Na mwandishi wetu;
Dkt. Jafari Rajabu Seif amechukua rasmi fomu ya uteuzi kuwania Ubunge wa Jimbo la Busanda kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo Agosti 25,2025, akidhihirisha dhamira yake ya kulihudumia jimbo hilo na kuliletea maendeleo endelevu. Zoezi hilo limefanyika katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nzera, chini ya usimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Katika tukio hilo lililojawa na
shamrashamra na hamasa kubwa, Dkt. Jafari ameambatana na viongozi wa CCM, mke
wake, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na umati mkubwa wa wanachama wa chama
hicho. Pia amesindikizwa na vijana waendesha pikipiki (bodaboda), ambao wamejitokeza
kwa wingi kuonesha mshikamano na kumuunga mkono.
Picha: Baadhi ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wakimsindikiza Dkt. Jafari Rajabu Seif kuchukua fomu
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Dkt. Jafari ametoa wito kwa wananchi wa Busanda kushikamana naye katika kuendeleza juhudi za chama, akisisitiza kuwa mafanikio ya jimbo hilo yatatokana na mshikamano na ushirikiano wa karibu kati ya kiongozi na wananchi.
“Ninawaomba tushirikiane kuipeperusha bendera ya CCM kwa nguvu zote. Ushindi wetu ni wa pamoja, na naamini kwa umoja wetu tutaweza kuleta mabadiliko chanya katika kata zote 11 za Jimbo la Busanda. Nitahakikisha kunakuwa na mawasiliano ya karibu kati ya mwakilishi na wananchi ili kuharakisha maendeleo,” amesisitiza Dkt. Jafari.
Ameongeza kuwa mojawapo ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo ndani ya jimbo hilo, huku akisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wakazi wa Busanda.
Kwa upande wao, vijana waendesha
bodaboda wameonesha imani kubwa kwa Dkt. Jafari, wakimwelezea kama kiongozi
mwenye dira, anayefahamu changamoto zao na aliye tayari kuzitatua.
“Tuna imani naye na tunaamini atatufanyia kazi nzuri. Sisi kama bodaboda tumepata mtu sahihi,” amesema Yusufu Emanuel, mmoja wa waendesha bodaboda waliohudhuria.
0 Comments