TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WANANCHI WA LUKIRINI WAPONGEZA UTEKELEZAJI WA AHADI ZA MAENDELEO, WAKOSHWA NA KANYASU

 Na; Editha Edward 

 

Wananchi wa mtaa wa Lukirini, kata ya Kalangalala, Geita mjini, wameonyesha furaha na kuridhishwa na juhudi za Mbunge wa jimbo la Geita mjini, Costantine Kanyasu, kwa kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020.

Wakizungumza kwa furaha, wananchi hao wamesema kuwa Kanyasu aliahidi ujenzi wa madarasa, zahanati, vituo vya afya, maji, na miundombinu ya barabara, na ahadi hizo zimetekelezwa kwa wakati. Wameongeza kuwa, kutokana na utekelezaji huo, wanafunzi sasa hawakabiliwi na changamoto zozote kwani  madarasa yaliyokuwa mabovu yamekarabatiwa na madawati yameongezwa.

Mbunge Kanyasu ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na madiwani. Alibainisha kuwa wakati anaingia madarakani, kulikuwa na shule saba za msingi, lakini sasa idadi imeongezeka hadi shule 29. Aidha, shule za sekondari zilizokuwa na kidato cha tano na sita zimeongezeka kutoka mbili hadi saba.

Kuhusu changamoto ya maji, Kanyasu amesema kuwa tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi hivi karibuni kupitia mradi wa ujenzi wa tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 40. Alifafanua kuwa mahitaji ya maji katika mji huo ni lita milioni 16, huku kiasi cha maji kilichopo sasa ni lita milioni nane pekee.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Kalangalala, Prundence Temba, alisemakuwa wamekarabati shule ya sekondari Geita, kujenga jengo la utawala, na kuongeza mabweni katika shule hiyo. Pia, Temba alieleza kuwa walipata kiasi cha shilingi bilioni moja baada ya juhudi za kutafuta fedha na walitumia katika kukarabati madarasa pamoja na kujenga jengo la kuhifadhia maiti, kichomea taka pamoja na ujenzi wa jengo la upasuaji.


Post a Comment

0 Comments