TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WASANII GEITA WACHANGIA DAMU

Uchangiaji Damu Salama kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu imeelezwa na Chama cha Wasanii wa filamu na picha jongefu wa mkoa wa Geita (TDFAA) kwamba sasa ni jambo la muhimu wala sio hiari tena.

Na Urban Epimark,  GEITA

Suala la kuchangia damu salama kuokoa maisha ya wagonjwa hospitalini na wanaopata ajali limeelezwa sasa kuwa ni la muhimu kwa jamii na sio tena jambo la hiari.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa chama cha wasanii wa filamu na picha jongevu wa mkoa wa Geita (TDFAA) Bi Rosemary Michael kwenye maonesho yanayoendelea mjini Geita ya teknolojia ya madini na uwekezaji. 

"Uhitaji wa damu ili kusaidia wagonjwa hospitalini pamoja na akina mama wanaojifungua na wanao pata ajali kwa sasa ni mkubwa hivyo si jambo la hiari tena bali ni la muhimu" alieleza Mwenyekiti wa wasanii.

Waziri wa Madini Mhe Dkt Doto Biteko (kulia) akipatiwa maelezo na mtumishi wa Benki ya Damu Bi Angelina Swai (kushoto) jinsi uchangiaji wa damu ulivyokuwa wa mafanikio makubwa baada ya kampuni ya GF Trucks & Equipments kufadhili mpango huo kwenye maonesho ya 5 ya kitaifa ya teknolojia ya madini na uwekezaji mjini.

Bi Rosemary Michael aliongeza kwa kusema wasanii kama sehemu ya jamii jukumu lao kubwa ni kutoa elimu kwa njia ya kuhamasisha jamii kujua jukumu hilo kwa kupitia kazi zao za usanii.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo aliongeza kwa kusema kwamba, wasanii tunao wajibu wa kuchangia pia damu ili kuokoa maisha ya wengine waliopo hospitalini na kwingineko.

Kikundi cha wasanii wa filamu na picha jongevu cha mkoa wa Geita (TDFAA) wakiwa kwenye banda la kituo cha Benki ya Damu kwenye maonesho ya 5 ya kitaifa ya teknolojia ya madini na uwekezaji mjini Geita baada ya kuchangia damu baada ya kuwezeshwa na kampuni ya GF Trucks & Equipments. Katika picha wa Nne kutoka kulia (walio simama) ni Mratibu wa huduma ya damu salama mkoa wa Geita Bw Charlse Mateso na wa tatu kutoka kushoto (walio simama) ni Mwenyekiti wa TDFAA mkoa wa Geita Bi Rosemary Michael pamoja na wasanii wengine.

Halikadhalika ameishukuru kampuni ya GF Trucks & Equipments ya mjini Kibaha mkoa wa Pwani kwa kufadhili wasanii hao kuweza kuchangia damu pamoja na gharama zingine kuwezesha majukumu yao.

Nae Mratibu wa huduma ya damu salama katika mkoa wa Geita Bw Charlse Mateso  amewashukuru wasanii hao kwa moyo wao wa kizalendo wa kuchangia damu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasanii wa filamu na picha jongefu wa mkoa wa Geita Bi Rosemary Michael (wa kwanza kulia walio keti) akiwa na Mratibu wa huduma ya Damu Salama wa Mkoa wa Geita Bw Charles Mateso (wa pili kutoka kulia walio keti) wakiwa katika picha ya pamoja na wasanii wa mkoa wa Geita mara baada ya wasani hao kuchangia damu kwenye maonesho ya 5 ya kitaifa ya teknolojia ya madini na uwekezaji mjini Geita.

Bw Mateso alibainisha zaidi kwamba, uhitaji wa damu kwa mkoa wa Geita ni wastani wa chupa 450  kwa mwezi ambapo mahitaji makubwa yapo kwa akina mama wanao jifungua pamoja na watoto chini ya miaka 5.

Kituo hicho cha benki ya damu salama cha Halmashauri ya Mji wa Geita kilijiwekea lengo la kupata chupa 210 za damu kwa muda wa siku katika maonesho haya ya madini lakini kwa muda wa siku 5 tangu maonesho yaanze Sept 27, 2022 tayari wameshapata jumla ya chupa 153 sawa na asilimia 73 ya lengo.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments