Na Theresia Method;
Taasisi ya ICAP, kwa ufadhili wa serikali ya Marekani kupitia
mradi wa CDC na PEPFAR, imekabidhi pikipiki 50 na vifaa tiba joto sita (thermocoagulators)
vya kupima saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake kwa serikali ya mkoa wa
Geita ili kuboresha huduma za afya.
Hafla ya makabidhiano ya vifaa
hivyo imefanyika leo 14 Januari 2025 katika
ofisi za ICAP mjini Geita.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mheshimiwa Martine Shigela ambaye
ni mkuu wa mkoa wa Geita ameishukuru taasisi ya ICAP na serikali ya Marekani kwa msaada wao endelevu katika mapambano dhidi
ya saratani ya shingo ya kizazi na UKIMWI.
"Msaada huu ni muhimu sana katika kuboresha huduma za afya vijijini, na tuna imani kwamba utaongeza kasi ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wanawake," alisema Shigela.
Shigela alisema, hatua hii nimatokeo
ya ushirikiano ambao unafanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
pamoja na serikali ya Marekani hasa katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Naibu Mkurugenzi Mkazi wa ICAP Tanzania Dk. John Kahemele,
alieleza kuwa vifaa hivi ni vya kisasa na vina uwezo wa kutoa matibabu kwa
usahihi zaidi bila kuwa na changamoto yoyote
Alisema katika kipindi cha mwaka jana 2024, jumla ya wanawake
elfu 27 walifikiwa na kwa mwaka huu 2025 malengo ni kuwafikia wanawake elfu 35 huku
wanawake 515 wakipatiwa matibabu ya saratani ya awali ya mlango wa kizazi kwa
mwaka huo wa 2024.
"Teknolojia hii mpya itaongeza uwezo wetu wa kuwahudumia
wanawake wengi zaidi hasa wale walioko maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa
huduma za afya umekuwa changamoto," alisema Dk. Kahemele.
Aidha shughuli hii imeonesha dhamira ya dhati ya ICAP katika kusaidia kupambana na UKIMWI na saratani ya shingo ya kizazi, ikiimarisha huduma za kinga na tiba kwa wanawake. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanawake wanapata huduma bora za afya na kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika.
Kupitia hafla hiyo
kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita kamishina msaidizi mwandamizi wa
polisi Safia Jongo aliiomba taasisi ya ICAP kuongeza nguvu katika upatikanaji
wa usafiri ili kuwawezesha askari wa jeshi la polisi hasa kitengo cha dawati la
jinsia na watoto kuwafikia kwa wakati wahanga wa matukio ya ukatili
Kamanda Jongo
alisema maeneo mengi ya vijijini ufikikaji umekuwa mgumu,hivyo ICAP walichukue suala
hilo kama changamoto inayohitaji ufumbuzi
“Tunawashukuru ICAP
kwa kutoa usafiri huu na vifaa tiba, lakini na mimi pia nitumie nafasi hii
kuwaomba mtuunge mkono katika kupata usafiri wa uhakika kwaajili ya kuwafikia
wahanga wa matukio ya ukatili hususani wale waliopo maneo ya vijijini”.
Alisema Kamanda Jongo
0 Comments