TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

SERIKALI KUBORESHA ELIMU YA AWALI NA LA KWANZA,TRILIONI 1.115 KUBORESHA MADARASA

Mkuu wa Wilaya Bukombe Said Nkumba aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela. 

 Na SALUM MAIGE, GEITA

Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki katika kutoa elimu ya awali kuifanya kuwa ya lazima kwenye sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ili kujumuisha elimu ya awali katika elimu ya msingi kwa kuzitaka shule zote za msingi kuwa na darasa la elimu ya awali kwa watoto chini ya miaka mitano.

Katika kuboresha elimu hiyo,Serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi Trilioni 1.15 kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili kuboresha miundombinu ya madarasa ya  kwanza na awali,ambapo madarasa 900 yatafanyiwa ukarabati ikiwa ni hatua ya kuondoa changamoto za ujifunzaji kwa wanafunzi wa madarasa hayo.

Pia,serikali imeagiza walimu wa darasa la kwanza na awali wanatakiwa kuwa mahili na wenye maadili katika ufundishaji ili kuondoa mtazamo wa jamii kwamba walimu wa madarasa hayo ni wale ambao hawajiwezi hali inayozorotesha ufundishaji.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Elimu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa(TAMISEMI) Vicent Kayombo kwenye kikao kazi cha mapitio ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji  na usimamizi wa elimu kwa mwaka wa 2022 na mpango wa Taifa wa mwaka 2023.

Katika kikao hicho kilichofanyika mjini Geita Januari 19,2023 kimejumuisha Walimu wakuu,wakuu wa shule,waratibu elimu kata,maofisa elimu wilaya na mkoa pamoja na wadhibiti ubora elimu ngazi ya wilaya na mkoa wa Geita ili kupokea maelekezo ya serikali katika kuboresha elimu kuanzia ngazi ya awali.

Walimu wakuu, wakuu wa Shule za sekondari, Maafisa Elimu kata na  Maafisa Elimu Wilaya ndani ya Mkoa wa Geita wakiwa kwenye kikao cha tathimini ya Elimu. 

Kayombo amefafanua kuwa msingi wa elimu ni kuanzia darasa la awali na la kwanza hivyo kasumba iliyojengeka ya kwamba Walimu wa madarasa hayo hawana elimu isiendelee kuwepo na kuagiza kwamba walimu wa madarasa hayo wathaminiwe na kupewa motisha.

“Walimu wa awali hawathaminiwi kabisa hivyo hii leo tunaagiza tuzo zinazotolewa kwa walimu wa madarasa mengine zitolewe pia kwa walimu wa madarasa ya kwanza na awali, pia tunakusudia kuanza kutumia walimu wenye astashahada,stashahada na shahada waanze kufundisha madarasa ya kwanza na awali” anasema Kayombo.

Kadhalika,amesema mwalimu asiende hatua inayofuata ya ufundishaji bila mwanafunzi kujua hatua ya awali hadi ahakikishe mwafunzi amefahamu hatua ya awali ndipo mwalimu aende nae hatua nyingine.

Kiongozi huyo amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika(KKK).

Mwalimu Mashauri Robert  wa shule ya msingi Nyamkanga wilaya ya Chato amesema ili kuwa na elimu bora inatakiwa somo la kiingereza lianze kufundishwa kuanzia darasa la kwanza ili mwanafunzi anapofika darasa la nne aweze kumudu somo hilo.

“Tunapoanza kumfundisha mtoto darasa la tatu somo la kiingereza tunakuwa hatumtendei haki kwani kwa sasa somo hilo linaanza kufundishwa darasa la tatu baada ya mwaka mmoja tu anaingia la nne na kufanya mtihani, kwa hali hii hawezi kufaulu somo hilo”anasema Robert.

Wanafunzi wa darasa la awali. 

Mathias Thomas mzazi wa mwanafunzi Jenifer anayesoma darasa la kwanza shule ya msingi Kukuluma anasema, elimu ya darasa la awali na la kwanza ni kama haitiliwi mkazo na serikali badala yake serikali inahangaika na madarasa ya juu na sekondari.

“Hapa kweli walimu ni wachache sana hasa wa darasa la awali na la kwanza, serikali ingeanza kwenye msingi wa elimu huku chini hata somo la kiingereza lingefundishwa kuanzia awali ili mtoto anapoenda darasa la nne awe na uwezo wa kulimudu somo hilo” anasema Thomas.

Akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela kwenye kikao hicho, Mkuu wa wilaya ya Bukombe Said Nkumba anasema mkoa huo umebaini asilimia 8.93 ya wanafunzi wa darasa la kwanza walikuwa hawamudu stadi darasani.

Amesema, kuja kwa maelekezo na mpango wa serikali wa kuboresha elimu kuanzia ngazi ya awali na msingi itasaidia kuondoa tatizo hilo ambalo linasababisha baadhi ya wanafunzi kufika madarasa ya juu bila kujua kusoma na kuandika.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT – MMMAM),Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia iliripoti upungufu wa asilimia 31.7 ya walimu wa elimu ya awali wenye vigezo katika shule za serikali kutoka walimu 7,861 mwaka 2017 mpaka walimu 5,367 mwaka 2018.

Aidha, uwiano wa wanafunzi na walimu katika mkondo wa elimu ya awali ya shule za serikali iliripotiwa kuwa mwalimu mmoja hufundisha wanafunzi 249 na mwongozo wa kisera wa uwiano ni wanafunzi 25 kwa mwalimu mmoja.

Picha ya Wanafunzi wa darasa la awali. 

Kutokana na hali hiyo wadau wanaotekeleza Programu za Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali(MMMAM) nchini kama vile Children in Crossfire(CiC) na Shirika la kuhudumia watoto Dunia(UNICEF) wameweza kutekeleza program ya mafunzo kwa walimu wa shule za awali waliopo kazini ili kutoa elimu bora kwa watoto katika mazingira yenye watoto wengi wenye uhitaji.

Kwa mujibu wa meneja wa taasisi ya CiC inayotekeleza mradi wa Mtoto kwanza nchini kwenye masuala ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Chiku Lweno ni kwamba mafunzo ya walimu hao yamezingatia sera ya Elimu na mafuzo pamoja na mitaala ya elimu ya awali iliyotolewa na taasisi ya elimu Tanzania ikiwa ni kuhakikisha Mwanafunzi wa darasa la awali anapata malezi na mafunzo bora kulingana na umri wake.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments