TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WAJAWAZITO 739 WAGUNDULIKA KUAMBUKIZWA V.V.U MKOANI GEITA NDANI YA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA 2021

Katika picha ni akinamama wajawazito mkoani Geita wakipata huduma ya vipimo vya afya wakati wa kuhudhuria kliniki ya wamama wajawazito  kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Disemba 2021

 Na; Salum Maige, Geita
Disemba mosi ya Kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani ikiwa lengo ni kutafakari hali halisi na mwelekeo wa mapambano dhidi ya janga hilo Duniani kote kwa wadau na makundi kuunganisha nguvu.

Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo jumla ya akina mama wajawazito 739 wapimwa na kugundulika kuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (V.V.U)mkoani Geita katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Disemba mwaka huu 2021.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya utekelezaji wa shughuli za mapambano dhidi ya Ukimwi katika mkoa wa Geita ni kwamba idadi hiyo ni sawa na asilimia sifuri nukta saba (0.7%) kwa wajawazito waliopatiwa huduma ya vipimo vya Ukimwi.
Hayo yalibainishwa na afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Geita Elikana Haruna, kwenye Maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo hufanyika Disemba 1 kila mwaka, ambapo katika mkoa wa  Geita yalifanyika wilaya ya Bukombe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama vya siasa.

Akisoma taarifa ya maambukizi ya Ukimwi Bw.Haruna alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Disemba mwaka huu jumla ya wajawazito 107,961 walipatiwa huduma ya ushauri  na kupimwa Virusi vya Ukimwi katika kuanza hudhurio la kwanza la kliniki.

Alisema kati ya idadi hiyo wajawazito 739 sawa na asilimia 0.7% walibainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na kuanzishiwa dawa ya kufubaza virusi hivyo pamoja na dawa za kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto aliyeko tumboni.

Aidha, katika kupambana na janga la Ukimwi hasa kundi la watoto, alisema katika kutekeleza mapambano ya tatizo hilo hasa kwa kundi la watoto, kupitia TACAIDS jumla ya walimu 532 kutoka shule za msingi 377 na jumla ya walimu 390 kutoka shule za sekondari 84 wamepatiwa elimu ya uzazi, malezi na makuzi kwa watoto.

Kwa upande wake mgeni Rasmi katika Madhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bi. Rosemary Senyamule alisema katika kukabiliana na maambukizi hayo, jamii inatakiwa kubadilika katika malezi na makuzi ya watoto ili kuwajengea kuwa na tabia njema.

Alisema tabia mbaya nayo inachangia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (V.V.U) kwa kuwa watoto wengi wanakosa malezi mazuri tangu wakiwa wadogo hadi wanakua na hivyo kusababisha kujiingiza kwenye mapenzi wakiwa wadogo, wenye wake au waume kujihusisha na mapenzi nje ya ndoa zao.

Aidha, alisema serikali ya mkoa wake itaendelea kutoa huduma kwa wajawazito na watoto wanaogundulika kuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (V.V.U) kwa kutoa dawa za kufubaza Virusi Vya Ukimwi na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Maadhimisho ya mwaka huu 2021 yalienda sambamba na Kauli mbiu isemayo "Zingatia Usawa,Tokomeza UKIMWI,Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko"

Post a Comment

0 Comments