TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

RPC JONGO AUAMINISHA UMMA GEITA, UWEZO WA MWANAMKE


Picha: Kamanda wa polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo akiwa katika sherehe ya mtandao wa polisi wanawake mkoa wa Geita, uwanja wa CCM Kalangalala


Na Samwel Masunzu;


Ni dhahiri kuwa jamii imekuwa na dhana ya kutokumwamini mwanamke katika masuala ya usimamizi na utawala kwa kuamini kuwa huenda usimamizi huo ukawa batili hasa katika maeneo yanayohitaji nguvu zaidi


Jambo hili linazidi kupungua kutokana na elimu ambayo inaendelea kutolewa kwa jamii na wanawake wanaopata nafasi za kiuongozi kuzitendea haki nafasi zao sawa na ambavyo wanaume wamekuwa wakifanya


Tafsiri ya moja kwa moja inaonekana hasa baada ya Dkt. Samia Suluhu Hassan (mwanamke) kuapishwa kuwa Rais wa jamhuri ya muunganoTanzania katika kundi la wanawake na wanaume ambao baadhi yao walionyesha kutokuwa na imani naye katika siku za awali za utawala wake mwaka 2021 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati Dkt. John Pombe Magufuli


Kuapishwa kwa Dkt. Samia Suluhu Hassana kuliwapa nguvu kubwa ya kujiamini wanawake ambao walikuwa katika kundi la wenye uwezo wa kufanya kazi na maamzi sawa na wanaume


Kupitia sherehe ya mtandao wa polisi wanawake machi 15, 2025 mkoani Geita , kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo alieleza kuwa , katika suala la ulinzi polisi wanawake walikuwa hawaaminiwi hasa katika misafara ambayo wao walikuwa hawapewi vipaumbele hatika nafasi hizo


Kamanda alieleza kuwa, hapo awali kabla ya mwaka 2007 ambapo polisi wanawake waliunda mtandao wa polisi wanawake, ubaguzi ulikuwa ni mkubwa


Alisema waliamua kuunda mtandao huo ili kuweka usawa na mabadiriko yalianza kuonekana na wakati huo kamanda mwanamke alikuwa ni mmoja lakini kwa sasa makanda wapo 5 na wakuu wa vikosi wawili, DCP 8 na SACP wapo wengi tofauti na awali


Katika sherehe hiyo alisema wakati anafika Geita alikuta matukio mengi ya ukatili na mauaji na kuanza kuweka mikakati ya kudhibiti matukio hayo


Alisema kwa mwaka 2023 matukio ya mauaji ya wanawake yatokanayo na wivu wa kimapenzi yalikuwa 37 lakini hadi kufikia mwaka 2024 disemba, matukio ya mauaji ya wanawake yamepungua na kufikia matukio 7


Aidha alisema katika matukio ya ukatili kwa ujumla, yalikuwa matukio 95 kwa mwaka 2023 na kufikia disemba 2024 matukio hayo yamepungua na kufikia matukio 53 jambo ambalo alisema ni zaidi ya asilimia 50 ya udhibiti wa matukio hayo


“Matukio ya ukatili yalikuwa yamekithiri mkoani Geita, lakni kwa ushirikiano wa jamii na mikakati yetu kupitia dawati la jinsia na watoto tumefanikiwa kudhibiti matukio hayo, japo bado yapo lakini nawahakikishia matukio hayo yatakomeshwa na Geita bila ukatili inawezekana”. Alisema kamanda Jongo.

Kamanda Jongo amewahi kunukuliwa akieleza kuwa, jeshi la polisi mkoa wa Geita liliwahi kutumia vikosi kutoka nje ya mkoa ili kudhibiti kundi la uharifu maarufu kama MAZOMBI ambalo liliibuka kwenye mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita na kundi hilo lilidhibitiwa na hali ikawa shwari

Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela akiwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo ya mtandao wa polisi wanawake mkoa wa Geita alieleza kuwa matuko mengi yakiwemo ya wizi wa mifugo (ng’ombe) amedhibitiwa na kamanda Jongo na changamoto zilizokuwepo kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini nazo zimedhibitiwa

Shigela alisema uwezo wa mwanamke hasa baada ya kupewa nafasi ni mkubwa hata kuzidi baadhi ya wanaume

“Wapo baadhi ya wanaume wapo hapa lakini uwezo wao ni mdogo kuliko wanawake, hivyo tusimtathimini mtu kwa kuangalia jinsi yake bali tumtathimini kwa utendajikazi wake, alisema Shigela.

Picha: Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe: Martine Shigela 


Baadhi ya wanawake waliohudhuria sherehe hiyo ambao ni Rosemary Paulo na Shukurani Sebastian katika mazungumzo nao walisema ili kuweka usawa katika majukumu, kuna haja ya jamii kuondokana na dhana potofu kuwa wanawake hawawezi na kujenga imani kwao sambamba na elimu kuendelea kutolewa

Walisema wanalipongeza jeshi la polisi mkoa wa Geita kwa kuendelea kutoa elimu katika jamii juu ya kutambua nafasi ya mwanamke na matokeo yake jamii imeendelea kuelimika.

Aidha katika sherehe hiyo polisi wanawake waliopo katika kikosi cha kutuliza ghasia FFU mkoa wa Geita walionyeha uwezo wao kwa kufanya onyesho la utayari hasa yanapotokea machafuko na walisema wapo tayari muda wowote kukabiliana na uharifu wa aina yoyote.




 

Picha: Polisi wanawake kutoka kikosi cha kutuliza ghasia FFU mkoa wa Geita wakionyesha mafunzo ya utayari ya kukabiliana na adui.



 Mwisho . 

Post a Comment

0 Comments