Na Salum Maige-Geita:
Siku chache baada ya tukio la kusikitisha la mama mzazi Shija Erasto kudai mwanae kufariki kwa uzembe wa watoa huduma katika zahanati ya Kigongo wilayani Chato, serikali imechukua hatua za haraka kwa kufanya mabadiliko ya baadhi ya watendaji wa idara ya afya wilayani humo, akiwemo mganga mkuu wa wilaya ya Chato.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Julai 10, mwaka huu, ambapo Shija alifika zahanati hapo majira ya saa mbili usiku julai 9, usiku wa manane akiwa anatokwa na damu nyingi, huku akiwa katika hatua za mwisho za kujifungua. Inadaiwa kuwa alilazimika kujifungua peke yake baada ya mganga mfawidhi wa zahanati hiyo, Cesilia Katoba, kushindwa kutoa msaada kwa wakati kutokana na uzembe.
Wazazi wa mtoto huyo wamedai kuwa uzembe huo ulianza tangu asubuhi ambapo walikuwa wameomba rufaa kwenda kituo cha afya au hospitali ya wilaya, lakini hawakupata msaada. Mtoto wao alifariki baada ya mganga kutumia muda mrefu kuvaa glavu badala ya kumhudumia mtoto sekunde chache baada ya kuzaliwa.
Kufuatia tukio hilo, idara ya afya ya wilaya na mkoa iliunda kamati ya kuchunguza mkasa huo, ingawa majibu ya kamati hiyo hayakuwekwa wazi. Hatua zilizochukuliwa zilisababisha mganga mfawidhi, Cesilia Katoba, kuhamishwa kutoka zahanati ya Kigongo na kupelekwa zahanati ya Msasa, huku mganga mkuu wa wilaya, Dkt. Eugen Restaisire, nafasi yake ikichukuliwa na Dkt. Aristides Raphael.
Mganga mkuu wa mkoa wa Geita, Dkt. Omar Sukari, alithibitisha mabadiliko hayo, akisema kuwa ni ya kawaida katika sekta ya afya pale panapotokea changamoto kama hizo. Aliongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hatua za kinidhamu zitachukuliwa endapo itabainika mtumishi amehusika moja kwa moja na kifo cha mtoto huyo.
Shija Erasto na mume wake, Austine Warioba, wamesikitishwa na kifo cha mtoto wao, wakimlaumu mganga kwa kutokuwajibika ipasavyo. Warioba alidai kuwa juhudi zao za kuomba rufaa kwenda hospitali ya wilaya ziligonga mwamba kwa kisingizio kuwa gharama za huduma hiyo ni kubwa mno kwao.
Tukio hilo lilibua hisia kali katika jamii ya Kigongo, ambapo wakazi wamekuwa wakilalamikia huduma duni na lugha mbaya kutoka kwa baadhi ya watoa huduma wa zahanati hiyo. Wananchi wamedai kuwa hata wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hulipishwa huduma ambazo zinatakiwa kuwa bure kwa mujibu wa sera ya afya ya Taifa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mganga mkuu wa mkoa wa Geita, Dkt. Omar Sukari, vifo vya wanawake wakati wa kujifungua vimepungua kwa miaka mitatu iliyopita, lakini tukio hili linaonyesha changamoto kubwa katika sekta ya afya, hasa vijijini.

0 Comments