TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI, AHAMASISHA WANANCHI WA BUKOMBE KUJITOKEZA KWA WINGI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA.

Na Theresia C Method: 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Bukombe, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.

Akizungumza leo tarehe 11 Oktoba, 2024, mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha shule ya msingi Bulangwa, wilaya ya Bukombe, mkoa wa Geita, Dkt. Biteko aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na aliwahimiza wananchi kufanikisha zoezi hilo kwa wakati, akisisitiza umuhimu wa kila mmoja kutumia haki yake ya kidemokrasia. 

Dkt. Biteko alibainisha kuwa zoezi la uandikishaji litaendelea hadi tarehe 20 oktoba, 2024, na wananchi wa Bukombe wanatakiwa kujitokeza kwa wingi, kwani maandalizi yote yamekamilika, "Zoezi hili linaanza leo hadi oktoba 20,2024. Wananchi wa Bulangwa mjitokeze waandikishaji wamejiandaa vizuri na tunataka tuone orodha ya watu  wote ili muda ukifika muweze kupiga kura" aliisema Biteko

Mkuu wa mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kushiriki zoezi hilo, akisema kuwa ameonesha mfano bora kwa wananchi wa Bukombe. "Tuendelee  kuwasihi wananchi kutoka kila kitongoji kujiandikisha katika daftari la mpiga kura kwa kuwa yametengwa maeneo ya kutosha ili kuwawezesha wananchi wote wenye sifa muweze kupata fursa hiyo" alisisitiza Shigella

Naye, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe, Bw. Lutengano Mwalyibwa, alisema kuwa maandalizi ya vituo 348 kwa jimbo hilo yamekamilika, huku matarajio yakiwa ni kuandikisha wananchi 109,124.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa kwenye foleni ya kujiandikisha katika daftari la wapiga kura katika kituo cha kujiandikisha cha shule ya msingi Bulangwa kilichopo wilaya ya Bukombe, mkoni Geita


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa anajiandikisha kwenye daftari la wapiga kura katika kituo cha kujiandikisha cha shule ya msingi Bulangwa kilichopo wilaya ya Bukombe, mkoni Geita

Post a Comment

0 Comments