TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

ZAIDI YA WATU 500,000 KUPATIWA CHANJO YA UVIKO 19 MKOANI GEITA

 Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela

Na Salum Maige,Geita.

Takribani Wananchi 513,313 katika mkoa wa Geita wanatarajiwa kufikiwa na huduma ya chanjo ya Uviko 19 kwa muda wa siku tano, ikiwa ni mwendelezo wa serikali katika kuwakinga wananchi dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa huo.

Utekelezaji wa Kampeni hiyo unasimamiwa na serikali kupitia wizara ya Afya Kwa kushirikiana na Shirika la Amref Health Africa Kwa Ufadhili wa Shirika la GIZ.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo,Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Geita,Wille Luhangija amesema kuwa,zoezi hilo litaanza kufanyika Oktoba 17 hadi Oktoba 22,mwaka huu.

Alifafanua kuwa,matarajio ya kuwafikia wananchi hao inatokana na mwitikio mkubwa wa wananchi wa mkoa wa Geita kuhamasika kujitokeza kupata huduma ya chanjo hiyo tangu ilipoanza kutolewa na serikali kupitia wizara ya Afya Agosti 3,mwaka 2021.

Tutawafikia wananchi katika maeneo yote,huduma hii inatolewa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma ya Chanjo,lakini pia tutatoa huduma hii kwenye maeneo ya makazi(nyumba)mikusanyiko ya watu kama vile magulio,mashuleni kwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 18”alisema Luhangija.

Aliongeza kuwa,Kutokana na mwendelezo wa utoaji wa huduma ya Chanjo ya Uviko 19 kumekuwepo na mwitikio mkubwa  kwa wananchi kupata huduma ya chanjo hiyo na kwamba takribani asilimia 72 ya wananchi wa mkoa wa Geita wamefikiwa na huduma ya chanjo hiyo.

Mmoja wa wananchi akipatiwa Chanjo ya UVIKO 19 

Pia ,Luhangija aliongeza kuwa ,takribani watu 309,699 Wanatarajiwa kufikiwa  na huduma ya chanjo hiyo ifikapo disemba 30,mwaka huu ili kuwakinga dhidi ya virusi vya Ugonjwa wa UVIKO 19.

Ninaendelea kuwahamasisha wananchi wa mkoa wa Geita waendelee kutupa ushirikiano wa kupokea huduma hii ya chanjo ya UVIKO 19,na tunazo timu 549 ambazo zinatoa huduma ya chanjo ,Pia tunatoa wito kwa Viongozi wa Mitaa,Vijiji na Kata pamoja na viongozi wa vyama vya siasa,dini na serikali kushirikiana katika kutoa hamasa kwa wananchi kupokea huduma hiyo”alisema Luhangija.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita,Martine Shigela amewataka wananchi kutopuuza zoezi la utoaji wa huduma ya chanjo hiyo kutokana na serikali kutambua umuhimu wa kuwakinga wananchi wake dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa huo.
Mratibu wa Huduma ya Chanjo Mkoa wa Geita Wille Luhangija.

Nitoe wito kwa wananchi kuwa na ushirikiano wa Kutosha katika kampeni ya utoaji wa huduma ya Chanjo hiyo..Chanjo hiyo haina madhara kwa binadamu,na chanjo hiyo inasaidia kuwakinga na ugonjwa huu hatari wa UVIKO,Rai yangu pia ka viongozi wa maeneo yote na wananchi kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa timu ya watoa huduma”alisema Shigela.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments