Na mwandishi wetu,
Beijing,
China – Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) inashiriki
kongamano la 5 la kimataifa la mashirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa,
linaloendelea jijini Beijing, China. Kongamano hili limewakutanisha mamlaka 219
kutoka nchi 121 duniani, likilenga kubadilishana uzoefu na utaalamu katika
jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa.
Kongamano
hili la siku tano limejumuisha warsha ya viongozi wa mamlaka za kuzuia na
kupambana na rushwa (High Level Forum), ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw.
Crispin Francis Chalamila, amewasilisha mada kuhusu “mfumo wa sheria wa
Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa.” katika mada yake, Bw. Chalamila
ameeleza jinsi ambavyo serikali ya Tanzania imekuwa ikijipambanua katika
mapambano dhidi ya rushwa kwa kuimarisha mifumo ya sheria na ya kitaasisi.
Alibainisha uanzishwaji wa divisheni ya mahakama kuu inayoshughulikia masuala
ya rushwa na uhujumu uchumi kuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji
na utawala bora.
TAKUKURU ilipewa nafasi ya pekee kutoa wasilisho, ikiwa ni miongoni mwa nchi 70 zilizoteuliwa kufanya hivyo, ikionesha nafasi ya kipekee ambayo Tanzania inachukua katika mapambano haya ya kimataifa dhidi ya rushwa. GlobE Network, ambao ulianzishwa mwaka 2021, umelenga kuongeza ushirikiano na kubadilishana taarifa, uzoefu, na utaalamu kati ya mamlaka mbalimbali duniani katika kupambana na rushwa. TAKUKURU ilijiunga na mtandao huu mwaka 2022 na imekuwa ikishiriki kikamilifu katika shughuli zake.
Katika
mkutano huo, Bw. Chalamila pia alipata fursa ya kukutana na viongozi wa mamlaka
nyingine za kuzuia na kupambana na rushwa, zikiwemo National Commission of
Supervision (NCS) ya China Beijing, Independent Commission Against Corruption
(ICAC) ya Hong Kong, na National Prosecutions Authority (NPA) ya Afrika Kusini.
Mazungumzo yao yalilenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya mafunzo ya
uchunguzi, ufuatiliaji na urejeshaji wa mali, ushahidi wa kiuchunguzi (forensic
evidence), intelijensia, na utoaji wa elimu kwa umma. Viongozi hawa wamepongeza
juhudi za TAKUKURU na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika nyanja hizo muhimu.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu Bw. Chalamila alikutana na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar, kwa lengo la kujitambulisha na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu mapambano dhidi ya rushwa. Balozi Omar alitumia fursa hiyo kuipongeza TAKUKURU kwa jitihada zake katika kuzuia na kupambana na rushwa na kuhimiza kuendelea kutumia fursa za ushirikiano zilizopo kati ya Tanzania na China kwa manufaa ya taifa.
Mkutano
huu unaonyesha dhamira ya dhati ya TAKUKURU katika kuhakikisha rushwa
inadhibitiwa kwa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kujenga mifumo imara ya
kisheria na kitaasisi. Kwa ushirikiano huu, Tanzania inatarajia kupiga hatua kubwa
zaidi katika mapambano dhidi ya rushwa, hivyo kuleta uwazi na uwajibikaji zaidi
katika uendeshaji wa shughuli za umma na sekta binafsi.
Mwisho.

0 Comments