Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita imemhukumu
Afisa Tabibu wa kituo cha Afya cha Katoro wilayani Geita kwa makosa
ya kuomba na kupokea Rushwa ya shilingi Elfu 30 kinyume na kifungu
cha 15 cha Sheria Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 .
Aliyehukumiwa kwenda jela baada ya kutiwa
hatiani na mahakama ni Samson Lameck Kuzenza aliyekuwa Afisa Tabibu
kituo cha Afya katoro katika kesi Namba 402/2019 iliyokuwa
ikisikilzwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu mkazi Geita, Mheshimiwa . Obadia Bwegoge alisema
Mshtakiwa amepatikana na hatia katika makosa yote mawili ya Kuomba na Kupokea
Rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
Na. 11/2007 na kwamba atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.
Mheshimiwa Hakimu Obadia Bwegoge alifafanua
kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa
TAKUKURU Augustino Mtaki umethibitisha pasipo kuacha shaka kwamba
Mshtakiwa Samson Lameck Kuzenza akiwa Afisa Tabibu alitenda kosa
hilo mnamo tarehe 07 Desemba 2019 akiwa katika Kituo cha Afya cha Katoro.
Mheshimiwa Bwegoge alibainisha
kwamba kwa mjibu wa ushahidi, Mtuhumiwa baada ya kuomba fedha hizo hakumhudumia
mgonjwa mpaka alipozidiwa ndipo alipomhudumia kwa masharti kwamba asingemruhusu
kutoka kituoni hapo mpaka atoe fedha hizo na kwamba huduma ya mama wajawazito
hutolewa bure hivyo utozaji wa fedha hizo ni Rushwa na kwa kuzingatia
ushahidi wa wa pande zote mbili akaamuru mshtakiwa kwenda jela
miaka mitatu kwa kila kosa na kutupilia mbali utetezi wake wa kuomba
kuonewa huruma .
Awali mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Augustino
Mtaki akiuongoza upande wa jamhuri aliiambia Mahakama kuwa
Mshtakiwa Samson Lameck Kuzenza ambaye alikana mashtaka
kuhusika baada ya kuosomewa mahakamani hapo anadaiwa kutenda kosa
hilo Desemba 7 mwaka 2019 kwa muomba Rushwa ya Shilingi 30,000/= Bwana
Said Kulwa Msuluzya ili amfanyie usafi mke wake ambaye ni Bi.Sheha
Hashim Hussein aliyepata tatizo la kuharibikiwa mimba.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita Leonidas
Felix kwa njia ya simu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wa
umma na wananchi katika kukemea vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
0 Comments