Na; Beatus Bihigi - Mtwara.
Mkuu wa Shule ya sekondari Mndumbwe Mwl. Ntarisa K. Ntarisa ametoa zawadi mbali mbali kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na tatu waliofanya vizuri sana katika mtihani wao wa kuhitimisha muhula wa pili wa masomo shuleni hapo kwa mwaka 2024.
Mkuu huyo wa shule ambaye pia ni naibu katibu TAHOSA wilaya ya Tandahimba ametoa zawadi ya madaftari makubwa, kalamu, rula, vitambaa vya kushona nguo hususani sare za shule hiyo pamoja na fedha taslimu Tsh. 10,000/= kwa wanafunzi wote waliopata ufaulu wa daraja la kwanza (Division One).
Mwl.Ntarisa aliwaeleza walimu na Wanafunzi wa shule hiyo kuwa huo ni mwanzo tu, ataendelea kutoa zawadi kedekede kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri shuleni hapo.
Aidha akizungumza na walimu pekee Ofisini kwake amewahakikishia kuwa walimu wote wanaofanya kazi kwa kujituma hatawaacha bila kuwapongeza, ambapo kwa walimu waliojitolea kufundisha wakati wa likizo fupi Septemba 2024 amewazawadia kiasi cha fedha Tsh. 50,000/= kila mmoja kama motisha.
Wakwanza kushoto ni Ntarisa K. Ntarisa Mkuu wa shule ya sekondari Mndumbwe Tandahimba Mtwara akiwa na Mathayo M. Kwaslema Mwalimu wa taaluma katika kikao cha kufunga shule leo 06/12/2024 |
"Niwaombe ndugu walimu wenzangu tuendelee kushirikiana katika shughuli zote za ndani na nje ya darasa kwa ustawi wa Mndumbwe, jamii na taifa kwa ujumla " alisisitiza Mkuu huyo wa shule.
Nao walimu walipata fursa ya kuwaasa Wanafunzi na kuwatakia likizo njema hadi hapo shule itakapofunguliwa mapema Januari 13, 2025.
Walimu na Wanafunzi shule ya sekondari Mndumbwe wakiwa kwenye hafla ya utoaji wa zawadi kuhitimisha muhula wa pili wa masomo kwa mwaka 2024. |
GPC blog alipata wasaa wa kuzungumza na baadhi ya wananchi na wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule ya sekondari Mndumbwe juu ya zawadi walizopata Wanafunzi ambapo walimpongeza Mkuu wa shule hiyo Bw. Ntarisa kwa zawadi nyingi hasa zawadi ya vitambaa vya kushona sare za shule na fedha na kusema wakuu wa shule kama Ntarisa ni mfano wa kuigwa ili kuchochea na kuleta hamasa kitaaluma mashuleni.
Mwisho.
0 Comments