MBUNGE Mhe. Dkt. Msukuma akiongea na wavuvi Wa mwaro Wa makatani alipowatembelea kujua kero zao. |
MBUNGE wa jimbo la Geita vijijini Joseph Kasheku Msukuma ameuagiza uongozi wa mwaro wa Makatani uliopo katika kata ya Nkome wilayani Geita kurejesha fedha zaidi ya shilingi laki nne (Tsh.400,000/=) walizochukua kwa baadhi ya wavuvi wa mwaro huo ambazo waliwatoza kama faini ya kuvua dagaa wakati wa giza kinyume cha utaratibu.
Mbunge Dkt Msukuma ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kushitukiza kwenye mwaro huo kisha kuzungumza na wavuvi wa eneo hilo ambapo bila kumung'unya maneno wavuvi hao walimweleza Mbunge wao kuwa uongozi wa kata hiyo wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuwatoza faini zisizo rafiki pasipo hata kuwapatia risti za malipo hayo.
Mhe. Dkt. Msukuma (MB) akizungumza na viongozi wa kata hiyo eneo la mwaro. |
Kufuatia malalamiko hayo Mbunge Msukuma alitaka kupata ufafanuzi kutoka kwa uongozi wa kijiji hicho na kuelezwa kuwa agizo hilo limetoka kwa uongozi wa halmashauri hiyo lengo likiwa ni kuokoa mazalia ya samaki
Mhe. Mbunge Dkt Msukuma akitembelea mwaro huo kujionea hali harisi kabla ya kuongea na wavuvi. |
"Mheshimiwa Mbunge siyo kwamba sisi tumejiamulia kuwakamata hawa wavuvi ni agizo kutoka kwa Mkurugenzi wa halmashauri na lengo ni kufanya samaki wazaliane" alisema mtendaji wa kata ya Nkome John Nzari.
Hata hivyo baada ya maelezo hayo kutoka kwa mtendaji wa kata, Mbunge Msukuma huku akipitia barua iliyotoka kwa Mkurugenzi Wa halmashauri hiyo inayoelekeza utekelezaji wa agizo hilo alihoji iwapo kwenye barua hiyo wameagizwa kuwatoza faini wavuvi hao pasipo kupatiwa risti lakini nakupata majibu yanayojitosheleza.
"Ni kweli hii barua imewaelekeza kukamata wavuvi wanaovua dagaa nyakati za giza lakini ni wapi ambapo imeelekeza muwatoze faini pasipo kuwapatia risti?" alihoji Mbunge Msukuma.
Mhe. Dkt Msukuma Mbunge wa Geita vijijini akizungumza na wananchi ambao ni wavuvi wa samaki Nkome Geita. |
Kufuatia hali hiyo mwenyekiti wa BMU kata hiyo Ntuzu Emmanuel alijitetea kuwa walikuwa na mpango wa kuwaita wavuvi hao ili wawapatie risti zao utetezi ambao pia uligonga mwamba kwa Mbunge huyo na kuamuru pesa hiyo irejeshwe haraka kwa wavuvi hao na iwe mwanzo na mwisho kuwatoza wavuvi hao pesa zao pasipo kuwapatia risti.
"Sasa nisikilizeni naomba pesa uliyochukua kwa wavuvi muirejeshe mara moja na iwe mwanzo na mwisho kuwatoza faini pasipo kuwapatia risti, mnasikia nyie wavuvi msikubali kutoa hela bila kupewa risti hata serikali inasisitiza unapofanya malipo ya aina yoyote ile dai risti" alisema Mbunge Dkt Msukuma huku akipigiwa makofi
Kufuatia hali hiyo uongozi huo wa BMU ulimhakikishia Mbunge Msukuma kuwa pesa yote watairejesha na kwamba suala hilo halitajitokeza tena.
Katika hatua nyingine wavuvi hao walimtaka Mbunge huyo kuondoka na mtendaji wa kijiji hicho Salum Mussa Kapami kwa madai kuwa amekuwa ni mungu mtu.
"Mheshimiwa Mbunge tunaomba uondoke na mtendaji wa kijiji amekuwa mungu mtu tunaomba uondoke naye" alisema Geradi Masaga huku akishangiliwa na wavuvi wenzake.
Aidha akijibu malalamiko hayo Mbunge Msukuma alimtaka mtendaji huyo kujibu hoja za wavuvi hao na kudai kuwa anasingiziwa.
"Ninakuomba ujirekebishe ukiendelea hivyo nitaongea na Mkurugenzi akuondoe maana wameshaondoka watendaji wengi sana hapa ambao hawawez kutatua kero za wananchiiiiiiiiii" alisema MBUNGE MUSUKUMA.
Mwisho.
0 Comments