakiuliza maswali kwa Mkuu wa Mkoa Geita Mhe Martine Shigela ili kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali kuhusu ugeni wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Geita Oktoba 15&16, 2022.


Mhe Shigela alifafanua zaidi kwamba, Mheshimiwa Rais atahitimisha ziara yake siku ya kwanza katika mkutano huo Uwanja wa CCM Kalangalala kisha kwenda kupumzika na kesho yake October 16, 2022 atatembelea wananchi wa Geita kupitia Runzewe wilayani Bukombe na kuongea na wananchi. 

Mkuu wa mkoa ametoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo ya Runzewe na Bukombe kujitokeza kwa wingi hapo kesho kumpokea Mhe Rais na kuongea nao  kisha ataelekea tena mkoani Kagera kuendelea na shughuki za kikazi.

Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe Martine Shigela amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kuhakikisha hadi ifikapo leo October 13, 2022 majira ya saa 9:00  alasiri, vitabu vyote vya kupokelea wageni katika nyumba za wageni (Guest Houses) vilivyo chukuliwa na watendaji wa Halmashauri viwe vimerudishwa vyote kwa wenyewe.

Mkuu wa mkoa ametoa maagizo hayo baada ya kuulizwa na wanahabari kwamba, wenye nyumba za wageni (Guest Houses) Mjini Geita wana malalamiko  huenda wakagoma kutoa ushirikiano kwa ugeni utakao kuja na Mhe Rais.

Hii ni kutokana na hali ya sintofahamu iliyopo baina ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita na wenye nyumba za wageni kuhusu malipo ya kodi na tozo zingine za Halmashauri na hivyo kutoa wito kwamba, mambo ya kodi Mkurugenzi wa Mji  akae pamoja na wafanyabiashara hao wayatatue lakini hataki aibu au mizozo katika mkoa wake, amesema Mkuu wa mkoa.

Moja ya nyumba za kulala wageni zilizopo Mjini Geita, "Harvest Hotel"


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments