![]() |
| Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Ndg Nicolous Kasendamila. |
Na Urban Epimark, GEITA.
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi-CCM pamoja na watendaji wa serikali katika mkoa wa Geita wametakiwa kuelezea kinaga-ubaga uhalisia wa utendaji mzuri wa kazi wa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi huku wakitaja wazi wazi takwimu sahihi za fedha alizoleta na mambo ya maendeleo yaliyo fanyika katika maeneo ya mkoa wa Geita.
Rai hiyo imetolewa leo January 23, 2023 na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Ndugu Nicolaus Kasindamila wakati alipokuwa akifunga kikao cha Halmshauri ya CCM ya wilaya ya Geita na kumpongeza Rais Samia kwa utendaji mzuri wa kazi na imani yake kwa wananchi wa mkoa wa Geita.
"Ndugu zangu wana-CCM katika mkoa wetu wa Geita, hebu elezeeni kwa kina na wazi wazi uhalisia wa utendaji kazi mzuri wa Rais Samia kwa wananchi wetu. Rais Samia ametuletea fedha nyingi tena zaidi ya bajeti za maendeleo zilizoombwa na watendaji serikalini na kuwezesha kutumia fedha ya ziada iliyoletwa kujenga zaidi ya shule mpya 26 za sekondari katika mkoa wetu" alisema Mwenyekiti huyo.
Mbali na agizo hilo, Mwenyekiti huyo aliwataka wana CCM pia kuhakikisha wanawasimamia vizuri watendaji wa serikali katika ngazi zote katika mkoa wa Geita kutekeleza vizuri Ilani ya CCM kwa wananchi kama kilivyo aminiwa na wananchi kuwaweka madarakani na pia kuimarisha mahusiano mazuri na kila mmoja katika jamii.
![]() |
| Wajumbe wa mkutano wa Halmashauri ya CCM katika wilaya ya Geita, wakifuatilia kwa makini taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM (w) Geita katika mkutano huo uliofanyika January 23, 2023. |
Katika hatua nyingine mkutano huo wa Halmashauri ya CCM katika wilaya ya Geita ambao ulikuwa wa kupokea na kujadili utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miezi sita kutokea Julai hadi December 2022, ilitoka na maazimio kadhaa.
Baadhi ya maazimio hayo ni pamoja na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa utendaji kazi mzuri na pia kutoa maelekezo kwa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa yaani NIDA katika mkoa wa Geita, kujiwekea mifumo mizuri ya kuwafikishia wananchi vitambulisho vyao baada ya kukamilika ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Akielezea maazimio ya mkutano huo mbele ya waandishi wa habari, Katibu Mwenezi wa CCM katika wilaya ya Geita Ndugu Gabriel Nyalusi alisema, kikao cha Halmashauri ya CCM wilaya ya Geita kwa umoja wao wameazimia kumpongeza kwa dhati Rais wetu Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa watu wa mkoa wa Geita.
"Ametuletea fedha nyingi za kufanikisha miradi ya maendeleo, tena zaidi ya zile zikizoombwa kwenye bajeti. Ni upendo wake kwa watu wa mkoa wa Geita" akiwaambia waandishi.
Kuhusu maelekezo ya vitambulisho vya uraia, Ndugu Nyalusi alisema, CCM haifurahishwi na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi kuilalamikia NIDA kuhusu vitambulisho hivyo, mkutano huo umeamua kutoa azimio hilo la NIDA kubuni mifumo mizuri ya kufikisha vitambulisho hivyo baada ya kuvikamilisha, alisema.
Mwisho.



_3.jpg)
0 Comments