TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MADIWANI GEITA DC WATAKIWA KUHAMASISHA KIDATO CHA KWANZA KURIPOTI SHULENI.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu.

Na Urban Epimark, NZERA GEITA.

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, mkoani Geita wamehimizwa kuhamasisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2023 wanaripoti kwenye shule walizopangiwa ili lengo la  serikali kutoa elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha Nne  lifikiwe.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Mhe Charles Kazungu wakati akifunga mkutano maalumu wa Bajeti wa Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo leo January 24, 2023 wa kujadili na kupitisha bajeti ya Halmashauri hiyo ya mwaka 2023/2024 kilichofanyika makao makuu ya Halmashauri Nzera, Geita.

"Waheshimiwa madiwani wenzangu, hadi leo January 24, 2023 idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu 2023 asilimia 50% hawajaripoti shuleni. Hili sio jambo zuri kwetu. Natoa wito kwenu nendeni kila mmoja akahamasishe waliopangiwa kujiunga kidato cha kwanza wanaripoti shuleni. Tukasaidiane na viongozi wengine katika kata zetu hadi ifikapo January 30, 2023 wanafunzi wote wawe wameanza masomo yao" alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Pia amewataka madiwani hao wakawaimize viongozi na watendaji wa vijiji katika kata zao kuhakikisha wanaandaa na kuwasilisha kwenye mikutano ya vijiji taarifa za mapato na matumizi ya fedha zilizoletwa na kukusanywa katika vijiji vyao ili kuongeza imani ya wananchi kukipenda chama tawala na kuondoa manun'guniko ya baadhi ya wananchi.

Wajumbe wa mkutano maalumu wa Bajeti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita wakiwa katika mkutano huo uliofanyika leo January 24,2023 katika ukumbi wa mikutano Nzera, Geita DC.

Katika hatua nyingine ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita imekiambia kikao cha Baraza hilo la madiwani kwamba katika kipindi cha mwaka wa bajeti ya serikali cha mwaka 2023/2024 itahakikisha inashughulikia na kuomba bajeti ya ununuzi wa thamani na vifaa vya ofisi ya jengo jipya la Halmashauri hiyo kutoka serikalini ikiwemo ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na ukumbi wa mikutano wa Baraza la Madiwani. 

Hayo yalielezwa na Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Bi Kasinje Bukombe katika kujibu swali kutoka kwa Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Maadili ya Baraza hilo la Madiwani Mhe Elisha Lupuga.

Katika hoja yake, Mhe Lupuga aliomba kujua endapo mpango wa bajeri ya mapato na matumizi ya mwaka mpya wa fedha wa 2023/2024 kama umejumuisha kasma ya ununuzi wa thamani na vifaa vya ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo pamoja na vifaa husika kama komputa wakati Halmashauri itakapo hamia katika ofisi za jengo jipya la Halmashauri. 

Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Bi Kashinje Bukombe (pichani) akitoa ufafanuzi wa bajeti ya ununuzi wa thamani za ofisi mpya ya Halmashauri hiyo kwenye kikao maalumu cha Bajeti ya Baraza la Madiwani uliofanyika Nzera Januari 24, 2023.

Kwa sasa wanatumia ofisi za majengo ya Hospitali ya wilaya hiyo ya Geita iliyopo Nzera.

Kikao hicho kwa kauli moja kilipitisha na kuidhinisha bajeti ya shilingi BIL 87.2/= za kutekeleza mipango ya maendeleo pamoja na matumizi ya kawaida kwenye Halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Mhe Elisha Lupuga (mwenye kaunda suti ya rangi ya khaki) akifuatilia hoja za kikao hicho akiwa na madiwani wengine nyuma yake, leo January 24, 2023.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments