TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

JESHI LA POLISI GEITA LAONGOZA MAANDAMANO YA UZINDUZI WA KAMPENI YA “TUWAAMBIE KABLA HAWAJAHARIBIWA” (KUPINGA UKATILI)

 Na Theresia C Method

Katika juhudi za kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia na watoto mkoani Geita, kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita kamishina msaidizi mwandamizi wa  jeshi hilo Safia Jongo jana Septemba 22, 2024, aliongoza jamii katika maandamano ya amani kuanzia halmashauri ya zamani  Gedeco hadi Shule ya msingi Uwanja kata ya Nyankumbu mjini Geita , kuashiria uzinduzi wa kampeni yenye kauli mbiu “Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa.”

Kampeni hii, inayoratibiwa na Jeshi la Polisi kupitia dawati la Jinsia na watoto nchini ilianza mwezi Julai 2024 na inalenga kuhamasisha jamii kutoa taarifa mapema kuhusu ukatili wa kijinsia na udhalilishaji, huku ikiwapa wanafunzi elimu ya namna ya kujilinda sambamba na elimu ya uzalendo. 


Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo akiongoza maandano ya amani kuelekea uwanjani.

Moja ya makundi yanayolengwa ni wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza, kidato cha tano, na vyuo kutokana na kuwa katika hatari kubwa ya kukumbana na vitendo hivyo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, kamanda Jongo alielezea umuhimu wa kampeni hii kwa mustakabali wa vijana  kabla hawajaharibiwa na kuwaelimisha juu ya athari za ukatili wa kijinsia, na kuwapatia ujuzi wa namna ya kujilinda dhidi ya vitendo hivyo.

''Kampeni  hii ni kwa ajili ya kuwaandaa vijana wa darasa la saba, kidato cha nne na sita na vyuo ambao kwa sehemu kubwa huondoka nyumbani kwao kwenda kupata elimu nje ya maeneo yao, hivyo wakipata elimu itawasaidia kuepukana na vishawishi kutokana na elimu waliyoipata,” alieleza Kamanda  Jongo.

Aidha, Jongo alitoa rai kwa wazazi kuwa makini na malezi ya watoto wao, hasa kuzingatia matumizi yao ya tehama kutokana na watoto kutumia mitandao ya kijamii isiyokuwa na mipaka.

Alisema kuwa, kutokana na kuenea kwa teknolojia, watoto wako kwenye hatari ya kuiga tabia mbaya kupitia mitandao, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa kwao na taifa kwa ujumla.

“Ndugu zangu, tunaona jinsi dunia inavyobadilika kwa kasi. Mmomonyoko wa maadili umeongezeka kutokana na utandawazi; tabia zisizofaa kama ulevi, madawa ya kulevya, na hata kujiingiza katika vikundi vya msimamo mkali zinawaathiri sana watoto na vijana wetu, ni lazima tuwaambie mapema kabla hawajaharibiwa,” alisema Jongo


Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo akitoa wito kwa wazazi  kuzingatia matumizi   bora ya tehama.

Naye mkuu wa mkoa wa Geita, Martine  Shigela aliyekuwa mgeni rasmi  katika uzinduzi huo,alieleza kuwa mabadiliko ya kidigitali yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hivyo kila mmoja anao wajibu wa kushiriki katika  mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na vijana. 

“Maendeleo ya teknolojia yamefanya dunia iwe kama kijiji,Mtoto anaweza kuwa nyumbani, lakini akaingiliana na watu ambao hawapo karibu naye kwa njia ya mtandao,Wazazi, lazima tuwe macho na tuchukue hatua za mapema ili kulinda watoto wetu,” alieleza Shigela.

Shigela alizielekeza ofisi zote kuanzia wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wote kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuendelea kudhibiti matukio ya ukatili katika jamii.

Kampeni ya "Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa" imeungwa mkono na makundi mbalimbali ikiwemo taasisi za serikali na za watu binafsi na wananchi, huku ikiwataka kushirikiana kwa dhati katika kuokoa kizazi kijacho kutokana na hatari zinazoletwa na mmomonyoko wa maadili na vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto.

 


Baadhi ya wanachama wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Geita walioshiriki katika maandamano hayo.

Post a Comment

0 Comments