Picha inayoonesha aina mbali mbali ya vyakula na matunda kwaajili ya lishe bora na Afya imara kwa watu wa rika zote hususan watoto wadogo. |
Salum Maige, Geita.
Wakazi wa Mkoa wa Geita wametakiwa kutumia chakula walichonacho kuwahudumia watoto ili kukabiliana na tatizo la udumavu na utapiamlo.
Afisa lishe mkoa wa Geita Riziki Mbilinyi alisema kuendelea kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu katika mkoa huo ni kutokana na wazazi kutozingatia ulishaji wa chakula kwa watoto.
Alisema kuwa katika Mkoa wa Geita udumavu unaonyesha ni asilimia 38.9 ambapo ni upungufu kutoka asilimia 41.2 za mwaka 2018/19.
Kauli hiyo ya Afisa lishe inakuja siku chache baada ya Tanzania kuungana na nchi wanachama wa shirika la chakula na kilimo duniani (FAO) kuadhimisha siku ya chakula Oktoba 16, 2021 ambapo hapa nchini maadhimisho hayo yalifanyika mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Mbilinyi alisema mkoa wa Geita bado unakabiliwa na udumavu kwa kiasi kikubwa kutokana na wazazi kushindwa kuzingatia ulishaji wa chakula bora kwa watoto.
“Suala la ulishaji watoto ni tatizo linachangia sana udumavu..unakuta mzazi mtoto anampatia chakula mara mbili kwa siku ilihali mtoto anatakiwa kupatiwa chakula mara kwa mara kutokana na matumbo yao kuwa bado hayajakomaa au ni madogo” alisema Mbilinyi.
Akizungumzia suala la ulishaji wa mlo kamili kwa watoto wadogo wadogo hasa chini ya miaka mitano ni asilimia 56.6, huku watoto wengine wakiwa hawapatiwi mlo kamili katika familia zao.
“Pamoja na kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, mikutano na waelimishaji ngazi ya jamii kuhusu jamii kuzingatia suala la ulishaji wa mlo kamili kwa watoto, wananchi wanatakiwa kutambua kuwa mtoto kumpatia chakula cha kutosha ni kumwongezea kinga thabiti ya mwili ili asishambuliwe na maradhi” alisema Mbilinyi.
Aisha Mohamedi aliulizwa sababu za baadhi ya wazazi na walezi kutozingatia ulishaji wa watoto na kusababisha udumavu na utapiamlo ni badhi ya familia kushindwa kuzingatia uzazi wa mpango na hivyo kujikuta wana watoto wengi ambao wanashindwa kuwahudumia inavyotakiwa.
“Ukiwa na watoto wengi kuwatunza ni kazi wanahitaji kula,kuvaa,kupata matibabu,sasa ..hapa lazima ukose namna ya kuwatunza na unakuta kipato chako kidogo” alisema Aisha.
Peter Mathayo alisema elimu ya uzazi wa mpango na namna ya kuwatunza watoto kwa kuwapatia mahitaji yao yote ikiwemo kuzingatia suala zima la ulishaji wa chakula bora hutolewa na watoa huduma wakati wa kuhudhuria kliniki.
Aidha maadhimisho ya chakula Duniani mwaka huu na kufanyika katika viwanja vya Pasua mkoani Kilimanjaro yaliambatana na kauli mbiu isemayo “Kesho Njema inajengwa na Lishe bora Endelevu”.
Chimbuko la maadhimisho hayo ya chakula ni mkutano wa mwaka 1979 ambapo nchi wanachama wa shirika la FAO walikutana na jijini Quebec nchini Canada na kujadiliana masuala yahusuyo chakula, kutathimini na kuweka mikakati ya upatikanaji wa chakula cha kutosha, salama, na chenye virutubisho kwa watu wote hasa watoto wadogo ambao hukabiliwa na maradhi.
Kwa Mujibu wa Waziri wa Kilimo Prof.Adolfu Mkenda alisema tathimini iliyofanywa hivi karibuni inaonyesha kuwa hali ya uzalishaji chakula kitaifa kwa mwaka 2021/22 umefikia Tani 18,425,250 ikiwa ni ongezeko la tani 1,903,096 sawa na asilimia 10.05.
Hata hivyo, Prof Mkenda alitaja mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi lakini inakabiliwa na udumavu ni pamoja na mkoa wa Njombe asilimia 53.6, Rukwa asilimia 47.9, Iringa asilimia 47.1, Songwe asilimia 43.3, Kigoma 42.3 na Ruvuma ni asilimia 41.0.
MWISHO.
0 Comments