![]() |
| Katibu Mkuu - TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe akifungua mafunzo elekezi kwa Maafisa Mipango wa Halmashauri na Sekretarieti za mikoa yanayofanyika mjini Morogoro. |
Urban Epimark - MOROGORO .
Serikali imekipongeza Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kupitia maandiko ya tafiti za wahitimu wake kwa kupendekeza mbinu mbadala za upatikanaji wa vyanzo vipya vya mapato katika Halmashauri na Sekretarieti za mikoa hapa nchini.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe ametoa pongezi hizo leo Januari 30, 2023 katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo Maafisa Mipango wa Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa kuhusu Uandishi wa Miradi ya Kibiashara yanayofanyika kwa juma zima katika Manispaa ya Morogoro.
Mafunzo hayo yaliyoanza Jumatano Januari 25 , 2023 yakishirikisha maafisa mipango kutoka halmashauri 13 na Sekretarieti za Mikoa 12 ya Tanzania Bara yataendelea hadi kuhitimishwa February 03, 2023 yatakapo fungwa na Waziri wa TAMISEMI Mhe Angellah Kariuki.
“Nimefurahishwa kuona kupitia tafiti za Chup cha Mipango na Maendeleo Vijijini mmekuja na suluhisho la uhaba wa vyanzo vya mapato kwenye halmashauri na Sekretarieti za Mikoa na hivyo kuandaa mafunzo elekezi ya namna Halmashauri zetu na Sekretarieti za Mikoa zinavyo weza kuongeza mapato. Niwapongeze sana wote mlioandaa mafunzo haya kwa wataalamu wetu ambayo nategemea yatakuja na matokeo chanya” alieleza Prof. Shemdoe
![]() |
| Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo, wakimsikiliza Katibu Mkuu - TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mafunzo hayo mjini Morogoro leo January 30, 2023 |
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa TAMISEMI Prof. Shemdoe amezitaka Halmashauri zote nchini kuacha kutegemea mazao ya chakula katika ukusanyaji wa mapato badala yake wabuni vyanzo vingine vitakavyo kuwa endelevu.
"Kutumia vizuizi vya barabarani na kutoza kodi mazao ya chakula ni ishara ya kuishiwa mbinu za ukusanyaji wa mapato. Acheni kuwasumbua wananchi, badala yake njooni na vyanzo mbadala na endelevu vya ukusanyaji wa mapato visivyoleta kero" alisisitiza Prof. Shemdoe
Akishiriki hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo kwa njia ya mtandao Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo cha Mipango Profesa Provident Dimoso ameishukuru Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa namna inavyotoa ushirikiano kwa Chuo cha Mipango katika dhima yake ya kutoa huduma kwa jamii.
Aidha, ametoa shukrani kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili wa utafiti na mafunzo hayo na kuahidi kuwa Chuo kitaendelea kufanya kazi kwa weledi ili kutoa huduma inayojibu changamoto za kimaendeleo zinazoikabili jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza Prof. Juvenal Nkonoki akitoa hotuba ya kumkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Chuo Profesa Hozen Mayaya alitoa ombi la mafunzo hayo elekezi kufanyika pia kwa Wenyeviti na Mameya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini mbapo ombi hili lilikubaliwa na serikali.
Akiongea kwa niaba ya washiriki wenzake Bi. Jachinda Chang’a amemshukuru Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutenga muda na kuungana nao katika hafla ya ufunguzi.
![]() |
| Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika kipindi cha majadiliano kwenye mafunzo hayo baada ya kufunguliwa rasmi na Katibu Mkuu- TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe mjini Morogoro leo January 30, 2023 |
"Uwepo wako ni ushahidi tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyo na dhamira thabiti ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu" alisema na kuongeza kwamba Chuo cha Mipango kinaomba amfikishie Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ahadi zao za kufanya kazi kwa bidii ili kumuunga mkono katika utendaji wake.
Mwisho.




0 Comments