TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

USHOGA NI MATOKEO YA KUPUUZWA KWA MALEZI: TGNP

Na Urban Epimark, DAR ES SALAAM 

Imeelezwa chanzo cha tabia za ushoga au mapenzi ya jinsia moja, sio tabia kutoka kwa mataifa ya kigeni pekee (wazungu) bali pia ni matokeo ya kupuuzwa kwa malezi sahihi katika ngazi ya familia za kiafrika.

Mkufunzi na mshauri wa mambo ya haki za kijinsia kutoka TGNP Bw Deogratus Temba (pichani) akitoa mafunzo kwa wanahabari (hawapo pichani) ukumbi wa chuo kikuu huria cha Tanzania (OUT) makao makuu Kinondoni Dar es Salaam leo machi 23, 2023.

Halikadhalika, baadhi ya tamaduni zetu zinachangia kuchochea tabia za ushoga mfano baadhi ya makabila ya kiafrika yanapo mtahiri kijana, kabla hajaruhusiwa kumwingilia mwanamke au kuoa hulazimishwa kumwingilia mbuzi au punda kwa majaribio kisha kuruhusiwa kuoa.

Hayo yameelezwa leo machi 23, 2023 jijini Dar es Salaam kwenye warsha ya mafunzo kwa wanafunzi wa chuo kikuu huria cha Tanzania, wanao soma kozi ya uandishi wa habari ambao utazingatia usawa wa kijinsia katika uandishi, yaliyo tolewa na TGNP na kuratibiwa na chuo kikuu huria cha Tanzania (OUT).

Sehemu ya picha ya washiriki wa mafunzo ya TGNP yaliyofanyika kwa siku ya kwanza leo machi 23, 2023 ukumbi wa chuo kikuu huria cha Tanzania (OUT), Kinondoni Dar es Salaam. Wa kwanza kulia katika picha ni Mratibu wa mafunzo hayo kutoka OUT ambae pia ni mkufunzi/mhadhiri katika chuo hicho Mr.Vincent Mpepo.

Mkufunzi na mshauri wa mambo ya haki za kijinsia kutoka Tanzania Gender Networking Programme (TGNP) Bw Deogratus Temba aliwaeleza washiriki wa warsha hiyo kwamba, kuibuka kwa vitendo vya ushoga kwenye mataifa ya Afrika kwa sasa, chanzo chake sio wazungu pekee  bali pia ni baadhi ya mila na desturi za makabila yetu ya kiafrika.

"Ukienda vijijini baadhi ya watu wazima wanao jihusisha na malezi au kufundisha watoto wadogo, huwachezea na kuwadhalilisha kimaumbile. Pia baadhi ya makabila wanapo wapeleka jando vijana wa kiume, yaani kuwatahiri huwafanyia majaribio kwa kuwaingilia mbuzi au punda. Tabia kama hizo vijana hukua nazo na kujenga mazoea ya kupenda kuwaingilia wenzao ukubwani" alisema mkufunzi huyo.

Mafunzo hayo yalifanyika pia kwa njia ya "Zoom" ambapo wanafunzi mbalimbali wanao soma uandishi wa habari katika chuo hicho cha OUT kwenye mikoa mingine nchini walishiriki kwenye mafunzo hayo kwa njia hiyo ya mtandao na kutoa maoni na michango yao kuhusu usawa wa kijinsia kwenye uandishi wa habari wenye tija hapa nchini.

Bw Temba ambae kitaaluma ni mwandishi wa habari mbobezi alikuwa akijibu hoja ya mshiriki wa mafunzo hayo kwa njia ya mtandao (video conference) kutoka Ilala jijini Dar es Salaam Bw Athman James aliye taka kujua TGNP inasaidiaje kukabili kuibuka vitendo vya ushoga katika jamii yetu.

Nae mwandishi wa habari za michezo hapa nchini Bi Victoria Mungure alitaka kujua jinsi TGNP inavyo saidia kuondoa tatizo la  kubinywa kwa haki za jinsia ya kike kushiriki katika soka la wanawake huko visiwani Zanzibar ambapo maeneo ya visiwa vya Pemba baadhi ya wasichana hunyimwa kushiriki soka la wanawake na kunyimwa haki hiyo ya kushiriki katika michezo.

Mkufunzi kutoka TGNP (jina halikupatikana mara moja) akielezea kwa washiriki wa mafunzo hayo historia ya kuanzishwa Tanzania Gender Networking Programme (TGNP) hapa nchini, malengo yake na pia sababu za TGNP kuamua kutoa mafunzo ya uandishi wa habari wenye kuzingatia usawa wa jinsia katika uandishi wa habari wa sasa.

Akijibu hoja hiyo Bw Temba alisema, TGNP inachofanya kuondoa tatizo hilo ni kushirikiana na asasi nyingine za kiraia pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini katika maeneo hayo kutoa elimu ya kuzingatia usawa wa kijinsia na kuondoa mfumo dume katika jamii.

Mafunzo hayo yatakayo tolewa kwa siku mbili (Machi 23 na 24)  yana lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wa vyuo vikuu wanao soma uandishi wa habari ili wajiandae kuzingatia jicho la usawa wa jinsia katika uandishi ili baadae waweze kuzingatia usawa kwa makundi yote na kuwezesha kutoa fursa sawa kwa vijana wa kike kushiriki katika mambo ya uongozi na mambo ya kisiasa. 

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ya uandishi wa habari kwa kuzingatia usawa wa kijinsia yaliyotolewa na TGNP Bw Urban Epimark (kushoto) ambae pia ni mwandishi wa habari kupitia magazeti mtandao (Blogs) akichangia mada kwenye mafunzo hayo leo machi 23, 2023. Aliye keti kulia ni Mratibu wa mafunzo hayo kutoka chuo kikuu huria cha Tanzania (Open University of Tanzania - OUT) Bw Vicent Mpepo.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments