TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MGOMBEA UDIWANI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KATA YA KALANGALALA, REUBEN EMMANUEL SAGAYIKA, ACHUKUA FOMU


Na Editha Edward-Geita;

 

Picha: Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kalangalala, Reuben Sagayika katikati mwenye shati la mikono mirefu akisalimiana na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi katika ofisi ya Kata ya Kalangalala

Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kalangalala, Reuben Sagayika, amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Udiwani huku akiahidi kuleta maendeleo ya kweli endapo atapewa ridhaa na wananchi.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo katika ofisi ya kata, Sagayika ameleza kuwa dhamira yake kuu ni kushirikiana na wananchi wa Kalangalala na Geita kwa ujumla ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kata hiyo.

“Nashukuru sana Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunipa nafasi hii adhimu ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huu. Naahidi kufanya kazi kwa kushirikiana na wanachama wote pamoja na wananchi wa Geita. Kipaumbele changu siyo kuitwa 'Mheshimiwa', bali ni kutoa huduma kwa nguvu zote na kwa ushirikiano mkubwa na wananchi,” amesema Sangaika.

Ameeleza kuwa, akichaguliwa kuwa Diwani, moja ya vipaumbele vyake ni kusimamia kwa karibu uboreshaji wa miundombinu ya barabara, sekta ya elimu na huduma za afya ili kuhakikisha maisha bora kwa wananchi wa Kata ya Kalangalala.

Aidha, amewataka wananchi waendelee kushirikiana naye katika kuhakikisha kata yao inasonga mbele kimaendeleo, akisisitiza kuwa maendeleo hayataletwa na mtu mmoja bali kwa nguvu ya pamoja.

Sagayika, ambaye aliwasili kuchukua fomu akiwa ameambatana na wanachama wa CCM pamoja na wananchi wa Kata ya Kalangalala, ametumia nafasi hiyo kuwashukuru kwa imani waliyoonyesha kwake na kuwahakikishia kuwa hatowaangusha, bali atafanya kazi kwa weledi, utiifu, na kwa uaminifu mkubwa.

“Imani mliyonipa siichukulii poa, nitaifanya kazi hii kwa moyo mmoja, kwa kusikiliza na kushirikiana na kila mmoja. Kalangalala ni yetu sote, na maendeleo yetu yatatokana na mshikamano wetu,” alihitimisha.

PICHA ZAIDI










Post a Comment

0 Comments