Afisa Vipimo Mkoa wa Geita akitoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Vipimo kwa Wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Vipimo kwenye maonesho ya Madini. |
Wakala wa Vipimo (WMA) inawakaribisha wananchi wote wa Geita na Mikoa yote ya karibu kuhudhuria katika maonesho ya nne ya Teknolojia na uwekezaji katika sekta ya Madini ambayo yanafanyika katika viwanja vya EPZ bomba mbili mjini Geita. Lengo kuu la Wakala wa Vipimo kushiriki katika maonesho haya ni kuwapa elimu Wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia Vipimo sahihi pamoja na kuhabarisha Umma kuhusu majukumu ya Wakala wa Vipimo katika sekta mbalimbali hususani ya Madini.
Akizungumza kwenye maonesho hayo Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Geita BW. Moses Ntungi amesema, Serikali inaendelea kuiwezesha Taasisi ya Wakala wa Vipimo kwa kuinunulia vitendea kazi vya kisasa kama vile mizani ya kupimia uzito wa madini pamoja na mawe maalumu (standards) zinazotumika kuhakikia mizani katika masoko ya madini na maduka ya kuuzia vito mbalimbali. Wakala wa Vipimo kupitia ofisi zake zote Tanzania Bara hufanya uhakiki wa Vipimo kwenye masoko ya madini na maduka ya kuuzia vito lakini kwa Mkoa wa Geita Wakala imefanya uhakiki wa Vipimo katika masoko tisa kumi (10) ya kuuzia na kununulia dhahabu ambayo ni Geita mjini, Katoro, Chato, Lwamgasa, Nyarugusu, Mbogwe, Bukombe, Nyang’wale, Nyakagwe na Plant and Elution.
Afisa Vipimo Mkoa wa Geita akihakiki mizani kwenye Soko kuu la Dhahabu Geita |
Meneja Ntungi amesema kuwa, Wakala wa Vipimo inamchango mkubwa sana katika sekta ya madini ambapo biashara hiyo haiwezi kufanyika bila kuwa na mizani sahihi na iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuweza kutambua uzito halisi wa dhahabu inayonunuliwa au kuuzwa. Jukumu kuu la Wakala wa Vipimo katika sekta hii ni kuhakikisha mizani yote inayotumika kuuzia na kununulia vito na madini inahakikiwa na inapima madini kwa usahihi na pia Taasisi hiyo inahakikisha inatoa ushauri wa kitaalamu juu ya mizani zinazopaswa kutumika kuuzia madini kwa kuwa siyo mizani yote inastahili kutumika kuuzia na kununulia madini.
Pia, ameeleza kuwa mara baada ya uhakiki wa mizani hiyo kukamilika na kuanza kutumika Wakala wa Vipimo hufanya zoezi la ukaguzi wa kushtukiza ili kuhakikisha Vipimo vinatumika kwa usahihi kama inavyopaswa. Mara baada ya kipimo kuhakikiwa na kubainika kipo sawa huwekewa alama maalumu (sticker) ya Wakala wa Vipimo ambayo husaidia kutambua kuwa kipimo kimehakikiwa na kinafaa kutumika kununulia madini na vito vya thamani. Aidha, alama zinazowekwa katika mizani iliyohakikiwa ni hiyo stika pamoja na muhuri (stamp) ambayo inakuwa na alama ya nembo ya taifa pamoja na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano (21) ikiashiria imehakikiwa 2021.
Vilevile, ameeleza kuwa lengo na dhumuni la Wakala wa Vipimo kufanya uhakiki wa mizani ya kuuzia na kununulia madini ni kuhakikisha matumizi ya mizani sahihi iliyohakikiwa yanazingatiwa matakwa ya Sheria ya Vipimo na kunakuwa na biashara ya usawa ambapo itawezesha Serikali kukusanya mapato kwa usahihi na wauzaji wa madini wanapata fedha stahiki kulingana na thamani ya madini wanayouza. Kadhalika, mara baada ya uhakiki wa mizani inayotumika kuuza na kununulia madini Wakala wa Vipimo hufanya kaguzi za kushtukiza mara kwa mara katika masoko ya kuuzia madini ili kujiridhisha kama mizani bado ipo sahihi na inaendelea kutumika kwa usahihi kama inavyostahili.
Dhahabu ikipimwa kwenye mzani uliohakikiwa na Wakala wa Vipimo |
Wakala wa Vipimo inatoa wito kwa wafanyabiashara kutojihusisha na vitendo vya uchezeaji wa vipimo kwa lengo la kutaka kujipatia faida zaidi kwani kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 ambayo inaeleza adhabu kwa mtu atakaye kutwa amechezea vipimo ni faini isiyopungua shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi millioni ishirini (20,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote pamoja faini na kifungo kwa kosa. Hivyo, wito umetolewa kwa watumiaji wote wa vipimo kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na wananchi kutembelea ofisi za Wakala wa Vipimo zilizopo katika mikoa yote Tanzania Bara kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu vipimo au kutoa maoni na kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha utoaji huduma wa taasisi hiyo.
Pia, wananchi wanakaribishwa kutumia namba ya simu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97 endapo watakumbana na changamoto yeyote ya kivipimo na kitaalamu ili iweze kufanyiwa kazi kwa wakati.
0 Comments