TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

AJALI BARABARANI TANZANIA: UKALI WA TAKWIMU, UZITO WA SHERIA NA UHITAJI WA UTEKELEZAJI WA DHATI

 Na Victor Bariety – Geita;


Picha: Ajali  iliyotokea Same hivi karibuni.

Tanzania inaendelea kupigania usalama wa raia wake kila kona ya nchi, lakini vita dhidi ya ajali za barabarani bado ni janga linalotikisa misingi ya maendeleo ya taifa. Mwaka 2024 pekee, ajali 1,735 ziliripotiwa, ambapo 1,198 zilisababisha vifo - idadi inayozidi kugeuza takwimu kuwa machozi, na namba kuwa vilio vya taifa.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, mwaka 2023 ajali zilikuwa 1,733 na ziliua watu 1,118. Hili si jambo la kushabikia. Ni mwangwi wa vilio vya watoto waliofiwa, wake waliopoteza waume, na wazazi waliobeba majeneza ya vijana wao. Ni kashfa ya maendeleo yanayojengwa kwa damu ya roho zisizostahili kufa ghafla barabarani.

Hivi Karibuni ajali kubwa zilizotikisa Taifa; Same, Kilimanjaro: Hasara ya Watu 37 Ndani ya Sekunde Chache

Tarehe 30 Juni 2025, taifa lilishtushwa na tukio la kutisha mkoani Kilimanjaro ambapo watu 37 walifariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa baada ya magari mawili  basi la Channel One na Coaster  kugongana uso kwa uso eneo la Saba Saba, Same Mjini. Baada ya kugongana, magari hayo yalishika moto wakati abiria wakiwa bado ndani.

Kamanda Jeremiah Mkomagi, wa Jeshi la Zimamoto Kilimanjaro, alithibitisha kuwa “moto huo ulishika kwa kasi kabla ya abiria wote kuokolewa.”

 Mateso ya Familia Moja: Simulizi Kutoka Ngusero, Same

Familia ya Mzee Abdallah Kiluvya, mkazi wa Ngusero, Same, imepoteza watu 10 — wakiwemo ndugu wanne wa familia moja na wapangaji sita. Walikuwa njiani kuelekea Moshi kwenye harusi ya ndugu yao katika ukumbi wa Kuringe Hall. Kati yao, asilimia 98 waliteketea kwa moto, hakuna aliyetambulika.

 “Huu ni msiba mkubwa. Tumepoteza ndugu, marafiki na wapangaji wetu katika tukio moja,” alisema Mzee Abdallah kwa sauti ya majonzi.

 Lindi: Lori Lawaangamiza Zaidi ya Watu 10 Usiku

Tarehe 27 Juni 2025, Lori la Specialised Hauliers Ltd lililokuwa likibeba makaa ya mawe liligonga watu zaidi ya 10 eneo la Mtegu, Lindi, saa moja usiku, kwenye mteremko mkali. Kamanda wa Polisi John Imori alieleza kuwa uzito wa mzigo na mwendokasi vilisababisha janga hilo.

 Sumbawanga: Mteremko wa Mlima Ulinji Wapoteza Wengine 6

Watu 6 walipoteza maisha na wengine 21 kujeruhiwa baada ya Toyota Hiace kugongana na bajaji katika mteremko wa Mlima Ulinji. Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, alithibitisha tukio hilo na kuwataka wananchi wawe makini kwenye maeneo hatarishi.

 Sheria Tunayo, Lakini Utekelezaji Ni Dhaifu

Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 imeweka misingi madhubuti ya usimamizi wa vyombo vya moto — lakini utekelezaji wake bado ni changamoto, hasa vijijini na barabara kuu za mikoani. Makosa kama uendeshaji bila leseni, ulevi, mwendokasi, kutofunga mikanda na kupita bila tahadhari yamekuwa janga la kawaida.

Katika kikao cha Machi 10, 2025, Kamishna CP Awadhi Juma Haji alisisitiza matumizi ya teknolojia — kamera za mwendokasi, magari ya doria, na ufuatiliaji wa kila siku — lakini bila dhamira ya utekelezaji, kila kifaa hubaki kuwa chuma kisicho na roho.

Ushuhuda Kutoka Barabarani: Sauti za Walionusurika au Kupoteza

 Suleiman Mawalanga, dereva wa magari madogo:

“Ajali nyingi ni uzembe. Barabara hazina taa wala alama. Hatuhitaji sheria mpya, tunahitaji utekelezaji.”

Tobias Moi, dereva wa basi;“Wamiliki wanatulazimisha tukimbie muda. Serikali iwabane pia.”

Neema Mathis, mfanyabiashara; “Dereva wa bajaji haogopi zebra crossing. Tunahitaji elimu endelevu kila robo mwaka.”

 Halma Juma, mzazi Kigamboni; “Watoto wanavuka bila walinzi. Serikali iweke ‘school crossing guards’.”

Hassan Mbaeuku, bodaboda; “Wengi hatujawahi kuona hata darasa la sheria za barabarani. Mafunzo ya leseni yawe ya lazima"

Reah Kazungu, abiria; “Tukinyamaza, tunahusika. Tuwakemee madereva wazembe.”

 Anni Nyagawa, mwamini; “Tuwe na maombi ya pamoja. Mungu atuepushe na haya majanga.

Goodluck,mjasiriamali; "Kila siku ajali. Same, Sumbawanga, Lindi. Basi jamani, Mungu atutete.”

Muhtasari wa Kisera: Nini Kifanyike Sasa?

 1. Uboreshaji wa Miundombinu:

Taa, alama, ‘speed humps’ na vivuko vya waenda kwa miguu vijengwe maeneo yote hatarishi.

2. Elimu ya Usalama Barabarani:

Kampeni zishuke hadi shule za msingi, makanisa, na masoko. Elimu ya sheria iwe endelevu.

 3. Utekelezaji Mkali na Usio na Upendeleo:

Doria ziongezwe, rushwa ipigwe vita, rekodi za madereva ziwe za kitaifa na ziweze kufuatiliwa kwa haraka.

 4. Maboresho ya Sheria:

Sheria ipitiwe upya kulingana na teknolojia ya kisasa ya magari, na adhabu ziwe kali zaidi kwa makosa yanayojirudia.

 5. Mfumo wa Kidigitali wa Rekodi za Madereva:

Kanzidata ya kitaifa ya madereva ianzishwe ili kudhibiti madereva wahalifu na kufuatilia faini, leseni, ajali na nidhamu.

 Hitimisho: Ajali Siyo Bahati Mbaya. Ni Uzembe Unaoweza Kuzuiwa

Ajali si mapenzi ya Mungu. Ni uzembe unaozuia watu kufika wanapokusudiwa — iwe ni kazini, sokoni au shuleni. Ni janga linalodhoofisha uchumi na kuchoma maisha kwa namna ya kutisha. Tuna sheria. Tuna takwimu. Tuna ushuhuda. Kilichobaki ni utekelezaji wenye dhamira ya kweli.

Kila safari inapoanza, usalama uwe kipaumbele. Kila maisha ni muhimu.”

MWISHO

 

Post a Comment

0 Comments