Na Victor Bariety;
Kwenye siasa za ushindani mara nyingi
mgombea anapokuwa hana mpinzani huwa ana nafasi ya kutulia, akingoja tu siku ya
uchaguzi. Lakini hali ni tofauti kwa Eng. Chacha Mwita Wambura, Mgombea Ubunge
wa Jimbo la Geita Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Pamoja na ukweli
kwamba hakuna chama cha upinzani kilichojitokeza kupambana naye kwenye uchaguzi
wa mwaka huu, bado ameamua kutembea kila kona ya jimbo akisikiliza kero na
changamoto za wananchi wake. Hii ndiyo taswira ya kiongozi anayeamini kwamba
kazi na matokeo havianzi baada ya kuapishwa, bali kabla hata ya kupigiwa kura.
Leo, Septemba 26, Eng. Chacha
alishusha hatua zake katika Soko la Nyankumbu, akiambatana na mgombea udiwani
wa Kata hiyo, Paschal Kimisha Sukambi, na viongozi wengine wa CCM Wilaya ya
Geita. Ziara hiyo imegeuka kuwa kioo cha dhati cha dhamira ya viongozi hawa kwa
wananchi, kwa kuwa haikuishia kwenye mikutano ya kampeni pekee bali ilijikita
kwenye kusikiliza na kuandika moja kwa moja kero zilizowakumba wafanyabiashara
wa eneo hilo.
Miongoni mwa changamoto zilizotolewa
na wafanyabiashara wa Nyankumbu ni pamoja na:
Ukosefu wa maji ya kutosha kwenye vyoo vya soko;
Kukosekana kwa eneo maalum la kushushia mizigo;
Matizo la mitaro ya maji machafu, yanayohatarisha afya na usalama;
Malalamiko juu ya tozo za vizimba
ambazo zinadaiwa kuwa kikwazo kwa wajasiriamali wadogo.
Badala ya kutoa majibu mepesi, Eng. Chacha aliwaeleza wafanyabiashara hao kwamba serikali ya CCM tayari imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha masoko yanakuwa na mazingira bora, salama na yenye tija kwa wafanyabiashara. Aliahidi kuwa, akipewa ridhaa ya kuwatumikia kama Mbunge, atashirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali na taasisi husika kuhakikisha changamoto hizo zinapata suluhisho la kudumu, huku akisisitiza kuwa Soko la Nyankumbu linastahili kuboreshwa kwa viwango bora kulingana na mpango wa kitaifa wa kuboresha masoko.
Lakini picha ya uongozi wa vitendo
haikuishia kwa Eng. Chacha pekee. Paschal Kimisha Sukambi, mgombea udiwani wa
Kata ya Nyankumbu, ameonyesha namna siasa za karibu na wananchi zinavyoweza
kufanyika kwa unyenyekevu. Badala ya mikutano mikubwa pekee, Sukambi amekuwa
akipita nyumba kwa nyumba, akisalimia wakazi wake na kuandika kwenye daftari
maalum kero wanazomweleza. Kauli yake ni rahisi: “Nikitunukiwa udiwani, nataka
nianze kazi nikijua pa kuanzia, kwa sababu changamoto zenu ndizo dira yangu.”
Kwa mtazamo wa wengi, mshindi wa kweli wa uchaguzi si jina litakalotangazwa na Tume ya Uchaguzi, bali ni yule ambaye wananchi wameshajionea kwa macho yao kwamba ana dhamira, uchapa kazi na msukumo wa kuleta matokeo. Na kwa dalili hizi, wakazi wa Geita wanashuhudia taswira hiyo mapema.
Kuna methali isemayo, dalili ya mvua
ni mawingu. Hali ya sasa ya Eng. Chacha na Sukambi ni mawingu yenye mvua ya matumaini.
Wanaonyesha kwamba siasa siyo ahadi za majukwaani pekee, bali ni kusikiliza,
kuandika na kutenda. Wameweka mizizi ya uongozi wa karibu na wananchi kabla
hata ya kupewa dhamana rasmi.
Wananchi wa Geita wanayo nafasi kubwa Oktoba hii ya kuamua mustakabali wa maendeleo yao. Na iwapo watachagua viongozi wanaosimama kwenye msingi wa kazi na matokeo, basi jimbo hili litakuwa darasa la mfano kwa nchi nzima.
Mwisho
Imeandaliwa na Victor Bariety
0757-856284














0 Comments