Na Theresia C Method,
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan leo Septemba 30, 2024 amezindua
Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake) katika kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Hayati Edward Moringe Sokoine alikua na sifa nyingi ambazo zinapaswa kuigwa na viongozi wa sasa na baadaye ikiwemo ya kuwa mwaminifu kwa mamlaka ya uteuzi na wananchi, akisema Sokoine alikua na sifa hiyo na akaaminiwa kuwa Waziri Mkuu katika umri mdogo na kwamba hii inatoa funzo kuwa ukiwa mwadilifu na mchapakazi vyeo vitakufuata ulipo bila kukimbizana navyo.
Akiongea jijini Dar es salaam leo septemba 30,2024 wakati akizindua kitabu cha Sokoine (Maisha na Uongozi wake), Rais Samia amesema "Sokoine alisimama imara katika kipindi ambacho nchi ilikumbwa na changamoto za kiuchumi, uhaba wa chakula, miundombinu duni na changamoto katika sekta za viwanda na afya, akiweka mkazo kuendeleza kilimo".
Sokoine aliongoza vita dhidi ya uhujumu uchumi na madhara yake, japo alifariki kabla ya kuona matokeo yake lakini dhamira yake ilikua wazi, funzo kubwa kabisa la uongozi kutoka kwa Sokoine ni uaminifu, nidhamu, uchapakazi, na hii mimi pamoja na vijana wa leo tunatakiwa kujifunza kwa pamoja.
"Sifa ambazo ningependa kuzisisitiza kwa viongozi kwa sasa na baadaye, Sokoine alikua mwaminifu sana kwa mamlaka yake ya uteuzi na kwa wananchi ndio maana haishangazi kwamba alikasimiwa majukumu mengi na makubwa ikiwemo Waziri Mkuu katika umri mdogo, katika hili tunajifunza kwamba ukiwa mwadilifu na mchapakazi hauna haja ya kukimbizana na vyeo bali vyeo vitakufuata ulipo"
Rais Samia akiwa kwenye picha ya pamoja na wake
wa hayati Edward Moringe Sokoine kabla ya kuzindua Kitabu kinachohusu Maisha na
Uongozi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)
leo tarehe 30 Septemba, 2024
Rais Samia akiwa na Viongozi mbalimbali
waliohudhuria hafla ya Uzinduzi wa Kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine
kinachohusu Maisha na Uongozi wake katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNICC).
Mwisho


0 Comments